Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, Tanzania ina vyama 22 vyenye usajili wa kudumu na vyama vitatu vyenye usajili wa muda.
Pamoja na ‘utitiri’ huo wa vyama, ni vyama vitatu ndivyo vinavyoonekana kufanya vizuri kwa kuwa na Wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa na vijiji; madiwani, wabunge na mameya.
Vyama ambavyo vinaendelea kutikisa siasa za nchi ni CCM kinachooingoza dola, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Vyama vingine kama UPDP, SAU, TADEA, UDM, CCK, AFP, Demokrasia Makini, TLP, APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, UDP, DP, ADC, Chaumma, NRA na ACT-Wazalendo, ni vyama ambavyo bado ‘vinachechemea’ kwenye kuongoza dola.
Vyama hivi ukiondoa ACT-Wazalendo yenye mbunge mmoja na Halmashauri; vilivyosalia havina hata mwenyekiti mmoja wa serikali ya mtaa au kijiji; mjumbe kwenye ngazi hiyo wala diwani.
ROBO KARNE NA UKAWA
Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, CCM bado imeendelea kupata madiwani, wabunge na wajumbe wengi wa serikali za mitaa na vijiji.
Takwimu za uchaguzi mkuu wa mwaka jana zinaonyesha kuwa Chadema ndicho chama cha upinzani chenye nguvu zaidi kikiwa na wabunge 70 ambao ni 34 wa majimbo na 36 wa Viti Maalum.
CUF nayo ina wabunge 45 ambao ni 35 wa majimbo na 10 wa Viti Maalum, NCCR-Mageuzi ikiwa na mbunge mmoja wa
jimbo na ACT-Wazalendo ambayo haiko kwenye muungano wa Ukawa ikiwa na mbunge mmoja.
Vyama 18 havina mbunge, diwani wala viongozi kwenye serikali za mitaa.
Katika uchaguzi huo, kwenye urais CCM iliibuka na ushindi wa asilimia 58.46, ikifuatiwa na Chadema iliyopata asilimia 39.97.
Kura za Chadema zimekuwa nyingi hasa kwa kuzingatia kuwa ilikuwa inaungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa.
UBUNGE
Ripoti ya uchaguzi inaonyesha kuwa CCM ilipata asilimia 73.86, ya wabunge ikifuatiwa na Chadema ambayo ilipata asilimia 13.26, CUF asilimia 12.12 na vyama vya ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi vilipata asilimia 0.38 kila kimoja.
Kwenye Udiwani nako CCM inaongoza kwa kupata asilimia 72.86, ikifuatiwa na Chadema (asilimia 20.3), CUF (asilimia 5.37), ACT-Wazalendo (asilimia 0.81), NCCR-Mageuzi (asilimia 0.58), NLD (asilimia 0.03)
na TLP ilipata (asilimia 0.05).
Akizungumza katika mahojiano na Nipashe, Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi, anasema vyama visivyo na uwakilishi vimedumaa kwa sababu ya mazingira yasiyo sawa ya kisiasa.
Anasema vyama hivyo havina ruzuku, rasilimali watu wala fedha; jambo linalowafanya wazidi kudumaa kwa kuwa hawawezi kusimamisha wagombea kwenye ngazi mbalimbali wala kuweka mawakala wa kulinda kura.
Muabhi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Makatibu Wakuu wa Vyama Visivyo na Wabunge, anasema: “Wananchi nao hawaoni umuhimu wala ubora wa vyama hivi nab ado vyenyewe vina matatizo ya ndani.”
“Tulidhani serikali ya Awamu ya Tano ingetusaidia kujenga uwanja sawa kwenye siasa kwa pengine kutupa ruzuku, lakini hili naona linashindikana,” anasema.
Anasema vyama vingine havina ofisi akitolea mfano kuwa vingine ofisi ni ndogo isiyotosha kuingia watu wanne kwa wakati mmoja.
“Unakuta Mwenyekiti wa chama anaishi kwenye nyumba ya kupanga hata kodi inamshinda…sasa ataendeshaje chama ambacho nacho kinahitaji kupanga ofisi,” anasema.
Anasema vyama vya upinzani vimeshindwa kupenya na kupata wawakilishi wa ngazi mbalimbali kwa kuwa serikali ya CCM imeshindwa kujenga mazingira hayo ikiwamo kutoa ruzuku kwa vyama vyote.
KATAZO LA HARAKATI ZA KISIASA
Akizungumzia tangazo la Rais Magufuli kuzuia mikutano ya kisiasa hadi 2020, Muabhi ambaye aligombea ubunge mwaka 2015 katika jimbo la Ubungo, anasema huko ni kufunika moto kwa blanketi.
“Anataka kubana watu ili kunyamazisha fikra…hii ni sawa na kufunika moto kwa blanketi. Kwa ujumla ni kitu kisichowezekana,” anasema.
Anaongeza kuwa: “Ukiondoa Chadema na CUF, vyama vingine vinaonekana ni vya mfukoni. Sasa kwa kuzuia mikutano ambayo ni haki ya kisheria, vyama vitapataje wanachama wapya, vitafunguaje matawi na tutaandaaje wagombea wa ngazi mbalimbali?”
Anasema vyama vya upinzani na hususani visivyo na ruzuku havina uwezo wa kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari kila siku au kwa wiki, hivyo ni kwa njia ya mikutano vinaweza kuwafikia wananchi.
Anasema: “Vyama havina hela ya kulipia matangazo kwenye televisheni, radio au magazeti kila siku…anataka kunyamazisha watu. Naona hatari ya jambo hili siyo kwetu tu bali hata kwake kwa sababu hawezi kuona sana kasoro zilizopo kwenye serikali yake.”
UCHAGUZI WA MARUDIO Z’BAR
Pamoja na kwamba vyama vyenye ushawishi mkubwa na vinavyopata ruzuku vilisusia uchaguzi wa marudio Zanzibar, visivyo na wabunge vilishiriki kwa maelezo ya kuweka maslahi ya Taifa mbele.
Vyama hivyo viliunda umoja wa vyama vya siasa visivyokuwa na uwakilishi Bungeni, ambavyo ni CCK, DP, SAU, AFP, TLP, UPDP, NRA, UMD na Demokrasia Makini.
Katika hilo, Muabhi anasema bila vyama vidogo kuamua kujitosa kwenye uchaguzi wa marudio wa Machi 20, CCM isingeweza kufanikisha uchaguzi peke yake.
“Sisi tungesusa (vyama vidogo), CCM isingeweza kabisa kushiriki uchaguzi Zanzibar…tangazo la Rais Magufuli kwamba siasa ni hadi 2020 naliona ni hatari zaidi kwa CCM,” anasema.
“Kwa sababu, kwa mfano tu bila sisi wasingefanya uchaguzi kule Zanzibar.”
Muabhi anasema kitendo cha Rais John Magufuli kuzuia shughuli za kisiasa hadi 2020, siyo tu kina hatarisha uhai wa vyama vya upinzani, bali hata CCM yenyewe.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilifuta uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka 2015 kwa kile ilichoeleza ni kasoro mbalimbali; jambo ambalo lilisababisha vyama tisa kususa kushiriki uchaguzi wa marudio.
Kufutwa huko kuliibua msuguano kati ya waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa ambao walidai uchaguzi wa Oktoba ulikuwa huru na haki na serikali ya Zanzibar.
Januari 29, mwaka huu Marekani, Canada na Umoja wa Ulaya (EU) inayojumuisha nchi za Ubelgiji, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Uswisi na Uingereza zenye ubalozi nchini, zilitoa tamko la pamoja la kumtaka Rais Dk. John Magufuli, kuingilia katika mgogoro huo.
Tamko hilo pia lilieleza kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, ulikuwa na kasoro zilizoelezwa na kwamba waangalizi wa kutoka Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki, EU, Marekani na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), waliridhika na mwenendo wa uchaguzi huo.










