Katika hafla hiyo iliyofanyika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, Dar es Salaam, Rais alizungumza mambo mbalimbali ikiwamo kuagiza viongozi wa kisiasa katika ngazi za chini kujumuishwa katika kundi la wanufaika wa mpango huo.
Pamoja na hilo, Rais aliagiza viongozi na watendaji wa TASAF kujikita zaidi katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya rasilimali zao badala ya kuwapatia fedha pekee.
Kwa kufanya hivyo, alisema itasaidia kuwaondoa watu hao katika umaskini unaowakabili na wakati huo huo, kutekelezwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG).
Bila kuruka maneno, Rais alisema mtu kuwa katika nafasi ya kisiasa haimaanishi kuwa ana maisha mazuri kwa kuwa wako baadhi ambao wanaishi maisha duni. Hatua ya baadhi ya viongozi kuwa na vyeo, imekuwa ikiwanyima fursa mbalimbali licha ya kwamba miongoni mwao wanaishi maisha duni.
Kama alivyosema Rais Samia, viongozi wanapochaguliwa katika nafasi, kigezo cha kuwa na maisha bora hakipo bali huangaliwa uadilifu, uwezo wao katika kuongoza, heshima na busara walizo nazo katika jamii wanazoishi.
Hii ni kutokana na miiko ya uongozi iliyowekwa na waasisi wa taifa kutokana na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyokuwapo baada ya kupata uhuru.
Pamoja na ukweli huo, kumekuwa na kasumba kudhani kwamba mtu anapochaguliwa kushika nafasi fulani, anajimudu kimaisha licha ya ukweli kwamba wako ambao hata uwezo wa kuhimili milo mitatu kwa siku hawana.
Hatua hiyo ya kutokupata fursa kama zinazopatikana kupitia TASAF zimekuwa zikiwapa kisogo na matokeo yake kuendelea kuishi katika umaskini uliokithiri.
Kwa maneno mengine, kunyimwa kwao fursa hizo ni moja ya aina za ubaguzi katika jamii. Mfano halisi ni viongozi walioko katika vyama vya siasa kuanzia ngazi za vitongoji, vijiji hadi kata ambao baadhi yao maisha yao ya kila siku ni ya kijungujiko yao.
Kuhusu elimu, ni jambo la msingi kutokana na uhalisia wa maisha ya Watanzania wengi kutokuwa na uelewa juu ya masuala mbalimbali ikiwamo kutumia rasilimali walizo nazo au zinazowazunguka katika kujiletea maendeleo.
Katika jamii za wafugaji, kwa mfano, ni jambo la kawaida kumkuta mtu akiwa na ng’ombe wengi, lakini anaishi maisha duni. Kwa maana hiyo anakuwa mtumwa wa mifugo badala ya kuwa mnufaika au anakuwa mchungaji na si mfugaji.
Agizo la Rais juu ya viongozi wa kisiasa kunufaika na fursa mbalimbali hasa zile za TASAF, limetolewa kwa wakati mwafaka na linastahili kupongezwa kwa kuwa ameonyesha upendo wa hali ya juu kwa wananchi wake.
Pia umefika wakati kwa Watanzania kuondokana na ufugaji au ukulima wa mazoea ambao umezidi kudumisha umaskini siku hadi siku badala ya kujikwamua na shughuli husika.
Ili kufanikiwa katika hilo, elimu inapaswa kutolewa kwa kiwango cha hali ya juu ili wananchi walime na kufuga kwa njia za kisasa. Yote hayo yatafanikiwa iwapo watendaji watakwenda kwa wakulima na wafugaji badala ya kukaa kwenye ofisi.
Kwa mantiki hiyo, kinachofuata sasa ni utekelezaji ikiwamo kuwabaini wale wasio na uwezo na hatimaye kupatiwa misaada.
Tunaamini kwamba kwa kuwa ni viongozi katika jamii, pia watatoa ushauri mzuri namna ya wananchi kuboresha maisha yao kupitia uwezeshwaji kutoka TASAF.
Pamoja na pongezi hizo, suala la mhusika anatoka chama gani cha siasa lisijitokeze kwani kuna uwezekano katika maeneo likajitokeza jambo hilo na hatimaye kuibuka kwa ubaguzi kwa misingi ya kisiasa.
Ni vyema kwamba jambo kama hilo litakapojitokeza, likemewe mara moja na wahusika wachukuliwe hatua stahili.
Tunasema hivyo kwa sababu Watanzania ni wamoja bila kujali imani zao za kidini, rangi, siasa wala kabila.










