Kasi ya kuunganisha umeme iongezeke

02Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kasi ya kuunganisha umeme iongezeke

JANA Wizara ya Nishati iliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23, iliyojikita kuimarisha upatikanaji wa umeme kutoka kwenye vyanzo mbalimbali, upatikanaji na bei za mafuta.

Bajeti hiyo imeonyesha vyanzo vipya ambavyo awali havikuwahi kutumika, huku kukiwa na mkataba na sekta binafsi zilizojikita kwenye uzalishaji wa nishati jadidifu.

Pia imelenga kusambaza gesi asilia kwenye makazi ya watu katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro huku ikisafirishwa kwenda nchi za Kenya na Uganda baada ya kukamilisha makubaliano baina ya pande hizo.

Kwa Dar es Salaam vitajengwa vituo vya kugandisha gesi asilia, pia wataunganisha kwenye nyumba 670 za Sinza 225, Police Barracks Kurasini 345, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) 100 na kiwanda cha Raddy Fiber Manufacturing Tanzania Ltd cha Mkuranga.

Vyanzo vipya vya vitano vya nishati ni jotoardhi vya Ngozi na Kiejo – Mbaka mkoani Mbeya, Songwe, Luhoi Pwani na Natron Arusha, ambavyo baada ya upembuzi yakinifu ilibainika vitazalisha megawati 200.

Nyingine ni nishati ya jua na katika mwaka ujao wa fedha serikali itaanza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa jua Shinyanga, utakaogharimu Euro milioni 115.30 (sawa na Sh. bilioni 286.2) na kwamba jumla ya Sh. bilioni 9.55 fedha za nje zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme jua megawati 50 na kukamilisha taratibu za ufadhili wa awamu ya pili ya megawati 100.

Waziri wa Nishati, Januari Makamba, aliliambia Bunge kuwa kumekuwa na changamoto ya kukatika kwa umeme nchini kutokana na miundombinu ya kuzidiwa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji kwa sasa, uchakavu wa miundombinu na shughuli za kibinadamu kama vile magari kugonga nguzo, nguzo kuchomwa moto na hujuma katika moto na hujuma.

Alisema ili kuimarisha miundombinu ya usambazaji umeme, serikali imeendelea kutayarisha na kutekeleza miradi ya kusambaza nishati hiyo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma na Pwani, itakayowezesha kuondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara ili kuwa na uhakika.

Mchanganuo wa uwezo wa mitambo ya kufua umeme katika gridi ya taifa kwa kila kimoja kiwango cha megawati kwenye mabano ni maji (574.60), gesi asilia (1,021.32) na tungamotaka (10.50) na kufanya jumla ya megawati 1,694.55.

Kwa mujibu wa waziri huyo, mahitaji ya juu ya umeme katika mfumo wa gridi ya taifa yameendelea kukua na kufikia Megawati 1,335.01 hadi Machi 25, mwaka huu saa 2:00 usiku, ikilinganishwa na megawati 1,201.02 zilizofikiwa mwaka 2020/21, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.16.

Tunaamini kupitia bajeti hii wananchi wataendelea kupata huduma ya umeme ipasavyo, kuanzia walioomba kuunganishiwa na kulipa na wanaotamani kufikiwa na huduma hiyo.

Ni muhimu nchi ikajipanga vyema kuendeleza vyanzo vya nishati jadidifu kwa kuwa ndiyo msukumo wa dunia, lakini kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ili huduma iwafikie wananchi wengine na kwa haraka.

Kuna viwanda vinazalisha umeme kutokana na mabaki ya miwa vinaliuzia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lakini wapo wengine wanaweza kuzalisha umeme wa jua kwa ajili ya matumizi yao ni muhimu kuangalia.

Pia kumekuwa na malalamiko ya urasimu kwa wawekezaji binafsi ambao wamewekeza kwenye sekta hiyo kutokana na kuwapo vibali zaidi ya 30 wanavyotakiwa kuvifuata sehemu tofauti nchini, jambo linalowapa gharama kubwa.

Wakati tukiendelea na vyanzo vilivyozoeleka ni muhimu kuwekeza na kuwa makini na uwekezaji unaofanywa kwenye vyanzo vya nishati jadidifu ambavyo ni rafiki kwa mazingira ambavyo ni jua, upepo, mawimbi na upepo wa bahari na tungamotaka, ili inapofika ulazima wa kuachana na gesi, mafuta na maji kuwe na maandalizi ya kutosha.

Maji ni chanzo kizuri cha kuzalisha umeme, lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi inapotokea ukame vyanzo hukauka na kushindwa kuzalisha nishati hiyo, mara kadhaa Tanzania imepitia mgawo sababu ikiwa ni kukauka kwa mabwawa ya kuzalisha nishati hiyo.