MASHUJAA WA SELIMUNDU
PRISCILLA Chassam, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania, anasema wamejikita kutoa elimu katika jamii baada ya kuona ugonjwa huo unaenea kwa kasi kutokana na ukosefu wa elimu.
"Kumekuwa na migogoro kwenye familia. Mtoto akipatikana na sikoseli, lawama zinamwangukia mama, anatelekezewa familia na mtoto analelewa katika mazingira yasiyo salama pasipo kuelewa kuwa wazazi wote wanachagia kupatikana ugonjwa huo, hivyo wanapaswa kushirikiana wote katika malezi," anasema.
Anasema ni wakati mwafaka kwa jamii kuwa na tabia ya kufuata huduma sahihi za afya kwa mtu mwenye tatizo hilo. Kuwafungia ndani au/na kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji wagonja wa selimundu ni kuhatarisha maisha yao.
"Tutaendelea kutoa elimu kwenye jamii ili kupunguza vifo vitokanavyo na sikoseli. Mpaka sasa tunatoa huduma kwa watu zaidi ya 300. Serikali itafute namna ya kufanya kampeni kwenye jamii hasa vijijini na kuhakikisha elimu juu ya sikoseli inawafikia wananchi ipasavyo.
"Kwa baadhi ya wilaya za vijijini tatizo ni kubwa. Mfano, tulikwenda Busega, walipimwa watu 365, nusu yao walikuwa na ugonjwa ya sikoseli, wengine wana chembechembe na wachache wakiwa hawana chembechembe wala sikoseli, Hapo utaona jinsi gani ugonjwa huo ulivyo mkali. Tunaendelea kutafuta fedha kuyafikia maeneo mengine ya vijijini," anasema.
MADAKTARI BINGWA
Daktari Bingwa wa Magojwa ya Watoto na Mtaalamu wa Selimundu katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando, Emmanuela Ambrose, anabainisha kuwa tatizo la ugonjwa huo ni kubwa nchini.
Bingwa huyo anabainisha kuwa utafiti unaonesha asilimia 75 ya watoto wanaozaliwa na sikoseli duniani wanatoka Afrika. Tanzania ni nchi ya tano duniani na ya nne Afrika kwa tatizo hilo, sasa inao wagonjwa takribani 14,000 waliozaliwa na ugonjwa huo na wengi wao wakitokea Ukanda wa Ziwa Victoria.
Dk. Emmanuela anafafanua kuwa hospitali hiyo kwa sasa ina zaidi ya watoto 1,000 ambao wanahudhuria kliniki kwa mwaka. Kila Jumatatu wanawaona watoto 30 hadi 50 huku Ijumaa wakiwaona watoto 50 hadi 80.
"Tunatoa ushauri na kuwaelimisha wazazi na walezi kuwa ugonjwa wa sikoseli hurithiwa kutoka kwa wazazi wote wawili; baba na mama. Elimu zaidi hutolewa kwa jamii jinsi ya kuepuka kupata mtoto mwenye tatizo hilo.
"Utafiti zaidi unahitajika ili kueleza bayana ukubwa wa tatizo hili kwani ugonjwa huo kwa sasa umekuwa mada kubwa kwa sababu watoto wengi wanazaliwa wakiwa na shida hiyo. Tatizo hili ni kubwa kwa sasa kutokana na watu kutokuelewa wamerithi chembechembe za ugonjwa huo, wanatambua tu pale wanapopata mtoto mwenye shida hiyo.
"Kusubiri mpaka upate mtoto ni kuchelewa, wanapaswa watambue hali zao kabla ya kubeba ujauzito. Kama wote wana urithi wa sikoseli wafanye uamuzi mapema, hivyo ni vyema wakapima kabla ya kuingia kwenye ndoa.
"Pia mtoto anapozaliwa apimwe, akikutwa na tatizo hilo anaanzishiwa kliniki na matibabu ya sikoseli mapema ambayo yatamsaidia kutibu matatizo yote yanayotokana na ugonjwa huo, hivyo kumfanya kuishi muda mrefu," bingwa huyo anashauri.
Njia nyingine ya kukabiliana na ugonjwa huo, Dk. Emmanuela anashauri mama mjamzito anapoanza kilinki apimwe hali yake, akionekana amebeba chembechembe iandikwe kwenye kadi yake ya cliniki 'AS' (ana chembechembe za selimundu), 'SS' ( ana selimundu) na AA (mtu asiyekuwa na chembechembe wala sikoseli).
"Watoto wote watakaozaliwa na mama mwenye SS au AS, lazima wapimwe hali zao watakapozaliwa. Hiyo itasaidia kuondokana na ugonjwa huu. Kupima watoto wote pia kutasaidia kupunguza gharama kwa nchi kukabili ugonjwa huu," anashauri.
Bingwa huyo pia anashauri kuwe na somo mahususi la selimundu shuleni kuchochea jitihada za kukabili ugonjwa huo. Upimaji wa selimundu ufanyike hadi shuleni ili watoto wajue hali zao wakiwa wadogo. Itawasaidia kutambua hatari iliyoko mbele yao na watakuwa makini.
Dk. Emmanuela anaweka wazi kuwa matibabu ya selimundu ni ghali, akiutaja ni ugonjwa wa kudumu. Mzazi lazima awe na fedha na hasa kwa wale walio juu ya miaka mitano.
Anafafanua kuwa muda mfupi baada ya kuzaliwa, mtoto akigundulika ana ugonjwa huo, anaanzishiwa dozi ya Folic acid inayosaidia uzalishaji damu. Pia dozi ya Penicillin V inayozuia magonjwa yanayosababisha vifo hasa kwa watoto chini ya miaka mitano na anapofikisha umri wa miezi tisa wanahakikisha ameanza dozi ya Hydroxyurea.
Dk. Emmanuela anasema anatamani serikali isaidie kutoa dawa kwa wagonjwa hasa dozi ya Hydroxyurea inayosaidia kupunguza shida zinazotokana na sikoseli ikiwamo maumivu, kulazwa mara kwa mara kuongezwa damu na kuzuia kupata kiharusi (kupooza) na damu kuwa nyepesi.
"Kupandikiza uroto ndio tiba, lakini ni gharama sana. Pia lazima uroto huo utoke kwa ndugu yako unayeendana naye kibaiolojia. Hapa nchini ni watoto wanne tu wamefanyiwa na wote wako salama, lakini nina imani wengi zaidi watafanyiwa hasa ambao hydroxyurea haijawa msaada kwao," afafanua.
KULIKONI KANDA YA ZIWA?
Dk. Emmanuela anaeleza kuwa Kanda ya Ziwa ni moja ya kanda za kitopikia ambazo zina tatizo kubwa la malaria, akiwa na ufafanuzi kuwa mwili wa binadamu umeshabuni njia ya kupambana na malaria kwa kusababisha hitilafu katika vinasaba na kuleta urithi wa sikoseli.
"Kwa hitilafu hii warithi waliweza kuishi/kujikinga na ugonjwa wa malaria uliokuwa chanzo kikubwa cha vifo. Hitilafu hiyo ikirithiwa kutoka kwa wazazi wote wawili ndio huleta ugonjwa wa sikoseli. Kuoana wenyewe kwa wenyewe katika sehemu za kitopikia imekuwa ni chanzo cha ongezeko la ukubwa wa tatizo.
"Pia kwa sasa utandawazi, watu kusafiri na kuishi na kuchanganyika maeneo mengine kumefanya tatizo la sikoseli kuwa sehemu nyingi nchini na duniani.
“Ndoa za mitala ndizo zinaleta urithi, sikoseli na Ukanda wa Kitopikia hasa Mwanza. Kitu cha muhimu ni kufanya vipimo kabla ya kuoana na ikibainika mna urithi wa sikoseli, bora msioane ili kuepuka nafasi ya kupata mtoto mwenye ugonjwa wa sikoseli," anashauri.
Hoja ya kuepuka kuoana wenye urithi wa sikoseli, inaungwa mkono na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Kansa kwa Watoto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Shakilu Jumanne, anayesema kuwa licha ya mikakati mingi ya kupunguza makali ya ugonjwa huo, hali ni mbaya nchini.
Anasema watoto wengi wanaendelea kuteseka na ugonjwa huo kutokana na uelewa mdogo wa wazazi kuhusu namna ya kuepuka mazingira yanayoweza kuchochea seli nyekundu kubadilika umbo na kuwa mundu.
Kama ilivyotolewa angalizo na mtangulizi wake Dk. Emmanuela, Dk. Jumanne pia alitahadharisha ndoa za watu wenye vinasaba vyenye ugonjwa huo zinachochea watoto kuzaliwa na ugonjwa wa sikoseli kwa sababu wote wanakuwa na vichocheo vya kurithi.
"Kila mwaka hapa nchini watoto 14,000 huzaliwa na ugonjwa huu huku watoto 10,000 kati yao huzaliwa mikoa ya Kanda ya Ziwa. Mkoa wa Mwanza tu wanazaliwa watoto 1,700 kwa mwaka wenye tatizo hili," anatahadharisha.
Takwimu hizo zina maana kwamba, kila siku watoto 39 wanazaliwa wakiwa na ugonjwa wa selimundu nchini. Kati yao, 28 (asilimia 72) huzaliwa mikoa ya Kanda ya Ziwa huku Mkoa wa Mwanza pekee ukiwa na wastani wa watoto watano kwa siku.
Kuhusu matibabu ya ugonjwa huo, Dk. Jummanne anaungana na Dk. Emmanuela kwamba njia ya ukakika zaidi ni kupandikiza uroto kutoka kwa ndugu wa karibu kwenda kwa mtoto mwenye tatizo.
"Matibabu ya sikoseli ni ghali hususani katika kupandikiza uroto. Huduma hii kwa mgonjwa mmoja hugharimu Sh. milioni 30 hadi 40, jambo ambalo ni gumu kwa Watanzania wenye maisha duni.
"Hivyo, ili kuepuka haya, lazima jamii ikubaliane kupima kabla ya ndoa ili kuwaepusha watoto wetu maumivu wanayopitia," bingwa huyo anashauri.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sikoseli Wizara ya Afya, Dk. Asteria Mpoto, anabainisha kuwa serikali inafanya jitihada kuweka unafuu kwenye huduma za sikoseli ikiwa ni pamoja na kuimarisha matibabu ya kibingwa ya kupandikiza uroto.
Anabainisha kuwa kwa kuanzia, serikali imeanza kugharamia matibabu ya kibingwa kwa watoto wenye ugonjwa huo kwa kupandikiza uroto ili kuwapunguzia maumivu wanayoyapata.









