Suala la watumishi hewa ni mtandao ndani ya serikali

17Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Suala la watumishi hewa ni mtandao ndani ya serikali

SERIKALI imebainisha kwamba kuna uozo wa watumishi hewa katika halmashauri nyingi nchini, hali ihayosababisha serikali itumia fedha nyingi kuwalipa mishahara.

Rais Dk. John Magufuli, amesema kuwa ameugundua uozo huo baada ya kufanyika uchunguzi na kuwaagiza wakuu wote wa mikoa aliowateua kwenda kusimamia halmashauri pamona na mambo mengine, kuhakikisha kwamba wanalikomesha.

Alisema alituma wataalam Februari, mwaka huu kwenda kufanya utafiti katika mikoa ya Singida na Dodoma kuhusu ulipaji wa mishahara Desemba na Januari na kubaini watumishi 26,900 katika halmashauri 14 waliofanyiwa uhakiki, 202 wanalipwa mishahara hewa.

Alifafanua kuwa kati ya watumishi hao hewa, baadhi wameshafariki dunia, kufungwa na wengine ni wastaafu na kwamba watumishi zaidi ya 3,320, wakati uchunguzi huo unafanyika hawakukaguliwa kwa kuwa walikuwa na ruhusa, wengine masomoni na baadhi wagonjwa.

Katika mwenendo huo, alisema kama hali hiyo ipo katika halmashauri zote 180 zilizoko nchini, basi kutakuwapo na watumishi hewa 5,297, na kwa makadirio ya kulipwa mshahara wa Sh. milioni moja, serikali inapoteza Sh. bilioni 2.59 kila mwezi.

Kutokana na hali hiyo, Rais Dk. Magufuli alitoa siku 15 kuanzia juzi kwa wakuu wapya wa mikoa wawe wamekamilisha na kurekebisha tatizo hilo kwa kuwatoa watumishi hewa katika orodha ya malipo ya mishahara na kwa mkurugenzi atakayeshindwa kufanya hivyo, kwa mwezi ujao atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe na atapelekwa mahakamani.

Watumishi hewa ni eneo lingine ambalo watumishi wasiowaadilifu serikalini wamekuwa wakitumia kukujipatia fedha zao binafsi bila kujali kwamba ni kujuma dhidi ya serikali. Sh. bilioni 2.59zinazotumika kila mwezi kuwalipa watumishi hewa ni kikubwa na kingeweza kutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwamo ununuzi wa madawati kwa watoto wetu shuleni.

Wakuu wa mikoa waliopewa maelekezo ya kuwabaini watumishi hewa katika halmashauri wanapaswa kutambua kuwa wanaihusika na kunufaika kutokana na atumishi hewa sio mtu mmoja, bali ni mtandao, wakiwamo watumishi waandamizi, hivyo wanapowafuatilia hawanabudi kuwa na taarifa kuwa wanafuatilia mtandao.

Kinachotushangaza ni kwamba watumishi hewa serikali iliwahi kuanzisha utaratibu wa kuhakikisha watumishi hewa wanadhibitiwa ukiwamo wa kulipa mishahara madirishani badala ya kuipitisha benki mapema miaka ya 1990.

Kilichobainika katika halmashauri kuhusiana na kuwapo na idadi kubwa ya watumishi hewa, kiwe changamoto kwamba uchunguzi kama huo ufanyika pia katika Serikali Kuu ili kujiridhisha kwamba wanaolipwa mishahara ni watumishi halali au fedha za umma zinaingia katika mifuko ya watu binafsi.

Tunaunga mkono hatua aliyoichukua Rais Magufuli ya kuelekeza watumishi hewa waondolewe katika halmashauri kwa sababu haiwezekani serikali yake ijikite kuongeza mapato na kuweka nidhamu ya matumizi huku baadhi ya watumishi wahujumu jitihada hizo.

Tunasisitiza kwamba suala la watumishi hewa ni mtandao ndani ya serikali, hivyo ipo haja ya kuwa na umakini katika kuufuatilia wote na kuufumua.

Lakini pia tunashauri kwamba ipo haja ya kuwasaka pia Serikali Kuu na taasisi zake, idara na wakala.