Tunasherehekea uhuru wa habari, lakini bado changamoto hazijaisha

03May 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tunasherehekea uhuru wa habari, lakini bado changamoto hazijaisha

LEO ni maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, kwa Afrika yanafanyika Tanzania kwa kuwaleta pamoja wanahabari na wadau wa habari wa nchi mbalimbali chini ya kauli mbiu ya ‘uandishi wa habari na changamoto za kidigitali’.

Kila mwaka maadhimisho haya yanafanyika kutathmini hali ya utendaji wa vyombo vya habari na wanahabari wenyewe, ili kuhakikisha mazingira mazuri ya utendaji kazi utakaowezesha upatikanaji wa taarifa.

Tanzania tunasherehekea tukiwa na matokeo chanya kwenye taaluma, kwamba serikali imeonyesha utayari wa kushirikiana na wadau kufanya mabadiliko ya sheria za habari ambazo zinakwaza utendaji kazi.

Lakini kumekuwa na utayari wa serikali kusikiliza wadau na wanahabari hali iliyoongoza kujitathmini kulikokuwa kumeshamiri kiasi cha maudhui nzuri kukosekana kwa hofu ya kuwakwaza watawala au kuchukuliwa hatua.

Tunaamini mchakato huu utashirikisha wadau wote wa habari kutoa maoni yao ili yanapofanyika marekebisho yabebe mahitaji ya wanataaluma wote, badala ya kundi moja au wachache kupewa kipaumbele.

Jana Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema serikali iko tayari kushirikiana na wadau wote wakati wowote na mchakato wa mabadiliko utakuwa shirikishi huku akiwahakikishia Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda wanahabari na ndiyo maana amesukuma kuwapo mabadiliko.

Moja ya mambo yaliyoibuka wakati wa kongamano la wanahabari kuelekea siku ya leo ni ukuaji wa teknolojia na namna vyombo vya habari vya magazeti, redio na TV vinavyoweza kuendana na mabadiliko hayo kwa kuziona fursa zilizoko kujipati mapato.

Pia, umuhimu wa umoja kwa wanahabari na taasisi zao barani Afrika, kwa kuwa changamoto zinafanana kama mabadiliko ya sheria kandamizi yanasambaa kutoka nchi moja kwenda nyingine, kuzimwa au kupunguzwa nguvu kwa intaneti hasa wakati wa uchaguzi mkuu.

Yote hayo yanakwaza uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa; kwamba mabadiliko hayo na watawala kutaka kunyamazisha vyombo vya habari Afrika, ni suala lenye kututaka tuwe wamoja wenye sauti moja linapotokea jambo ambalo siyo la maendeleo ya uandishi wa habari.

Jingine ni ukuaji wa teknolojia uliotoa nafasi kwa raia kutumia intaneti kusambaza taarifa mbalimbali ambazo siyo za kitaaluma, kisha kujiita wanahabari na inapokuwa haina maadili jamii inawalaumu wanahabari kuwa wakosaji walioshindwa kufanya kazi yao kwa mujibu wa maadili.

Pia, waandishi wa habari bado wana hali duni za maisha kwa sababu baadhi ya vyombo vya habari haviwalipi au vinachelewesha malipo yao kwa muda mrefu kiasi cha wengi kugeuka ombaomba, jambo linalohitaji mikakati ya pamoja kutatua vinginevyo maadili yataendelea kuwa kitendawili.

Aidha, ukuaji wa vyombo vya habari mtandaoni ambavyo maudhui yake haikidhi matakwa ya uandishi wa habari, hali inayoifanya taaluma kudharaulika na kuonekana kila mtu anaweza kuifanya.

Kongamano hilo linatuleta pamoja kuziona changamoto na tunaposherehekea siku hii muhimu, lazima kushirikiana na wadau wote ikiwamo serikali, ili inapofanya mabadililo ya sheria nasi wanahabari tubadilike kwa ambayo yapo ndani ya uwezo wetu katika kutatua.

Lazima tuendelee kuelimisha jamii na kutengeneza tofauti ya waandishi wa habari waliosomea na wanaotambulika kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari 2016, na wananchi wanaorusha taarifa kwenye mitandao yao ya kijamii.

Tunapoadhimisha siku hii tunapaswa kuona umuhimu wa kuendelea kupaza sauti juu ya umuhimu wa haki ya taarifa ambayo wananchi wanastahili kupata habari hasa kwa serikali ambayo inawajibika kwao.

Bado changamoto zipo licha ya mafanikio yanayoonekana kwa kuwa kwa sasa wanaandikishwa waandishi wa habari kwenye wilaya na mikoa mbalimbali pasipokuwa na taarifa rasmi za kwanini wanataka hizo taarifa zao.