Simba, Namungo tunataka rekodi nyingine kimataifa

01Mar 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Namungo tunataka rekodi nyingine kimataifa

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Klabu ya Simba na Namungo, wiki hii na ijayo watashuka katika viwanja tofauti ugenini kuendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.

Katika michuano hiyo, Simba inapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa wakati Namungo ikiwa na jukumu hilo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, mashindano yote yakiwa na utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani humu.

Tayari wawakilishi hao wameweka rekodi kwa kuwa timu mbili za kwanza kutoka nchini kufuzu hatua ya makundi kwa msimu mmoja wa michuano hiyo ya CAF, jambo ambalo linaonyesha namna soka la Tanzania limezidi kupiga hatua.

Simba ambayo tayari imeshacheza mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ipo Kundi A, pamoja na AS Vita ya DR Congo, Al Ahly ya Misri, na Al-Merreikh ya Sudan. Lakini pia imeshinda mechi zake mbili za kwanza dhidi ya AS Vita ikiwa ugenini bao 1-0 na pia ikapata ushindi kama huo dhidi ya Al Ahly nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, hivyo kukaa kileleni mwa kundi hilo ikiwa na pointi sita.

Kwa upande wa Namungo, ndiyo kwanza imefuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kuitoa Clube Desportivo Primeiro de Agosto ya Angola kwa jumla ya mabao 7-5, hivyo kupangwa Kundi D pamoja na Nkana FC ya Zambia, Pyramids ya Misri na Raja Casablaca ya Morocco.

Hivyo, wiki ijayo Machi 10, itaanzia ugenini nchini Morocco kucheza dhidi ya wenyeji wao, Raja Casablaca, ikiwa na lengo la kuendeleza moto wake ili kusaka nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Lakini kwa Simba ambayo msimu wa 2018/19 wa Ligi ya Mabingwa Afrika ilifika robo fainali kabla ya kutolewa na TP Mazembe ya DR Congo, kesho inatarajia kukwea ndege kuelekea nchini Sudan tayari kwa mechi yao ya tatu dhidi ya Al-Merrikh itakayopigwa Jumamosi Machi 6.

Tayari Simba ipo katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali kwa mara nyingine kutokana na ushindi wa mechi zake mbili, ingawa bado kinachotakiwa kwa sasa ni kuhakikisha inashinda tena angalau mechi mbili ili kujihakikishia kwa asilimia 100 kutinga hatua hiyo.

Nipashe tunatamani kuona Simba na Namungo zikiendeleza wimbi lao la ushindi ili kuweka rekodi nyingine kwa kuwa timu za kwanza kutoka Tanzania kwa mara ya kwanza kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ndani ya msimu mmoja.

Tunatambua bado kuna milima mirefu ya kupanda kabla ya kufika hatua hiyo, lakini sisi tunaamini malengo yakiwapo huku juhudi na kujituma zikitangulizwa mbele, hakuna kinachoshindikana kwa wawakilishi hao wa Tanzania hasa kutokana na kiwango ambacho kimekuwa kikionyeshwa na wawakilishi wetu hao katika mechi zao walizocheza hadi sasa kwenye michuano hiyo ya Afrika.

Tunaamini kama mabenchi ya ufundi ya timu hizo yatakuwa yakiendeleza pale yalipoishia kutoka katika kila mchezo, kuna mwanga mkubwa kwa timu hizo kushangaza Afrika katika michuano hiyo msimu huu ambao timu nyingi zinaonekana kutokuwa fiti kutokana na kutocheza kwa muda mrefu kulikochangiwa na mlipuko wa maambukizo ya virusi vya corona.

Tunawatakia kila la kheri wawakilishi hao wa nchi katika jukumu la kuipeperusha bendera ya Tanzania.