Fursa za Kiswahili ni nyingi, tuzichangamkie

21Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Fursa za Kiswahili ni nyingi, tuzichangamkie

LUGHA ya Kiswahili ina fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri, zinaweza kuwanufaisha Watanzania wengi.

Pamoja na lugha ya Kiswahili kuwa ya Taifa tangu baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1964, bado fursa zake hazijatumika ipasavyo katika kuinufaisha nchi yetu na wananchi wake.

Umekuwapo uhamasishaji ambao umekuwa ukifanywa na viongozi wa serikali pamoja na wadau wengine, lakini kimsingi, Watanzania hatujazitumia fursa za lugha hiyo.

Matumizi ya lugha ya Kiswahili yamekuwa yakiongezeka kutokana na kasi kubwa ya maendeleo duniani, ambayo kwa kiwango kikubwa yamechochewa na utandawazi.

Kukua kwa sayansi na teknolojia kumeifanya dunia sasa kuwa sawa na kijiji. Kwa maneno mengine, kwa sasa hakuna nchi inayoweza kujitenga na kujiita kisiwa, vinginevyo itaachwa na kubakia yenyewe.

Maendeleo hayo yameongeza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika nchi nyingi, hivyo kuendelea kuongeza wigo katika mahitaji yake.

Awali lugha hiyo ilikuwa ikitumika kwa kiwango kidogo katika mataifa jirani ya Afrika Mashariki, lakini kwa sasa mataifa hayo na mengine nje ya ukanda huo yameanza kuitumia sana na mahitaji yanazidi kuongezeka kila uchao.

Jinsi mahitaji yake yanavyozidi kuongezeka na kuvuka mipaka, hivyo kuwa fursa katika maendeleo, serikali imeliona hilo na kutoa msimamo.

Hatua hiyo ilitangazwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye ametoa maagizo matano ya kimkakati ya matumizi ya Kiswahili, ikiwamo kuwapo kwa sera ya lugha hiyo.

Aliagiza kuhakikisha kumbukumbu zote muhimu za nchi zinatolewa kwa lugha ya Kiswahili.

Akifungua maadhimisho ya Siku ya Kiswahili nchini juzi, Samia alisema ili kufanikisha matumizi ya lugha hiyo, ni lazima matumizi yake yapangwe na kuratibiwa.

Alisema Kiswahili kina fursa nyingi za kiuchumi, kijamii na kisiasa duniani, na kuagiza kwamba kwa wizara zote mbili na mabaraza na taasisi zingine za kuendeleza Kiswahili kwamba hadhi ya sasa ya Kiswahili kikanda na kimataifa inachagiza kuwapo kwa mageuzi.

Aliagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na wizara hiyo kwa upande wa Zanzibar, kukaa na wataalamu na kubaini maeneo na nyaraka za kiserikali ambazo bado Kiswahili hakitumiki ili hatua zichukuliwe.

Aliipongeza Wizara ya Katiba na Sheria ambayo imeanza kuchukua hatua kuhakikisha hukumu za mahakama zinatolewa kwa Kiswahili ili kuhakikisha wananchi wanyonge wanapata haki zao.

Aliagiza pia wizara hizo kushirikisha wadau wengine kuandaa mikakati ya kutangaza, kufundisha na kuendeleza lugha hiyo nje ya nchi.

Pia wizara zije na mkakati wa kuandaa wataalamu mbalimbali wa Kiswahili wakiwamo wakalimani, watafsiri, walimu na wengine ambao Tanzania itaanza kuwatumia kimkakati katika kukieneza Kiswahili.

Alisema taasisi za kuendeleza Kiswahili kama BAKITA na BAKIZA nazo sasa zikumbukwe kwa kupatiwa wataalamu na rasilimali fedha za kutosha ili kutekeleza jukumu hili  la kimkakati la kukiendeleza Kiswahili, ikiwamo ni kuimarisha kitengo cha uchapaji na uchapishaji cha TUKI pamoja na kampuni za uchapishaji lengo ni kuhakikisha machapisho ya Kiswahili yanawafikia watu wengi wa ndani na nje ya nchi.

Kwa kufanya hivyo, sisi kama taifa tunaweza kunufaika kwa kuwatumia wataalamu wetu kupata ajira kwa kwenda kufundisha lugha hiyo nje ya nchi pamoja na kufanya kazi za ukalimani.