Kero za usafiri Mbezi Luis zipate ufumbuzi

02Mar 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kero za usafiri Mbezi Luis zipate ufumbuzi

KITUO Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Luis Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, kimeanza kazi, lakini kuna mambo ya msingi lazima yafanyiwe kazi ili kiendelee kuwa bora na safi muda wote.

Mathalani, baadhi ya mama na babalishe hawana maeneo ya kupikia, kiasi cha baadhi kuingia na majiko ya mkaa kituoni, jambo ambalo ni hatari.
 
Tunashukuru mamlaka ya usimamizi imewaondoa na kuwapa eneo la muda la kupikia, huku wafanyabiashara wanaoruhusiwa kuingia kituoni wakiwa ni wanaouza bidhaa za vyakula vilivyopikwa na vingine ambayo siyo hatari.
 
Kituo hicho ni kizuri na bora Tanzania kutokana na majengo ya kisasa na mpangilio mzuri uliopo, na kama kitasimamiwa kama inavyotakiwa, kitaendelea kuwa na maana ya uanzishwaji wake na kitahudumia abiria vizuri.
 
Kwa sasa bado hakuna mpangilio mzuri wa wasafiri na watumiaji wengine, namna ya kuingia na kutoka kiasi cha kutumia njia ya magari, huku kukiwa na ongezeko la bajaji na pikipiki ambazo hazina eneo maalum pa kuegesha.
 
Tangu kuanza kwa kituo hicho zimeibuka kero mbalimbali kama za wasafariri wa mikoa ya kusini kwamba wanaruhusiwa kushusha abiria kituo cha Mbagala na Temeke pekee, baada ya hapo kituo cha mwisho ni cha Magufuli.
 
Maana yake msafiri anayetakiwa kushuka Buguruni, Tabata au Ubungo hataruhusiwa kushuka njiani hadi mwisho au ashuke kabla na kutumia usafiri mwingine kwenda kwake.
 
Tunaona hakuna sababu ya kuzuia abiria kushuka njiani, bali kuwe na vituo maalum vya kushusha kwa kuwa kutaka kila abiria afike mwisho wa gari ni usumbufu na kuongeza msongamano eneo la kituo.
 
Aidha, mabasi yanayotumia njia ya Bagamoyo yanashusha abiria njiani kwenye vituo vinavyoruhusiwa, lakini kwa njia mpya ya Goba ambayo inatumiwa na baadhi ya mabasi hawataweza kushusha jambo ambalo ni usumbufu kwa wasafiri.
 
Pia, kutokana na kuwapo kituo kipya magari yaliyokuwa na ofisi nje ya kituo cha Ubungo kama eneo la Shekilango hayataruhusiwa kutumia maeneo hayo bali yote kuanza na kumaliza safari zao ndani ya Kituo cha Magufuli.
 
Tunaona maamuzi hayo ni usumbufu mkubwa kwa wasafiri, mathalani baadhi ya mabasi yana ofisi Kigamboni ili kuwarahisishia abiria wameamua kusogeza huduma hiyo karibu kwamba basi lianzie kule likusanye abiria na kupita kituoni humo.
 
Kama suala ni kupata ushuru ungewekwa utaratibu mzuri wa kuhakikisha kila kampuni inalipa, na wakati huo inapunguza usumbufu kwa wasafiri kuhakikisha anapata huduma za usafiri kwa urahisi.
 
Tunaona hakuna sababu ya mtu anayekwenda Tabata kupelekwa hadi Mbezi na baadaye kurudi Tabata, kiuchumi anapoteza muda mwingi barabarani na unamlazimisha kutumia gharama kubwa ambayo ingeepukika kama angeshusha njiani.
 
Hakuna sababu ya mtu anayetakia kuteremka Ubungo au Mwenge kulazimishwa kuja hadi Mbezi, wakati inawezekama kabisa kumshusha eneo hilo na kumrahisishia.
 
Kituo kwenda Mbezi kisigeuke kuwa fimbo kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa umma kwamba anatumia gharama kubwa kuliko nauli ya aendako, tunaona ni muhimu mamlaka husika zikaja na utaratibu mzuri wa kuhakikisha wasafiri hawasumbuki.
 
Kama ilivyofanyika kwenye miji mingine abiria wanapakiwa na kushushwa kwenye vituo maalum na siyo wote lazima wafike mwisho wa basi.
 
Pia ni muhimu sana mamlaka za usimamizi zikasimamia kituo cha Magufuli ili kiendelee kuwa bora, kuruhusu shughuli za kipika na nyinginezo hatari ndani ya kituo mwisho wake ni janga kubwa kukinyemelea kituo hicho kilichojengwa kwa mabilioni ya fedha za walipakodi.