Watoto walivyokuwa 'wanamaindi' baba kula paja, nyama kubwa, kidari

11Feb 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Watoto walivyokuwa 'wanamaindi' baba kula paja, nyama kubwa, kidari
  • Ukikosa nyama, unakwenda uani kwa mama kuangua kilio

BAADA ya makala iliyopita kwenye safu hii iliyokuwa na kichwa cha habari 'Zama za mwiko mtoto mdogo kula firigisi, mjamzito  mayai' ambayo ilikuwa ikielekezea jinsi wazee wa zamani walivyokuwa na sheria, taratibu na kanuni ambazo ziliwakataza watoto kufanya vitu fulani,

Au kula baadhi ya vyakula, huku kukiwa na mikwara ya vitisho kama vile ukifanya kitu fulani kikatokea kitu fulani, baadhi ya wasomaji wameonekana kuvutiwa na kueleza hisia zao kuhusu hilo.

Hata hivyo kumbe wengi wao ambao kwa sasa ni watu wazima wameonekana kuwa hawakuwa wanapendezewa kabisa, baba kula nyama kubwa, firigisi, kuanza kula yeye kabla ya wengine na hata kumsubiri yeye ndiye ashibe aanze kunawa ndiyo na watoto wakale na waondoke.

Wengi waliopiga simu na kutuma meseji walisema ni kwa sababu ni baba tu na hawakuwa na namna ya kufanya chochote, lakini walikuwa wanatamani mno nao kula firigisi, paja, kiasi kwamba walianza kuuchukia utoto na kutaka kuwa wakubwa ili nao waanze kufaidi ule upendeleo wote wa baba.

Kwenye safu hii leo nitaweka baadhi ya meseji ambazo nimetumiwa na wasomaji wa safu hii ambao wengi wamechangia kwa hisia kali kuhusu utaratibu wa zamani, wakitaja kanuni mbalimbali zisizo rasmi ambazo ziliwekwa na wazee kwa ajili tu ya kutaka mambo yaende sawa.

Pamoja na yote, wote walikubaliana kwamba kilichokuwa kikifanyika na kuwalea kwenye mazingira mazuri, adabu na heshima, lakini hilo walilitambua walipokuwa watu wazima, lakini wakati ule bado wadogo walichokuwa wanaona ni kama wanaonewa hivi na walikuwa 'wanamaindi' baba kuwa kama nahodha wa safari nzima ya msosi, akiwa kama staa wa filamu za kihindi kila kitu anajua yeye.

Kama kawaida, meseji za wasomaji wa safu hii huwa majina yake hayachapishiwi kwa sababu wengi wao hawahitaji kwa sababu sasa ni watu wazima, wenye familia zao, na wengine hadhi kubwa na viongozi kwenye nyanja mbalimbali.

"Kakumbusha sheria ya baba ndio anagawa nyama, utakayopata ndiyo hiyo hiyo, paja lazima ale yeye na kipapatio ndio tunakula watoto." Aliandika msomaji mmoja kutoka Kibaha, mwingine akaandika.

"Kiboko ni ile sheria ya nyama kubwa na zenye mfupa ni za baba, yaani kama nyumbani kwetu ilikuwa hivyo," aliandika mwingine.

"Nakumbuka wakati wa kula kama wali na nyama, baba ndiyo anaanza kunawa, anachukua bakuli la mboga, anamimina mchuzi, akimaliza kumwaga wote mnatakiwa muangalie pembeni akiwa anachagua nyama ya kuanza nayo." Jamaa huyu yuko sahihi kabisa, ila meseji yake inafurahisha sana. Mwingine akaandika.

"Paja kidari cha wakubwa kichwa miguu ndiyo yako mtoto, wa mwisho kula ndiye atakayefagia na kuukunja mkeka."

Meseji nyingine iliandikwa hivi. "Kichwa anakula baba kama ni Samaki, mfupa anakula baba kama ni nyama na Paja au kidari anakula baba, sasa wewe jitie mjanja..." Bado meseji ziliendelea kumiminika kuonyesha watoto wakati huo walivyokua 'wakimaindi' baba kula mapaja ya kuku.

"Paja na firigisi la baba, hakuna kugusa nyama mpaka aanze na hata ukishiba huinuki mpaka baba ashibe nilikuwa nachukia sana."

Meseji moja iliunga mkono tabia za kinababa wa zamani.

"Huo haukuwa ukatili bali tulifunzwa kuwa na nidhamu hata sasa hivi kwenye kizazi cha sasa itokee wageni wale chakula na mwanao halafu aanze kumega tonge na kuwahi paja la kuku kabla ya wakubwa lazma ujisikie vibaya, halafu mbona siyo kinababa tu  hata kijana tu akibaki nyumbani na wadogo zake kwenye msosi lazima uwapunje."

Hizi ni baadhi tu ya meseji zilizoonyesha watoto walivyokuwa 'waliwamaindi' baba zao wakati huo, sasa kuna hizi zingine kwenye sheria ya kula hapo zamani.

"Siku ya ubwabwa mchele unachaguliwa saa tisa, chakula kinapikwa saa 11:00, mnaoga mapema hamtoki nyumbani, na ole wako uwaite rafiki zako muda wa kula na hakuna kutangaza mnapika wali, pia kikibaki kidogo anabakishiwa mtoto."

Lakini pia hata staili ya kuitwa kula inabadilika siku ya ubwabwa utasikia “weee Happy shauri yako” bila kumalizia njoo ule.

 Meseji moja iliunga mkono tabia za kinababa wa zamani.

Mwingine akatoa mpya kwenye meseji yake.

"Ukikosa nyama unaenda kulia kwa mama uani huku unalia, unapewa nyama na chakula pia."

Mama mmoja akaandika kuwa wakati huo yeye ndiye alikuwa mdogo kwao.

"Mimi ndiyo nilikuwa mtoto, basi nawekewa mpaka kwenye sahani ndugu zangu wasiuvuke ili nishibe kwa sababu wenzangu walikuwa wanakula matonge makubwa, leo nimekuwa mkubwa."

Yupo aliyeandika meseji staili ya kula wakati taa yenyewe ni kibatari.

"Hakikisha taa haizimi na ipo karibu muda wote tukio la likiendelea, na ikizimika tu, mkono unakwenda kuziba nyama isichukuliwe." Meseji ya mwisho imeandiwa hivi.

"Kwetu mtoto ukichukua nyama kubwa utakatwa jicho na mama mpaka utajuta kuzaliwa."