Utabiri huo ambao unaeleza kuwapo kwa upungufu wa mvua katika maeneo kadhaa ya nchi yetu wakati wa msimu wa vuli, unamaanisha kuwa kuna uwezekano wa kuwapo kwa athari mbalimbali, ukiwamo upungufu wa chakula.
Tunasema hivyo kutokana na mikoa maarufu ambayo huzalisha chakula kwa wingi hususan nafaka kuwa miongoni mwa mikoa ambayo itapata mvua za wastani au chini ya wastani.
Ikumbukwe kwamba mikoa hiyo mingi ikiwa ya Nyanda za Juu Kusini kuna wakati iliitwa kwa jina la ‘The Big Four’ kutokana na kuwa mzalishaji mkubwa wa nafaka hasa mahindi, hivyo kuwa tegemeo kubwa kwa uzalishaji nchini.
Katika taarifa yake ya utabiri juzi, TMA ilisema kwamba mikoa inayozalisha chakula kwa wingi nchini inatarajiwa kuwa na uhaba wa mvua na kwamba ni mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka kuanzia Novemba hadi Aprili mwakani.
Utabiri huo unaonyesha maeneo mengi ya mikoa yatakayopata mvua chini ya wastani na wastani kwa baadhi ya maeneo.
Mikoa hiyo inayotarajiwa kupata mvua pungufu ni Mbeya, Songwe, Ruvuma, Iringa, Rukwa, Katavi, Njombe, Lindi, Mtwara na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Morogoro.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alibainisha hayo mkoani Dar es Salaam na kufafanua kuwa hali hiyo inatokana na mifumo ya hali ya hewa, mvua za wastani mpaka chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa hiyo ikiwamo pia mikoa ya Kigoma, Tabora, Singida na Dodoma.
Kwamba hali ya sasa ya joto la bahari eneo la kati la Bahari ya Pacific iko chini ya wastani na inatarajiwa kuendelea kuwa chini ya wastani katika nusu ya kwanza ya msimu. Alisema hii inatarajiwa kudhoofisha mifumo inayosababisha mvua katika maeneo ya pwani ya magharibi.
Alisema kutokana na hali hiyo inayotarajiwa kunaweza kutokea athari mbalimbali na kuwataka wananchi na mamlaka husika kuchukua tahadhari.
Katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula kutokana na mvua za chini zinazotarajiwa, alisema kutakuwa na upungufu mkubwa wa unyevunyevu kwenye udongo na kuathiri ukuaji wa mazao, lakini kunatarajiwa kuwapo kwa visumbufu vya mazao kama mchwa, panya, viwavijeshi na wadudu wengine.
Aliwashauri wakulima kupanda mazao na mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili mvua chache kama ya jamii ya mizizi na mazao ya bustani, akisema mazao haya ni kama mihogo, viazi, mtama na mazao mengine yenye kustahimili mvua chache.
Aidha, athari nyingine ni kwa upande wa mifugo na uvuvi ambapo kutokana na uhaba wa mvua hizo kunaweza kukaathiri upatikanaji wa samaki na uhaba wa malisho ya wanyama.
Kwa kifupi, sisi kama taifa tunapaswa kuanza kuchukua hatua za tahadhari kuanzia sasa, kwa kuwa ni dhahiri kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kutokea upungufu wa chakula.
Katika nchi zinazoendelea ambazo hazijawa na teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji, mvua inapokosekana maana yake ni ukame, hivyo ni dhahiri kwamba kutakuwa na upungufu wa chakula.
Tunaishauri serikali ianze maandalizi ya kusambaza chakula cha ziada katika maeneo yatakayokuwa na upungufu na kama ziada haitatosheleza, basi ikiagize kutoka nje. Kwa upande wao wakulima wapande mazao ya muda mfupi yanayostahimili ukame.










