Kilele cha tamasha hilo linaloshirikisha michezo nane kinatarajiwa kufanyika leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi katika ufungaji anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Lengo kuu ya tamasha hilo lilikuwa ni kutaka kufahamu sababu kuu inayowafanya wanamichezo wanawake nchini washindwe kufanya vyema zaidi na kufahamu njia ya kutatua changamoto hizo kwa sababu hakuna kinachoshindikana.
Imeelezwa na imetolewa ushuhuda kwamba wanamichezo mbalimbali wanawake kuanzia soka, mpira wa kikapu na riadha wamekuwa wakifanya vyema katika mashindano ya kimataifa wanayoshiriki licha ya kuzingirwa na changamoto mbalimbali kuanzia wakati wa maandalizi.
Changamoto namba moja iliyotajwa ambayo inachangia kukwamisha maendeleo kwa michezo na vyama vya soka vya wanawake ni kutojitangaza kama wanamichezo wanaume wanavyofanya licha ya wao kupambana kusaka matokeo chanya.
Mara kadhaa timu au wanamichezo wanawake wamekuwa wagumu au wavivu wa kutoa taarifa za kalenda za mashindano yao jambo ambalo linawaweka kwenye wakati mgumu wa kupata wadhamini wa kusaidia kuendesha mashindano yao mbalimbali.
Kupitia tamasha hilo, viongozi na wanamichezo wanawake wametakiwa kubadilika kwa kutumia vyombo vya habari kujitangaza na kwa kufanya hivyo, si tu itawavutia wadhamini kujitokeza, lakini pia itasaidia kuongeza hamasa na ushiriki wa wachezaji kutoka sehemu mbalimbali.
Inafahamika wazi wachezaji wenye vipaji wanapatikana kuanzia ngazi za chini na ili kuwapata ni lazima chipukizi hao wafahamu uwepo wa mashindano na hapo ni rahisi kuwabaini na baadaye kuendelezwa kwa ajili ya kuzitumikia klabu au kuitwa kwenye vikosi vya timu za taifa.
Wanawake pia wamekumbushwa kuajiri wataalamu katika michezo wanayoicheza na kuacha kuajiri wafanyakazi kwa mazoea, kwa sababu dunia ya sasa wachezaji wanatakiwa kuongozwa na makocha wenye weledi ambao watawasaidia kukabiliana na ushindani pale watakapokwenda kuchuana kimataifa.
Wachezaji wanaopata misingi sahihi, huwa imara na tayari kuipa matokeo chanya klabu au nchi yake kila wanapokwenda kupeperusha bendera katika mashindano watakayoshiriki.
Wanawake pia wamekumbushwa kuwa katika mstari wa mbele kutumia njia za kisasa za mawasiliano ili kujitangaza na kuwavutia wadhamini kama ambavyo matakwa halisi yanavyotulazimisha kwenda na kasi hiyo.
Lakini pia wanawake wamekumbushwa kutumia vyombo vya habari katika matukio chanya, kuheshimu katiba zao lakini pia kutokaribisha migogoro baina yao na kuweka mbele maslahi ya mchezo husika.
Tukumbuke kwa sasa nchi inaongozwa na Rais mwanamke ambaye ameweka mabilioni kwa ajili ya kuendeleza michezo hapa nchini.
Si kwamba anafanya hivyo kwa makosa, bali nia na malengo ya kiongozi wetu ni kuona timu za Tanzania zinakuwa vinara na washindani kwenye michuano mbalimbali wanayokwenda kushiriki.
Tunawakumbusha kufanya vizuri kwa wanamichezo wanawake, mbali na kulipa taifa sifa, pia kutasaidia kuwanyanyua kiuchumi na kuwaepusha na majanga yanayoweza kuwatokea kwa kutumia muda mwingi kufanya mazoezi.
Sifa ya kwanza ya mwanamichezo ni nidhamu, hivyo kama wanamichezo wanawake watakuwa na nidhamu, ni dhahiri jamii inayowazunguka kuanzia katika familia wanazotoka, hali itakuwa nzuri na nchi itakuwa na mabadiliko.