Surua kuua watoto, yamkurupusha waziri kuibukia Katavi na kampeni

02Mar 2023
Yasmine Protace
KATAVI
Nipashe
Surua kuua watoto, yamkurupusha waziri kuibukia Katavi na kampeni

SASA katika baadhi ya maeneo nchini kumetangazwa mlipuko wa maradhi surua, ambayo yaliwahi kuzuka zama zilizopita na hasa kwa watoto, ikiwa na kasi kubwa ya uambukizaji.

Pia, kuna wakati ikapewa jina Rubeola, ikibeba sifa katika homa na ugumu wa kupumua. Kitaalamu, inatajwa kuwa ya hatari na yenye historia ya kuua, hususan Afrika na Kusini- Mashariki mwa Asia, waathirika wakuu ni watoto. Vilevile, inatajwa kuzuilika kirahisi, ikianzia na chanjo.

Surua inaenezwa zaidi na virusi aina ya ‘morbillivurus paramyxvirus’ vinavyoenea haraka kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, ikipitia kwenye hewa na hasa mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya.

Ni ugonjwa unaoathiri watu wa rika zote, licha ya kuwa zaidi ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Sasa kuna mlipuko unaotangazwa katika mikoa mbalimbali, ikiwamo Katavi.

WAZIRI UMMY

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anasema serikali sasa imewaelekeza wazazi na walezi mkoani Katavi, kuwapeleka watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wakapate chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa surua.

Agizo hilo alilitoa akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya na kuzindua kampeni ya kuongeza kasi na hamasa ya chanjo ya surua kwa Halmashauri ya Mpimbwe. wilayani Mlele, mkoani Katavi.

Ummy anasema, anayo mamlaka ya kisheria kupitia Sheria ya Afya ya Jamii kuamua chanjo za watoto za kuwakinga na surua si ya lazima, hivyo anawataka wakuu wa wilaya na mikoa kuwachukulia hatua wazazi na walezi watakaoshindwa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo ya surua.

"Wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, mhakikishe watoto wanapata chanjo,kama kuna mzazi au mlezi atashindwa kumpeleka mtoto kupata chanjo achukuliwe hatua," anasema.

Anaeleza msimamo wake kwamba, hatokubali kwa nafasi yake ya serikali, kuona watoto wanapoteza maisha, ilhaIi wana uwezo wa kuwakinga kwa kuwapatia chanjo ya surua mapema.

Waziri anawaelekeza wazazi na walezi mkoani Katavi kupeleka watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano kupata chanjo ya kujikinga na surua, alipokuwa anazindua kampeni ya kuongeza kasi na hamasa ya chanjo ya surua katika Halmashauri ya Mpimbwe, wilayani Mlele.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy, kuna watoto zaidi ya 400,000 waliokosa chanjo hiyo, huku tayari kuna vifo vilivyoripotiwa hadi sasa 13, kati yake 11 vimetokea majumbani na viwili hospitalini, sababu kuu ni wagonjwa kucheleweshwa kufika katika vituo vya huduma za afya.

“Leo tupo hapa Majimoto Mpimbwe kuwaunga mkono wana Mpimbwe na wana Majimoto, ili tuishinde surua. Lazima, watoto wote umri chini ya miaka mitano wakamilishe dozi ya chanjo ya surua”, anaagiza.

Pia, anafafanua takwimu ilivyo, katika kila watoto 100 wanaougua surua katika Halmashauri ya Wilaya Mpimbwe, 40 wanatoka katika Kata ya Majimoto.

Hata hivyo, Waziri Ummy anasema hadi sasa kazi ya chanjo inaenda vizuri na kupitia ziara hiyo, amezindua msafara wa kampeni ya bodaboda na magari 10 yanayotoa elimu na hamasa ya chanjo kwa wananchi Mpimbwe, ili kusambaza uelewa wa kupeleka watoto kupata chanjo ya surua mapema.

Pia, anasema kuna magari mengine matano yatakayopelekwa katika Halmashauri ya Wilaya Mlele na matano Halmashauri ya Wilaya Tanganyika, kufanya kazi hiyo wakipita ‘nyumba kwa nyumba’ kuhakikisha kila mtoto wa umri chini ya miaka mitano akapatiwe chanjo, akihimza umakini na ujasiri wao kulifanikisha hilo.

Waziri Ummy anaelimisha kwamba, kwa aliyepata chanjo, hata akipata surua, haitakuwa kali tofauti na asiyechanjwa, akitoa mfano wa hatua kama hiyo imewanusuru wengi na maradhi Uviko-19.

Pia, anawataka waganga wa tiba asilia, nao washiriki kuhimiza wateja wao chanjo ya surua, kwa kuwaelekeza kwenda kwenye vituo vya afya wakahudumiwe.