Tiketi kielektroniki zianze kimaridhiano

06Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tiketi kielektroniki zianze kimaridhiano

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafirishaji Nchi Kavu (LATRA) imeagiza mabasi ya wasafirishaji abiria kuanza kutoa huduma ya kuuza tiketi kwa mfumo wa kielektroniki, kuanzia jana.

Hilo ni jambo jema linalorahisisha na kuwawezesha wananchi kununua tiketi kwa urahisi na kupunguza usumbufu, gharama za kuzifuatilia pamoja na kuepusha kuibiwa hasa kwa wageni wanaozifuatilia tiketi hizo vituoni.

Lakini ni jambo jema pia kudhibiti uhalifu hasa unaotokana na ulanguzi wa tiketi hizo unaotokea msimu wa sikukuu hasa za mwisho wa mwaka ikiwamo na Noeli pia na hata kipindi cha Pasaka ambacho baadhi ya watu hupenda kurudi nyumbani kusherehekea na familia zao.

Kusisitiza uwepo wa tiketi za kielektroniki ni mwendelezo wa mipango ya serikali ya kuboresha sekta ya usafirishaji na kuifanya pia ichangie kwenye uchumi wa nchi kwa kupanua wigo wa vyanzo vya mapato, ikikumbukwa kuwa serikali imeanza na kukatisha tiketi kielektroniki kwenye usafiri wa treni.

Tunaipongeza serikali kwa mipango ya kupunguza adha wanayoipata wakazi wa maeneo mbalimbali hasa wa mbali na stesheni au mawakala wa tiketi ambao wanahitaji kupata huduma hiyo hivyo kuufanya uuzaji wa tiketi kuwa rahisi na unaopatikana kwa wakati, lakini ni jambo ambalo linahitaji maandalizi zaidi na ushiriki wa pande zote wadau wa usafirishaji, LATRA, Mamlaka ya Mapato (TRA), mawakala, abiria na wenye kutoa huduma za mtandao.

Anawezekana utaratibu huo unakuwa na changamoto zake kwa kusababisha wasafirishaji hawajaridhika na pia hakujawa na maelekezo ya kutosha kutoka pande zinazosimamia mapato hasa TRA na LATRA, hivyo ni vyema kuangalia upya utaratibu huo na kuufanyia kazi kikamilifu ili kuziridhisha pande zinazohusika ili kuepusha wenye mabasi kugoma na kuhatarisha abiria kukwama au kulala vituoni kutokana na kukosa magari.

Tunaona kuwa ni vyema kutoa huduma hizo kwa hatua na uanzishaji wa mfumo wa mabasi kwa njia ya tiketi za mtandao utengenezwe kwa namna ambayo pande zote zitanufaika kwa sababu kuendesha huduma ya usafiri nako kuna gharama kubwa na wakati mwingine wahusika wanaweza kupata changamoto ya idadi ndogo ya wasafiri kwa vile si wakati wote watu hutumia vyombo hivyo.

Licha ya LATRA kuwa na nia njema ya kuanza kutekeleza agizo hilo kwa mabasi yakiwamo yanayosafiri kati ya Dar, Tanga, Lindi na Tanga hadi Arusha, msimu huu unaweza kuwatatiza wanafunzi wanaorudi shuleni.

Lakini, pia bila kuwa na utaratibu unaoeleweka na kukubalika kuna uwezekano wa mamia ya abiria walioko mikoani kukwama kurejea kazini hasa wanaosafiri kati ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Tanga na Dar es Salaam.

Kabla ya kuingia kwenye mkwamo ni wakati wa wadau wakiwamo wamiliki, watoa huduma za mitandao, TRA, LATRA na wengine kusikilizana, kutoa na kusikiliza maoni ya pande zote na kuanza utaratibu mpya baada ya makubaliano.

Tunawakumbusha wasafirishaji kuwa hawana sababu ya kuhofia usafirishaji unaotumia njia za kielektroniki kwa vile zama hizi kila jambo linafanywa kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Tunawakumbusha watoa huduma kuwa ni wakati muafaka wa kujipanga na kuanza kazi, ikizingatiwa kuwa kama LATRA, ilivyoeleza, stendi mpya ya Mbezi jijini Dar es Salaam ni ya kimataifa, hivyo tiketi za mtandaoni itakuwa utaratibu endelevu unaohusisha wasafiri wa nje ya nchi.