Tuanze mikakati kufikia soko la wenye COVID-19

19Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuanze mikakati kufikia soko la wenye COVID-19

RAIS John Magufuli, ametoa wito kwa Watanzania kuzalisha kwa wingi hasa mazao ya chakula ili kuyauzia mataifa ambayo yameathirika na COVID-19 ambayo bila shaka ni nchi za Afrika.

Alilozungumza Rais ni jambo linaloonyesha wazi kuwa serikali imeazimia kuwaunga mkono wakulima na wazalishaji wakiwamo wasindikaji na viwanda ambavyo vina fursa ya kuuza kwa tija kupitia angalizo hilo.

Ni wazi kuwa ni fursa ambayo inahitaji uwekezaji kuanzia sasa ambao utafanikisha kulima na usindikaji wa nafaka kama mahindi kupata unga wa madaraja mbalimbali, mchele wa viwango na madaraja tofauti, kadhalika matunda na mboga.

Tunatamani kuona maelekezo ya Rais yakianza kufanyiwa kazi sasa kwa vile kuna mazao ya kutosha yanayoweza kuuzwa kwa tija kwa mataifa kama Malawi, Rwanda, Burundi, Zambia, Congo DRC na Sudan Kusini.

Mauzo yanaweza kufanyika sasa iwapo kuna wakulima wenye akiba ya nafaka kama mchele, ngano, mtama na mahindi. Aidha, kama kuna mbegu za mafuta kama korosho na karanga. Kuna jamii ya kunde hasa choroko, kunde, dengu, mbaazi na maharage.

Lakini, vipo viungo kama vitunguu vya aina mbalimbali, yapo matunda kuanzia matikiti maji, nyanya, mafenesi, maparachichi na ndizi. Si hivyo pekee kuna mifugo kama nyama na hata maziwa ambavyo vyote vinaweza kuuzwa kwa tija na wakulima wakanufaika na fursa hiyo ya kuwapo kwa soko la chakula kwa mataifa yaliyoathirika na COVID -19.

Kama Rais alivyosema ni muhimu Watanzania wakazalisha kwa wingi mazao ya chakula, ili kunufaika na soko lililoko kwenye mataifa ambayo hakuna chakula kutokana na wananchi kufungiwa ndani kuepuka kusambaa kwa maradhi ya corona.

Rais anasisitiza umuhimu wa kutumia mvua zinazoendelea kunyesha na kukumbusha kuwa hivi sasa maeneo mbalimbali ya nchi hii yana mvua hivyo watu waanze kulima mazao hasa ya chakula tena kwa wingi ili baadaye yauzwe kuwasaidia wenzetu ambao wanashindwa kulima kutokana na corona.

Wakuu wa Wilaya na Mikoa waisikie kauli ya Rais kuhamasisha kilimo, kwa mfano mijini kuna mapori mengi na watu hawayatumii kwa kilimo, kwa mfano Dar es Salaam, kuna mashamba makubwa ambayo hayajaendelezwa, mathalani kuweka nyumba za makazi, ni vyema viongozi wa serikali za mitaa wakahimiza watu kuruhusiwa kuyalima kupanda mazao ya muda mfupi kama mihogo, ndizi, viazi, kunde, mbaazi na choroko ambayo wanaweza kuuza na kunufaika na fursa hiyo ya ‘soko la corona.’

Ni wakati pia wa kuangalia jinsi bora ya kusindika bidhaa hizo ili kunufaika na soko hilo. Ndiyo maana tunawashauri wadau wa uwekezaji kwenye viwanda likiwamo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TRIDO), Viwango la Taifa (TBS) na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuweka mikakati ya namna bora ya kuwawezesha wananchi kunufaika na soko la corona lililoko nje ya nchi.

Pamoja na jitihada hizo Mamlaka ya Uuzaji Nje ya Nchi (EPZA) ina nafsi ya kusaidia kufanikisha juhudi hizo kwa kuwezesha uwekezaji na hata kutoa nafasi zinazoweza kutumiwa kama viwanda ili kuzalishaji bidhaa zinazotokana na kilimo, ufugaji na uvuvi na kusindika mathalani, pamba ili kuzalisha nguo zinazoweza kupelekwa kwa nchi zenye corona.

Tunaona kuwa ni sasa tuwe na mikakati ya kitaifa ya kuandaa mipango, kuisimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo ya kuuza nje kwa kuwa ni soko lisilo na upinzani linaloweza kuwaondolea Watanzania wengi umaskini wa kipato.