Hata hivyo, hivi karibuni Mahakama Kuu Masijala Kuu, Dar es Salaam, ilibadilisha vifungu vya sheria vinavyoruhusu kuwapo kwa wagombea wa aina hiyo ili kila anayewania uongozi, apande jukwaani kunadi sera kwa wananchi.Kutokana na uamuzi huo, Nipashe imezungumza na baadhi ya wadau wa siasa ili kupata mtazamo wao kuhusu kile kilichofanywa na mahakama.Miongoni mwao ni mwanasiasa mkongwe Thoms Ngawaiya.
Huyo ni kada wa CCM, ambaye awali alishadumu katika ngome ya upinzani ikiwamo Chama Cha Tanzania Labour (TLP) chini ya Mwenyekiti, marehemu Agustino Mrema, sasa anapongeza uamuzi wa mahakama, kwa hoja kwamba unakwenda sawa na kile ambacho Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akikifanya cha kuimarisha demokrasia.
Ngawaiya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA) anasema mahakama haina budi kupongezwa kwa uamuzi huo.Anasema kulikuwapo na mchezo mchafu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi wa kubeba baadhi ya wagombea kwa kukataa kupokea fomu za wengine, ili wanaowataka wapite kirahisi.
"Bila kujali itikadi za vyama vyetu, tuipe mahakama hongera kwa uamuzi huo wa busara, kwani unakwenda sawa na kile ambacho Rais Samia anakitaka cha kuimarisha demokrasia nchini," anasema Ngawaiya.
Anasema imedhihirisha jinsi inavyosimamia haki, kwa kuwa kulikuwa na njama za wazi zilizokuwa zikifanyika za kuzuia wagombea wengine wasichaguliwe an badala yake wale wasiotakiwa wanapata uongozi,
"Mfano, mgombea anachukua fomu lakini wakati wa kuirejesha anaambiwa msimamizi ameenda kujisaidia, anasubiri hadi usiku bila msimamizi kurudi au anaambiwa kuwa muda wa kupokea fomu umeisha, lengo likiwa ni kubeba baadhi ya wagombea," anasema.
Kada huo anasema ipo haja kwa mahakama kuendelea kuondoa sheria zote zilizokuwa kama kichaka cha kujificha wale wanaotafuta uongozi kwa ujanja ili kuimarisha utawala bora unaoutaka Rais Samia.
"Mimi ni kada wa CCM, lakini kwenye ukweli ni muhimu kuusema ili kusaidia wenzangu kuachana na mbinu ambazo wakati mwingine zinasababisha kupata viongozi ambao hawakubaliki," anasema.
WANAOSAKA HAKI
Dk. Anna Henga ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambaye anasema kwa uamuzi huo, sasa haki ya kuchagua na kuchaguliwa itapatikana.
Anasema mgombea kupita bila kupingwa ni sawa na kumnyima mpigakura haki yake ya kuchagua mtu anayemtaka amuongoze, na kwamba kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa.
"Kwa mtindo wa kupita bila kupingwa, maana yake ni kwamba baadhi ya wagombea wanakosa haki ya kuchaguliwa na pia wapigakura wanakosa haki ya kuchagua," anasema Dk Anna.
Anasema yeye alikuwa miongoni mwa Watanzania walioumia katika uchaguzi wa serikali za Mitaa mwaka 2019 baada ya kwenda kupiga kura na kuambiwa kuwa mgombea amepita bila kupingwa.
Una uhakika gani kwamba huyo aliyepita bila kupingwa anapendwa? Tufike wakati sasa haki ya kuchagua au kuchaguliwa ichukue mkondo wake ili tupate viongozi tunaowataka," anasema.
PENYE UTATAMwanasheria na pia Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Bob Wangwe, anasema pamoja na uamuzi huo, lolote linaweza kutokea la kutokukubaliana na mahakama hiyo."Ilitakiwa iwe hivyo kwa mujibu wa sheria zetu, lakini kwa sababu ya kutokuwa na tume huru ndio maana kumekuwapo na viongozi wa aina hiyo kuanzia serikali za mitaa, madiwani na wabunge," anasema.
Anaongeza kuwa suala hilo pia bado lina utata, kwa madai kwamba inawezekana Mwanasheria Mkuu wa Serikali akakata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama na hivyo akashinda.
Anafafanua kuwa uamuzi unaweza kukatiwa rufaa na mahakama ya juu nayo ikatengua, hivyo Watanzania wakajikuta wakiendelea kuwa ndani ya utaratibu wa baadhi ya wagombea kupita bila kupingwa.
"Binafsi ninapenda watu washindane siyo kubebwa, ili wananchi wapate viongozi wanaotaka, hivyo uamuzi huo ungeheshimiwa ingawa inawezekana ukakatiwa rufaa. Kwa mantiki hiyo siwezi kushangilia, kwa sababu lolote linaweza kutokea hasa kukatiwa rufaa," anasema.
KESI ILIVYOKUWA
Mahakama ilifikia uamuzi huo katika hukumu yake ya kesi ya kikatiba, iliyofunguliwa na mwanasiasa, mwanachama wa chama cha ACT–Wazalendo, Joran Bashange, baada ya kukubaliana na hoja zake.Bashange alifungua kesi hiyo Mahakama Kuu Masijala Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akipinga kuwepo kwa wabunge na madiwani wanaotangazwa kupita bila kupingwa.
Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 19 ya mwaka 2021, Bashange alikuwa akihoji uhalali wa kikatiba wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Sura 343 kinachoruhusu kuwapo kwa wabunge wanaopita bila kupingwa.
Pia alikuwa akihoji uhalali wa kikatiba wa vifungu vya 45(5) na 13 (7) vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292 vinavyoruhusu kuwepo kwa madiwani wanaopita bila kupingwa.
Hukumu hiyo iliyotolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo; John Mgetta (kiongozi wa jopo), Dk Benhajj Masoud na Edwin Kakolaki, mahakama hiyo inasema vifungu hivyo vinakinzana na Katiba.
Hivyo, inasema ni batili kwa kukiuka masharti ya Ibara ya 21(1) (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ambavyo imekuwa ikirekebishwa mara kwa mara.