Ni hata mbunifu na mshiriki mkuu, Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, akaitolea maelezo machache, kwamba gharama si ya kubebeshwa serikali moja kwa moja, yenye ujumbe “ikianza mtaona thamani yake.” Ni kweli sasa hali ikatoa majibu.
Hapo Rais Dk. Samia akashiriki kwenye uzinduzi wa filamu ya Tanzania The Royal Tour, katika ukumbi wa Guggenheim Museum, New York nchini Marekani Aprili mwaka jana, katika ukumbi wa Guggenheim Museum.
Hapo akapata wasaa wa kuhojiwa, naye akatumia vyema fursa hiyo kuelezea uzuri wa Tanzania kufanya utalii akiwahakikishia ‘mtu hatajutia.’
Jambo mojawapo lililowavutia wengi, ni pale Rais Dk. Samia alipobainisha la ukweli na mzaha, ameendesha gari kwenye uandaaji wa filamu hiyo baada ya miaka 15 kutofanya hivyo.
Akiwa na mwongozaji maarufu wa filamu, Peter Greenberg, Rais Samia alitembelea nchini na kuonyesha wageni vivutio mbalimbali vya utalii, uwekezaji, sanaa na utamaduni vilivyopo nchini na kuwaelezea ukarimu wa Watanzania.
Pia, akawafafanulia wageni nyakati za kuzuru nchini, akiutaja mwezi Juni hadi Agosti, kipindi kisicho na mvua wala joto na kwa wanaotamani kuona makundi ya wanyama yakiwa yanahama, ingawa watalii wanaweza kuja muda wowote watakao.
Lingine, ni pale akaeleza jitihada ambazo zinafanywa kuwahamasisha waigizaji wa kike na kiume kutumia vipaji vyao na sanaa kuitangaza Tanzania.
Wakati huo akasema ameshafanya mazungumzo na nchi tano zinazoongoza kwa watalii wengi Tanzania, wakikubaliana kuchukua hatua za kuisaidia sekta utalii.
Muandaaji wa filamu, Peter Greenberg, akawaahidi uzinduzi huo wa filamu ungeendelea katika maeneo mengine ya Marekani, Rais Dk. Samia akihudhuria tukio la jijini Los Angeles.
SOKO LACHANGAMKA
Hadi kufika mwanzoni mwa Mei mwaka jana, wiki chache tu baada ya uzinduzi Marekani, matunda ya The Royal Tour yakaanza kujionyesha nchini, wadau mbalimbali duniani wakijitokeza kuja kutathimini misitu nchini kwa ajili ya biashara ya hewa ukaa.
Rais Dk. Samia akasema katika uzinduzi wa filamu hiyo nchini jijini Dar es Salaam Mei mwaka jana, kwamba tayari ameshafanya mazungumzo na wadau wakubwa wa utalii walioonyesha ishara nzuri.
“Nimefanya mikutano kadhaa na ‘giant’ (vigogo) wa sekta ya utalii, nao pia baada ya kuona hii filamu, wameahidi kuja” anasema na kuendelea:
“Filamu hii imeonyesha hali ya mazingira ya Tanzania, msitu na tayari tushapokea maombi ya watu wa hewa ukaa kuja kufanya tathmini ya msitu wote waliouona, msitu wa Tanzania, ili tuanze kuvuna fedha za hewa ukaa.”
Hadi sasa biashara ya ukaa imeshaanza kufanyika, ikiwamo mkoani Katavi ambayo ni kwa maslahi ya wakazi, ikiwa ni matunda ya moja kwa moja ya The Royal Tour.
NAFASI YA TFS
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, mwaka jana, akasema filamu ya The Royal Tour imewasaidia kuvutia wawekezaji wengi nchini kuwekeza hususan katika biashara ya hewa ukaa.
Anaongeza kuwa wadau hao wameamua kushirikiana na Tanzania kuimarisha misitu, ili iweze kuwa sehemu ya chujio la hewa chafu duniani na kupunguza mrundikano wa gesi joto inayosababisha kuongezeka kwa joto duniani.
“Eneo la biashara ya hewa ukaa limeonekana kuwavutia wawekezaji wakubwa duniani katika bara la Asia na Marekani kuja kuwekeza na tayari kuna wawekezaji waliojitokeza tuko kwenye mazungumzo nao,” anasema mkuu huyo wa TFS.
Aidha, Prof. Silayo anasema TFS imejipanga katika maeneo matatu: Kuhakikisha uhifadhi wa misitu unakuwa imara; pili kutumia maeneo ya vivutio vya misitu kuvutia wawekezaji kwenye suala la utalii; na mwisho kuhakikisha kunakuwapo uwekezaji katika viwanda vya misitu na nyuki.
MWEKEZAJI KIMATAIFA
Kazi ya Rais Dk. Samia mwaka jana kutangaza utalii nchini kupitia filamu The Royal Tour, zikaendelea kuzaa matunda kwa nchi kupokea mwekezaji mkubwa wa hoteli za kifahari nchini Marekani, Munir Walji, aliyewasili kwa mazungumzo na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana, kuhusu uwekezaji hoteli za kitalii.
Akaeleza ni miradi itakayoongeza thamani katika sekta hiyo ili kwenda na kasi ya ujio wa watalii nchini. Hapo Walji anaipongeza Tanzania kuweka mazingira bora yanayohamasisha kutangazwa na kuvutia wawekezaji.
Mtayarishaji sinema wa California Marekani, John Feist, naye akafika jijini Dar es Salaam, kutoa semina ya kuboresha kazi za filamu nchini akiwa na uzoefu wa miaka 22 iliyopita na nchi tisa, ikiwamo Tanzania.
MATUNDA YA FILAMU
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania unasema, tangu Rais Samia Samia alipozindua filamu ya Royal Tour, idadi ya watalii wanaotembelea utalii Ikolojia nchini, imeongezeka kutoka 49,000 kwa mwaka hadi 150,000.
Umesema kutokana na ongezeko hilo TFS nayo imeamua kuboresha njia za kupita watalii, maeneo ya malazi na kuwepo maeneo bora ya kupumzikia.
Mkuu wa Uhamasishaji wa TFS, Anna Lauwo katika Maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa mwaka jana anasema watalii hao walipotembelea Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia Pugu Kazimzumbwi, Dar es Salaam.
Anaitaja kuwa zao la kuunga mkono jitihada za Rais Samia, kutangaza sekta ya utalii kupitia filamu ya The Royal Tour na kuhamasisha utalii wa ndani.
“Royal Tour imehamasisha wengi kufahamu kumbe kuna utalii, kumbe Tanzania kuna kitu cha pekee ambacho sehemu nyingine hakipo na watu wameamka kumbe kuna umuhimu wa kwenda kupumzika," anasema Lauwo.
Msitu wa Pugu ulioko wilayani Kisarawe Kanda ya Mashariki, ni kati ya misitu 23 inayosimamiwa na TFS na imepandishwa hadhi.
Anafafanua yana vivutio mbalimbali, ikiwamo maporomoko ya maji, mojawapo ni ya pili kwa urefu barani Afrika, kwa urefu mita 235 inayopatikana katika Hifadhi ya Kalambo, kukiwapo utalii unaofanyika kwenye mashamba ya miti yanayosimamiwa na TFS, akitoa mfano wa utalii wa kuendesha baiskeli.
MAONI WIZARANI
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana, Juni mwaka jana akawa na ufafanuzi katika eneo hilo:“Napenda kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Rais Samia kwa juhudi zake kubwa za kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia programu ya Tanzania – The Royal Tour.
“Imeanza kuleta matunda kwa kuvutia watalii na wawekezaji kutembelea nchini, ambapo wakala wa utalii zaidi ya 30 kutoka katika masoko ya utalii yakiwamo Marekani, Ufaransa na Lithuania wamehamasika kutembelea Tanzania kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa lengo la kuvitangaza katika nchi zao.
“Vilevile wawekezaji kutoka Taifa la Bulgaria wameonyesha nia ya kuwekeza nchini kwa kujenga hoteli nne zenye hadhi ya nyota tano katika Hifadhi za Taifa Serengeti, Ziwa Manyara na Tarangire na eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
“Serikali, pia imesaini mkataba wa ushirikiano katika masuala ya utalii, biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Jiji la Dallas Marekani, mwezi Aprili, 2022, hatua ambayo itafungua fursa za usafiri wa anga kwa kuwezesha safari za moja kwa moja za ndege kutoka Tanzania hadi Dallas, Marekani na kuongeza idadi ya Wageni nchini”
Akizungumza Juni mwaka jana, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda an Biashara, Godius Kahyarara, anasema ziara za Rais Dk. Samia ughabuni, pamoja na sinema ya The Royal Tour, zimeongeza pato la nchi kutoka Dola za Marekani bilioni moja (Sh. trilioni 2.3) za awali, hadi Dola bilioni 9.2 (Sh. Trilioni 21.16).
Kahyarara anasema, pia mauzo ya bidhaa nje ya nchi katika kipindi hicho yakapaa hadi Dola bilioni 10 sawa na Sh. trilioni 23, kutoka Dola bilioni saba (Sh.trilioni 16.1)










