Lilieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya kupungua kwa kina cha maji katika chanzo hicho kutokana na upungufu wa mvua kwa msimu huu na ujao pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kibindamu.
Sababu kubwa ni kupungua kwa kina cha maji ikilinganishwa na Septemba mwaka jana, kilipokuwa na kina cha milimita 12,500 hadi kufikia 7,500 kwa sasa.
Kwa mujibu wa Bonde hilo, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inachukua milimita 5,000 kwa sekunde kutoka katika mto huo. Aidha, walitahadharisha kuwa kama hali ya ukame itaendelea, mto huo utakauka na kusababisha mitambo ya DAWASA kupungua uwezo wa uzalishaji maji na kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.
Jitihada za awali ni kuweka sandarusi (maarufu kama viroba) kuongoza maji kwenda kwenye mitambo yao ili kukabiliana na upungufu huo.
Tunafahamu kuwa mabadiliko ya tabianchi ni mojawapo ya chanzo cha uhaba wa maji duniani, uwapo wa ukame na ongezeko la joto kuna changia kwa asilimia kubwa kukauka kwa mabwawa na vyanzo vya maji.
Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kiasi cha maji yanayohitajika kwa matumizi na kwa hivyo kuathiri haki ya msingi ya binadamu kwa mabilioni ya watu ya kutumia majisafi na salama kwa matumizi mbalimbali.
Hivyo, mamlaka husika zinapaswa kuhakikisha zinadhibiti hali ya uharibifu wa mazingira miongoni mwa wakulima wanaolima pembezoni mwa kingo za maji, wanapaswa kuondolewa kwa mujibu wa sheria ya mazingira inayopiga marufuku kutofanyika kwa shughuli zozote ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji.
Mbali na hilo, jamii inapaswa kuelimishwa kuhusu matumizi makubwa ya maji hususani ya kuogea, kufulia, kupikia, tabia ya watu kutumia maji kwa fujo inapaswa kupunguzwa.
Tukumbuke kuwa utunzaji wa vyanzo vya maji ni jukumu la watu wote, kwani kuacha vyanzo hivyo vikatumika kiholela au kuharibiwa, madhara yake ni makubwa kwa kila binadamu.
Suala la kufanya shughuli za kibinadamu kando ya vyanzo vya maji kama vile ulimaji kunasababisha ubora wa maji kupungua kwani mbolea inayotumika katika kilimo huenda ardhini na kuingia katika tabaka la maji na kuaribu ubora wa maji.
Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) mwanzoni mwa mwezi huu ilitoa taarifa ya tahadhari ya hapo baadaye kuwapo kwa ukame katika baadhi ya mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka, hali ambayo iliyowahi kutokea miaka 16 iliyopita.
Kutokana na tahadhari hiyo, mamlaka husika kwa maana ya serikali inapaswa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya maji kwa wananchi.
Wananchi wanapaswa kuwa na matumizi mazuri ya maji hususani majumbani ambako kunaelezwa baadhi ya jamii zimekuwa na matumizi mabaya. Tabia ya watu kuoga mara tano, kufua kila siku ama kuosha vyombo kwa kutumia ndoo ya ujazo wa lita20 kunapaswa kupunguzwa, kubana matumizi kunapaswa kuzingatiwa.
Kadhalika, wakulima wakubwa wenye mashamba yenye hekari 10 na kuendelea wanapaswa kuanza kuchukua hatua ya kubana matumizi ya maji. Kama mkulima alikuwa amefunga mfumo wa umwagiliaji siku nzima anapaswa kupanga muda maalum wa umwagiliaji.
Ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anatunza vyanzo vya maji, kutokufanya hivyo kutasababisha sehemu ya jamii hususani wanawake na watoto kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.