Vita: ‘Jipu’ linalowakosesha makazi mil. 65

29Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Vita: ‘Jipu’ linalowakosesha makazi mil. 65

MACHAFUKO ya kisiasa yanayoendana na vita vya wenyewe, kwa kutumia msamiati wa Rais Dk. John Magufuli, ni ‘jipu.’

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia wakimbizi, Filippo Grandi

Kwa bahati mbaya jipu hilo ni baya zaidi kwani linasababisha janga la maafa, njaa na ukosefu wa makazi.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Wakimbizi (UNHCR), tayari watu milioni 65 duniani kote hawana makazi kutokana na janga la vita vya wenyewe.

Nusu ya idadi hiyo yaani asilimia 51 ni watoto ambao wamepotezana na wazazi au walezi wao wakati wa vita.

Kwa hesabu ya karibu, idadi hiyo ni sawa na zaidi ya asilimia 150 ya Watanzania wote; wanaotaabika na janga linaloweza kuzuilika, sababu kuu ikiwa ni misuguano ya kijamii katika sura mbalimbali kama vile kisiasa, kiuchumi au kijamii.

Kwa mfano wa nchi jirani ya Somalia, hali si shwari kwa robo karne (miaka 25) sasa, wananchi wake wakitangatanga na kuangukia maisha ya mateso kama vile ama wakimbizi au wahamiaji haramu katika maeneo mengine, mbali na kwao.

Kama walivyo baadhi ya Wasomali wanaoishi ukimbizini nchini Kenya hivi sasa, Tanzania kwa kipindi kirefu, kumeshuhudiwa raia wa nchi kama Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda kwa miaka iliyopita, wakiishi kama wakimbizi nchini.

Wiki iliyopita dunia iliadhimisha siku ya Kimataifa ya Wakimbizi na Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti iliyoonyesha kwamba idadi ya watu waliopoteza makazi ya kote duniani imefikia rekodi mpya.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Ujerumani ndio nchi iliyopokea maombi mengi ya hifadhi kuliko nchi nyingine yoyote.
Chanzo cha watu milioni 65 kukosa makazi kinaelezwa kuwa ni mateso na mizozo katika nchi kama vile Syria na Afghanistan.

Mizozo katika nchi hizo mbili imetajwa kuongeza idadi ya wakimbizi na watu walioachwa bila makazi kufikia watu milioni 65.3 hadi mwishoni mwa mwaka jana, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, idadi hiyo ni kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambapo watu milioni 60 waliachwa bila makazi.

Aidha, takwimu za UNHCR zinaonyesha kuwa mwaka jana Ulaya iliyumba kutokana na ongezeko kubwa la wahamiaji, ambao waliongeza idadi ya watu waliokosa makazi kwa takribani asilimia 10.

Kutokana na hali hiyo, UNHCR yenye makao makuu jijini Geneva limewaomba viongozi wa UIaya na kwingineko duniani kuchukua hatua ili kumaliza vita ambavyo vinasababisha watu kukosa makazi.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia wakimbizi, Filippo Grandi, anasema: "Kile wakimbizi na wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediterranean na kuwasili katika fukwe za Ulaya, ujumbe ambao wanaubeba ni kuwa iwapo hautayatatua matatizo, matatizo yatakukujia. Na huo ni ujumbe mkali.”

UNHCR inasema kuwa kwa kiwango cha wastani, mwaka jana watu 24 walipoteza makazi kila dakika idadi ambayo ni sawa na watu 34,000 kwa siku kutoka idadi ya watu sita kila dakika mwaka 2005.

Idadi ya watu waliopoteza makazi kote duniani imeongezeka maradufu tangu mwaka wa 1997, na kuongezeka kwa asilimia 50 tangu mwaka wa 2011 pekee wakati vita vya Syria vilipoanza.

Aidha, takwimu hizo zinaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya wakimbizi wote walitokea nchi tatu za Syria, Afghanistan na Somalia.

UNHCR inaeleza kuwa Uturuki ndiyo nchi inayoongoza kwa kutoa hifadhi kwa mwaka wa pili mfululizo kwa kuwapa hifadhi karibu watu milioni 2.5 wengi wao wakitokea nchi jirani ya Syria.

Nchi za Afghanistan na Pakistan zilikuwa na watu milioni 1.6, wakati Lebanon na Syria, iliwapa hifadhi watu milioni 1.1.
Inakadiriwa kuwa takribani watu milioni 40.8 wanaoishi katika kambi za ndani kwenye nchi zenye migogoro.

Watunga sera na makundi ya uhamasishaji yanakiri kukabiliana na changamoto kubwa za kuwasaidia watu wengi walioachwa bila makazi.

Grandi anasema zaidi ya watu milioni moja walikimbilia Ulaya mwaka jana na kusababisha mzozo wa kisiasa katika Umoja wa Ulaya.

"Hakuna mpango mbadala kwa Ulaya katika siku zijazo, hakuna mpango mbadala. Ulaya, imekuwa na itaendelea kuwapokea waomba hifadhi. Takwimu huenda zikatofautiana. Natumai zitapungua, maana matatizo yatapungua.”

UNHCR imezitaka nchi kupambana na chuki dhidi ya wageni ambayo imeandamana na ongezeko la idadi ya wakimbizi na vizuizi vinavyowekwa na baadhi ya nchi za Ulaya zikiwamo sheria ambazo zinawazuia wakimbizi kuingia katika nchi tajiri na zenye utulivu zaidi.

Takwimu zinazozusha hofu katika ripoti hiyo zinaonyesha kuwa watoto walijumuisha asilimia 51 ya idadi ya wakimbizi kote ulimwenguni mwaka jana.

Wengi watoto hao walipoteleana na wazazi wao au walisafiri peke yao na zaidi ya maombi ya hifadhi 98,400 yaliwasilishwa na watoto ambao hawakuandamana na wazazi.

Shirika la kuwashughulikia watoto nchini Ujerumani limetoa wito wa kupewa elimu watoto wakimbizi zaidi ya 8,500 ambao wazazi wao hawajulikani waliko.

Mkuu wa shirika hilo, Thomas Kruger, amekaririwa akieleza kuwa watoto walio katika janga la ukimbizi wanakabiliwa na tishio la kuingia katika ukahaba, utumwa au hata kuuzwa kwa ajili ya biashara haramu ya viungo vya mwili.

www.guardian.co.tz/circulation