Nidhamu mbovu Ligi Kuu Bara 'mfupa' unaokomaa

30Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Nidhamu mbovu Ligi Kuu Bara 'mfupa' unaokomaa

LIGI Kuu ya NBC Tanzania Bara ndio ligi ya juu hapa nchini na msimu huu mwaka 2021/22 inashirikisha jumla ya timu 16 kutoka mikoa mbalimbali.

Timu hizo zinazoshiriki ni mabingwa watetezi, Simba, Yanga, Azam, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Ruvu Shooting, Polisi Tanzania, Dodoma Jiji, KMC, Biashara United, Geita Gold, Tanzania Prisons, Mbeya City, Mbeya Kwanza, Coastal Union na Namungo.

Mechi zote za ligi hiyo ambayo hutoa wawakilishi wa nchi katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, inaonyeshwa mubashara kupitia Azam Media.

Kwa maana hiyo, mechi zote zinaonekana duniani kote kwa sababu kupitia simu za mkononi, wadau wa soka wanaweza kushuhudia mitanange mbalimbali inayochezwa hapa nchini.

Hata hivyo, wakati ligi hiyo ikiendelea kupanda viwango, bado kumekuwa na matukio mbalimbali ya aibu ambayo kila mara yanakemewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini yanajirudia na yamekuwa hayana afya katika maendeleo la soka nchini.

Viongozi wa timu, makocha au wanachama wanaojulikana kwa jina maarufu la 'makomandoo' wamekuwa wakionekana kwenye picha mnato au za video wakiongoza wachezaji kupitia milango isiyo rasmi kwa madai ya kukwepa ushirikina.

Wakati mwingine timu hizo zikiwa zinawasili viwanjani na wakifahamu wazi kamera ziko mbele yao, viongozi hao wanawaongoza wachezaji kufanya vitendo vinavyotafsiriwa au vinavyohusishwa moja kwa moja na imani za kishirikiana.

Tumeshuhudia pia wakati mwingine viongozi hao wakiwakataza wachezaji kutoingia kwenye vyumba rasmi za kubadilishia nguo wakidai vimepulizwa dawa za kuwalegeza nyota wao ili washindwe kucheza kwa viwango vya juu na kutumia magari waliyokuja nayo au kukaa chini ya miti.

Haya yanayoendelea hayaendani na maandalizi makubwa yaliyofanywa na viongozi husika kuanzia kwenye mchakato wa usajili, kambi za ndani na nje ya nchi, michezo mbalimbali ya kirafiki waliyocheza, kuendelea kufanya 'mauzauza' haya kunashusha heshima ya ligi.

Wakati wadau wengine wakiitaka TFF kuongeza kiwango cha faini kwa timu zinazorudia makosa hao mara kwa mara, umefika wakati kanuni kali zikawekwa ili kuitokomeza tabia hii 'mbovu' inayoonekana kukomaa au kuonekana kama ni jambo la kawaida.

Kutokana na teknolojia na vyombo vya dijitali vinavyotumika, si wakati wa kuendelea kufanya vitendo hivi kwa sababu mbali na kuivunjia heshima ligi, lakini havitoi taswira yenye afya kwa wachezaji chipukizi ambao baadaye wanatarajiwa kuitumikia nchi.

Si tu matukio haya yanashusha heshima ya ligi, lakini pia yanapunguza hadhi ya klabu, wachezaji na wote wanaoshiriki.
Na kwa sababu baadhi humulikwa na kamera, basi hujipunguzia heshima au dhamana waliyopewa na wanachama wao kwa kuweka mbele imani za kishirikina hali ya kuwa waliwaaminisha wamefanya usajili mzuri na maandalizi sahihi kuelekea msimu husika.

Adhabu za faini ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wahusina zinaonekana kulipika hivyo, hivyo wahusika wanaendelea kurudia makosa hayo mara kwa mara.

Tuachane na vitendo hivyo kwa maslahi ya soka letu, haipendezi kuipa Kamati ya Mashindano ya TFF kazi ya kutunga kanuni kali na badala yake wahusika wakaacha tabia hizo, wasijifishe kwenye 'kivuli' cha kufanya ushirikina ili kuhalalisha kupatiwa fedha za kukamilisha mchakato huo.

Tunawakumbusha wale wote wanaosimamia timu kuacha mara moja kufanya matukio haya kwa sababu tunahitaji kuona Tanzania inasifika kwa mambo mazuri, na kila mmoja afahamu mpira wa miguu ni mchezo unaohitaji maandalizi bora na matokeo chanya kamwe hayapatikani na njia za miujiza.