Tangawizi ‘yafuta’ umaskini na kuipaisha Same kimataifa

25Mar 2016
Leonce Zimbandu
Nipashe
Tangawizi ‘yafuta’ umaskini na kuipaisha Same kimataifa

MWAKA 2009 Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Same Mkoa wa Kilimanjaro, lilithibitisha Tangawizi kuwa zao kuu la biashara na kuelekeza nguvu kazi na rasilimali katika uzalishaji wa zao hilo.

tangawizi.

Hiyo ni baada ya kufanyika kwa mafunzo na warsha (maarufu kwa jina la mafunzo ya Post Osaka), kwa viongozi wa Wilaya na Halmashauri wa Mkoa wa Kilimanjaro mwaka 2006.

Mafunzo hayo yalilenga kuwapatia viongozi hao uzoefu juu ya uzalishaji wa zao hilo kutoka kwa watu wa Japan.

Kwamba mafunzo hayo yaliwahamasisha viongozi na watendaji kiasi cha kuibua fikra katika kuboresha kilimo hicho, ili kipewe kipaumbele katika uzalishaji wenye tija na kuwa na zao kubwa litakalokuwa la biashara wilayani humo.

Licha ya hayo, lakini changamoto kubwa katika uzalishaji wa zao hilo ni pamoja na Same kuwa miongoni mwa Wilaya zenye mvua chache kwa mwaka.

Kwa kiasi cha wastani wa kati ya 400-600 mm upande wa chini na 800-1200 kwa upande wa juu na joto la wastani, kiwango hicho hakitoshi katika uzalishaji wa mazao yanayohitaji mvua au maji mengi.

Kuongezeka kwa idadi ya watu, kulisababisha uhaba wa ardhi kwa ajili ya kilimo, upungufu wa maji ya umwagiliaji katika kilimo uliosababishwa na uharibifu wa mazingira.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa miundombinu ya barabara kutoka shambani hadi sokoni ilikuwa sio mizuri, hali hiyo imesababisha bei ya mazao ya biashara na chakula kuwa ndogo.

Tangawizi iliuzwa kwa bei ya Sh. 150 hadi Sh. 250 kwa kilo moja ikiwa mbichi, changamoto hizo zilisababisha kushuka kwa uzalishaji na kipato kwa wananchi wa wilaya ya Same.

Kutokana na bei hiyo ndogo, viongozi wa wilaya na watendaji waliwahamasisha wananchi kulima tangawizi kutoka kata tatu hadi kufikia kata 12 na kukubali kuanzisha chama cha ushirika kilichosajiliwa kwa jina la Mamba Ginger Growers Rural Co-operative Society Ltd.

Lengo la chama hicho ni kusimamia na kuinua uzalishaji wa zao la tangawizi, baada ya uamuzi huo uzalishaji wa zao hilo umeongezeka kutoka tani 7,000 kwa mwaka 2008 hadi tani 12,000, mwaka 2011.

HALI YA SOKO
Halmashauri kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi (wakati huo, hivi sasa Tamisemi ipo chini ya Ofisi ya Rais) na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, kupitia programu ya AMSDP, iliteua shirika la Faida Mali (Partner Agent), ili kufanya utafiti wa masoko.

Kutokana na utafiti huo Wafanyabiashara wa ndani wamehamasishwa kununua zao la tangawizi kupitia chama cha ushirika baada ya kutunga sheria ndogo ya kudhibiti bei ya soko ili mazao yote yakusanywe na kuuzwa kupitia chama cha ushirika.
Awali, bei ya tangawizi mbichi kilo moja iliuzwa kati ya Sh. 150 na Sh. 250, lakini baada ya kuboresha uzalishaji na kuanza kusindika tangawizi ya unga (ginger powder), kilo moja iliuzwa kwa bei ya Sh. 4,000.

Kupitia utafiti uliofanyika na kubaini kwamba wateja wengine wanahitaji ‘chips’ (sliced ginger), kwa ajili ya kutengeneza dawa, hivyo kiwanda kilijengwa kwa lengo la kuongeza ubora, ili kukidhi viwango vinavyohitajika katika masoko.

Matumizi ya ardhi ni ya kitaalamu, eneo dogo linazalisha kwa wingi na mbinu za uzalishaji zimeboreshwa, miundombinu ya umwagiliaji imejengwa (ndiva) na maji yanatumika katika utaratibu mzuri.

Miundo mbinu ya barabara imeboreshwa na kujenga barabara mpya kwenda kwenye maeneo ya uzalishaji, ikiwamo eneo la masoko na kiwandani.

MATOKEO
Kiwanda cha kusindika tangawizi Same kimeajiri wafanyakazi wa kudumu 30 na vibarua 100, wafanyakazi na vibarua wanatoka katika kata zinazolima zao la tangawizi.

Hivyo kipato cha mwananchi mmoja mmoja na kaya kimeongezeka baada ya kupata ajira, pia pato la Halmashauri liliongezeka kutoka Sh. 10,000,000 hadi Sh.300,000,000 kwa mwaka.

Kutokana na kukidhi viwango vya ubora wa kimataifa wamefanikiwa kupata masoko ndani na nje ya nchi kama Uholanzi na nchini Kenya.

Kiwanda hicho kimejengwa katika kata ya Mamba Myamba wilayani Same, baada ya wananchi kukubali kutoa ardhi yao wenyewe, hivyo kwa kuthamini viwanda vyetu utaalam uliotumika kujenga kiwanda hicho umetoka ndani ya nchi yaani Shirika la kuendeleza viwanda vidogo (Sido).

Ikumbukwe kuwa hicho ni kiwanda pekee nchini cha kusindika tangawizi na kina uwezo wa kusindika tani tatu za tangawizi mbichi kwa siku.

UZOEFU KUTOKA JAPAN
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Same, Jeseph Mkude, ambaye hivi sasa ni Mkurugenzi Halmashauri ya Muleba, anasema wamejifunza mambo mengi nchini Japan.

“Lakini katika eneo hili Wilaya ya Same wamefanya mambo ya kuigwa na pengine kutumia uzoefu waliopata kwa kuthamini mazao ya eneo unalotoka Proud of Ging,” anasema.

Anasema Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zinapaswa kuwa karibu na wananchi na kuwasaidia wanapoonesha juhudi ili kuinua uchumi.

“Wananchi washiriki kwa kutoka nje ya box (Think globally act locally), ili kutambua rasilimali walizokuwa nazo na kuziendeleza,” anasema.

MIKAKATI ENDELEVU
Mkurugenzi huyo anasema pamoja na kuhamishiwa Halmashauri nyingine, lakini mafunzo aliyoyapata Japan atawashirikisha wananchi wa Same ili kuendeleza ushirikiano na jamii kwa kuwapatia wakulima wa tangawizi utaalamu na kuwahamasisha kujiunga katika ushirika.

Kuihamasisha jamii kutambua na kuthamini mazao na rasilimali zao ili kudumisha ushirikiano katika kuboresha mazao ya kilimo katika kuyaongezea thamani.