Katika makakati huo, Sido imeainisha fursa za uwekezaji hadi katika ngazi ya wilaya nchini, huku mameneja wa mikoa wa shirika hilo wakiwa na malekezo maalum ya kusaidia ufanikishaji wa mkakati tajwa.
Akizungumza na Nipashe ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa Sido, Injinia Omary Bakari, anasema wameshajipanga na moja ya hatua wanazoendelea nazo, ni kuhamasisha wananchi kuwekeza katika maeneo yao.
Mkurugenzi huyo anataja baadhi ya mambo wanayoyapa kipaumbele katika mkakati huo, ni umuhimu wa nembo, vifungashio, mikopo na vituo vya mauzo .
Injinia Bakari anasema mkakati unaowawezesha wazalishaji wenye viwanda vidogo kukopa kuanzia Sh. milioni sita hadi Sh. milioni 50, kuanzia mwaka ujao wa fedha unaoanza mwezi ujao.
Bakari anasema Sido itakuwa na majengo maalum maarufu kama ‘industrial cluster’ itakayowahudumia wazalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Mtendaji huyo mkuu anasema mkakati ulioko sasa ni kuwa na majengo maalumu ya biashara katika mikoa minne anayoitaka kuwa ni: Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Morogoro.
“Tumekubaliana kwamba mameneja wote wa mikoa watambue fursa za kiuwekezaji kwa maana ya malighafi zilizopo kwenye wilaya zao, ili tuwaambie wananchi nafasi waliyo nayo ya kuwekeza,” anasema mkurugenzi huyo
Anasema Sido inatambua fursa za uwekezaji katika maeneo ya wananchi na kwamba wakazi wa eneo husika wanapaswa kuwekeza, badala ya kusubiri wawekezaji wa nje.
“Kwa mfano, ukienda Rombo unakuta ndizi ni nyingi sana kwa hiyo tunategemea Mtanzania atatumia fursa ya uwepo wa malighafi ya ndizi kutengeneza bidhaa mbalimbali. Karatasi au ‘crips’ na kadhalika,” anasema.
Anafafanua kuwa uwekezaji wa kwenye eneo ambalo malighafi inapatikana, inapunguza gharama za uendeshaji na kumhakikishia mwekezaji malighafi.
“Tunachofanya sasa ni katika kila wilaya, kuainisha fursa ambazo zipo hata uongozi wa wilaya na wenyewe wanaziona, ili tuweze kuzitumia katika uhamasishaji wa uendelezaji na uanzishaji wa viwanda,” anasema.
Anaongeza: “Hasa tunachotaka kutumia ni ‘industrial cluster development approach’...tunataka ‘tu-facilitate’ (tuhamasishe) watu ambao wana-focus in the same sector (wenye mtazamo katika sekta moja).”
Bakari anatoa mfano huo kwa kuoanisha na eneo la mfano la uzalishaji ndizi kwamba inawezesha kuzalishwa na kusambazwa kwa wingi, katika maeneo baadhi ya maeneo.”
Mkurugenzi huyo anasema Sido ina wataalam wa kushauri namna ya kuandaa na kuanzisha viwanda vidogo na vya kati.
Pia wana idara ya utoaji taarifa na masoko kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwamo wanaohitaji bidhaa za kila aina.
“Tunatoa huduma ya kitaalam, sisi (Sido) tutakuambia teknolojia inapatikana wapi, gani, utaendesha biashara yako namna gani na wapi utaweza kupata mikopo,” anafafanua.
MIKOPO
Akizungumzia mikopo, Bakari anasema Sido ina tawi linalokopesha wajasiriamali kwa riba nafuu na anasimulia:
“Ili uweze kukopesheka, lazima uwe umeweka rekodi zako vizuri; lazima uwe na andiko la biashara linaloeleweka na wataalam wa Sido watakusaidia.”
Anafafanua kwamba kwa mwaka wa fedha wa 2016/17, serikali imetenga Sh. bilioni 2.4 za kusaidia uendelezaji viwanda vidogo na vya kati, ambazo zitatolewa kama mikopo.
Bakari anasema fedha hizo zitaingizwa katika Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF), ili kuwasaidia wajasiriamali katika sekta ya uzalishaji, kupata mikopo kwa njia rahisi na riba nafuu.
Mkurugenzi huyo wa Sido anasema nia ni kuchochea ukuaji uchumi, kutengeneza ajira na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
“Tunasubiri kamati ya NEDF ikae na kuamua namna gani Sido inaweza kutumia fedha hizo, kwa kutoa mikopo kwa wazalishaji wadogo na wa kati,” anasema.
Kiongozi huyo anasema wazalishaji wataweza kukopeshwa hadi Sh. Milioni 50, ikilinganishwa na awali walikuwa wanakopeshwa kuanzia Sh. 500,000 hadi Sh. milioni sita.
“Tunamalizia kubuni mbinu nyingine ya kumsaidia mjasiriamali ambaye ana soko lakini hana ‘working capital’ (mtaji wa kuendeshea) ya ku-fulfill (kutimiza) lile soko.
”Tunasema ukiwa na mkataba ambao umesaini wa wewe ku-supply (kuhudumia) na unakosa mtaji, tutafanya makubaliano na wenye malighafi ambazo unazihitaji ili tukudhamini uchukue kisha utalipa baadaye…lakini tukijua masharti ya mkataba wako,” anasema.
UFUNGASHAJI
Bakari anasema Sido ina jengo la kufunga bidhaa mbalimbali (packaging center) na mashine za kisasa kwa ajili ya kazi hiyo.
“Packaging center (kituo cha ufubgashaji). Hii dhumuni lake ni kutoa huduma mbalimbali kwa ajili ya wajasiriamali,:” anasema na kuongeza:
“Tunafanya mazungumzo na wazalishaji wa vifungashio mbalimbali kutoka Misri, wazo ni kukubaliana nao ili Sido iwe msambazaji wao kwa nia ya kuhakikisha wajasiriamali wetu wanapata vifungashio bora na kwa bei nafuu.”
Anasema Sido imeanza kuzalisha wa vifungashio vinavyopatikana kwenye ofisi mbalimbali ya mikoa yote na katika kituo cha vifungashio, kuna mashine za kufunika chupa zinazofanana na za soda, mvinyo, kufunga mifuko ya nailoni na karatasi.
Kwa mujubu wa Bakari, zipo mashine za kubandika nembo za bidhaa zinazomuwezesha mjasiriamali kutengenezewa nembo na kuichapisha.
Inawlezwa katika utengenezaji huo, kuna mtaalamu wa kushauri mambo mbalimbali, kuanzia utengenezaji wa nembo hadi aina ya kifungashio, kulingana na bidhaa inayozalishwa.
AJIRA
Bakari anasema kuwa, Sido inahamasisha uwekezaji kwenye viwanda vidogo, ikiamini hiyo ndio tiba ya tatizo la ajira na kuwahamisha watu kuondoka katika fikira ya kuajiriwa.
Anasema Sido inalea watu wenye mawazo ya kuanzisha viwanda au biashara na kuhakikisha mawazo hayo yanafanyika kwa vitendo, hivyo vijana wanapaswa kutumia fursa hizo.
Mkurugenzi anasema kinachofanywa sasa na mameneja wote wa mikoa, ni kuchambua fursa na malighafi zilizopo kwenye mikoa yao, ambazo watazitangaza kwa umma hivi karibuni.
MZIZI WA KIWANDA
Majengo maalum yanayopewa jina la kitaalamu ‘Industrial Cluster’ yanayolenga kuhudumia wajasiriamali wa aina zote, wakiwamo wanaozalisha bidhaa za ngozi, vyakula, manukato, viungo na kazi za mikono.
"Tunataka ukiingia ‘industrial cluster’ unakutana na wazalishaji mfano wa samani wote sehemu moja. Ukienda upande mwingine, unakuta wa ‘spices’ (viungo) vya kila aina, kwingine wa manukato; na kadhalika," anasema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu– Bakari, ni kuhakikisha zinapokuja tenda kubwa kwa mzalishaji mmoja ambaye hatoweza kuimudu peke yake, wanaungana mara moja na kuzalisha bidhaa kwa wakati.
"Mfano halmashauri inasema inataka madawati 1000. Ni wazi kwamba mtu mmoja hawezi kuzalisha kwa mara moja.
Kwa hiyo, wakiwa wengi wanaungana ndani ya muda mfupi wanatengeneza na kuyapeleka yanapotakiwa," anasema.
Bakari anaongeza kuwa: "Hivyo hivyo kwenye ngozi, labda inatokea shule inahitaji viatu kwa wanafunzi 2000, wanaangana wazalishaji kadhaa wanazalisha haraka viatu na ku-supply (kuhudumia)."
Bakari anasema ujenzi wa majengo hayo, umepangwa kuanza mapema mwezi ujao, ambao ni mpya wa fedha.










