Juhudi za serikali kupambana na dawa za kulevya ziungwe mkono

18Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Juhudi za serikali kupambana na dawa za kulevya ziungwe mkono

SERIKALI imesema kuwa watu 3,000 wametiwa mbaroni nchini kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.

Watuhumiwa hao wamekamatwa katika kipindi cha miezi mitatu tu tangu serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli iingie madarakani.

Taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa hao zilibainishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, katika mahojiano na gazeti hili na kwamba miongoni mwa waliokamatwa kuna wakubwa sana, wakubwa wa kati na wanaopokea wamekamatwa zaidi ya 20 huku wasambazaji wakikamatwa zaidi ya 100.

Waziri Kitwanga alieleza kwamba idadi kubwa miongoni mwa waliokamatwa ni wale wanaouza kidogo kidogo. Waziri huyo ingawa hakufafanua kuhusiana na hatua zinazoendelea dhidi ya waliokamatwa, lakini aliapa kuwa serikali itapambana na uhalifu huo kwa nguvu zote na kwamba yeye binafsi hataogopa kufa.

Aliongeza kuwa serikali haitakubali dawa hizo ziingizwe Tanzania au iwe njia ya kuzipitishia kwenda sehemu nyingine na kwamba hakuna atakayewalinda wahusika kwani mtu atakapohisiwa atachunguzwa ili azihakikishie mamlaka husika kuwa siyo muuza dawa za kulevya.

Hatua zilizochukuliwa na serikali kwa kipindi hicho kifupi ilichokaa madarakani ni za kupongezwa na wananchi wote hawanabudi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa kuhusiana na watu wanaowahisi kwamba wanahusika katika biashara hiyo haramu na hatari kwa nchi yetu.

Ni ukweli ulio wazi kwamba kasi ya kubwa ya biashara ya dawa za kulevya nchini ilichochewa na serikali kutokuwa makini kuwashughulikia wahusika. Wapo watu wanaosafirisha nje dawa za kulevya na wanaoziingiza nchini ambao wanafahamika, lakini wameendelea kufanya hivyo kutokana na kutokamatwa na mkondo wa sheria kuchukua nafasi dhidi yao.

Hili linathibitishwa na kauli zilizokuwa zinatolewa na baadhi ya viongozi waandamizi katika Serikali ya Awamu ya Nne kwamba wana majina ya wafanyabiashara ya dawa za kulevya. Hata hivyo, serikali hiyo iliondoka madarakani bila kuwakamata, kuwataja wala kuwafungulia mashtaka.

Kimsingi, nchi yetu imeathirika sana kwa dawa za kulevya. Vijana wetu wengi wamegeuka mateja mitaani na kuishia kuwa wapigadebe katika vituo vya mabasi, hali inayosababisha taifa likose nguvu kazi kwani hawawezi kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa. Aidha, vijana hao wamegeuka kuwa mzigo katika familia zao.

Kama serikali zilizopita zingechukua hatua madhubuti kudhibiti biashara ya dawa za kulvya, leo hii tusingeshuhudia athari kubwa tunazozishuhudia katika jamii yetu.

Tunaipongeza serikali ya Rais Magufuli kwa kulipa uzito suala la kudhibiti biashara ya dawa za kulevya kwa kipindi kifupi. Jitihada hizo zinatupa matumaini kwamba zitawezesha kukamatwa kwa mapapa wote wanaohusika na kuwafikisha mahakamani.

Jambo la msingi ni kwamba serikali ihakikishe kwamba uchunguzi dhidi yao na ushahidi haviachi shaka kwa ajili ya kuwaadabisha kisheria.

Tunaishauri jamii nzima kuunga mkono juhudi hizo za serikali ili kuokoa vijana wetu sambamba na kuiondolea nchi yetu aibu inayoipata kutokana na ripoti mbalimbali za kimataifa kuonyesha kuwa Tanzania ni njia ya kusafirisha dawa za kulevya.