Rais Magufuli mpe Dk Dau tuzo ya heshima

01May 2016
J.M. Kibasso
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Rais Magufuli mpe Dk Dau tuzo ya heshima

RAIS John Magufuli, amezindua Daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambalo sasa linaitwa Daraja la Nyerere. Ni kivutio kikubwa ambacho siyo siri waliokamilisha kazi hiyo wanastahili kuenziwa.

Rais dk. john magufuli akiwa na Dk. Ramadhani Dau siku ya ufunguzi wa daraja la mwalimu nyerere kigamboni.

Nilikuwa miongoni mwa Wana-Dar waliojaliwa kuhudhuria uzinduzi huo hivyo napenda nieleze kwa uchache baadhi ya matukio niliyoyashuhudia na kuvutiwa.

Nianze na suala la kuenzi desturi na tamaduni zetu za utani miongoni mwa makabila mbalimbali hapa nchini. Nisema wakati akihutubia watu waliofurika kushuhudia sherehe hizo, Rais Magufuli, alionekana wazi kufuata nyayo za hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa akipenda kuchombeza maneno ya utani kwenye hotuba zake.

Kwa mfano, Rais alisema, leo hii, daraja hili limekamilika, halitabagua mtu kwa sababu ni wa CCM. Watapita hapa wa Chadema na kwa bahati nzuri Mstahiki Meya wa Jiji hili ambaye ni Chadema naye yuko hapa na amepita katika daraja hili.

Alichombeza neno la utani akasema; “Mstahiki Meya wa Jiji ni Chadema kiitikadi. Lakini ukimwangalia usoni vizuri, ni CCM wa dhati moyoni!!” hili liliwafurahisha watu walioangua kicheko.

Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi aliyependa mambo ya utani. Watani zake wakubwa walikuwa ni kabila la Wahaya. Nakumbuka mtani wake mmoja maarufu alikuwa akiitwa “Batengas” ambaye sasa ni marehemu.

Siku moja Batengas alitumia mwanya wa utani akaenda kiwandani akadai ametumwa vyerehani avipeleke nyumbani kwa Mwalimu Nyerere.Alipewa na kuahidi Mwalimu Nyerere angevilipia. Mara baada ya kuvichukua alimpelekea Mwalimu Nyerere cherehani kimoja kama rafiki yake.

Muda ulipozidi kwenda, Batengas alikamatwa. Hata hivyo alijitetea na kuwaambia kuwa ni mwongo, basi waongozane waende kwa Mwalimu ili wathibitishe ukweli kama Mwalimu hana cherehani moja inayofanana na vile vilivyo nyumbani kwake.

Walipofika nyumbani kwa Mwalimu wakaikuta cherehani kama zile, wakashindwa wafanye nini Mwalimu Nyerere akaelezwa yaliyojiri, “Kumbe mtani wake kamwingiza mjini”. Hakuwa na la kusema alibaki kucheka hatimaye akavilipia. “Utani una karaha na raha zake”

Pili jambo ambalo nilishuhudia ni ujasiri wa Rais Magufuli kukataa Daraja la hilo kuitwa kwa jina lake badala yake akaagiza jina la Daraja la Nyerere litumike ili kumuenzi Baba wa Taifa kwa mchango mkubwa wa maendeleo alioutoa kwa Tanzania.

Kimsingi kilichonihamasisha zaidi ni uamuzi wa Rais kumfagilia Dk. Ramadhani Dau, aliyejywa MKurugenzi Mkuu wa Shirika la Akiba ya Wafanyakazi (NSSF)

Alimtambulisha Dk. Dau kwenye hadhara hiyo ili asalimie wananchi, akisema naomba nimtambulishe mtu mmoja mwenye mchango mkubwa katika ujenzi wa daraja hili. Watanzania hawapendi kukumbuka historia, “Mnyonge Mnyongeni lakini haki yake mpeni. Dk. Dau na NSSF wamefanya kazi kubwa,” alisema Rais Magufuli.

Aliendelea kueleza kuwa Balozi Dau alimfuata ofisini kwake,wakati huo akiwa Waziria wa Ujenzi na kumuagiza
aanze kufanyakazi.

“Ni Dau na NSSF ndiyo waliosimama na kuhakikisha daraja hilo linajengwa na kukamilika kwa kiwango hicho. Haitakuwa busara kulizindua bila kutambua mchango wake. Ni kawaida kwa watu wenye michango mikubwa kusahaulika wakati wa mafanikio”.

Kauli ya Rais Magufuli ilinitoa machozi nikainama chini. Sikutarajia kusikia sifa hizi akimwagiwa Dk. Dau. Nasema sikutarajia kwasababu katika siku za karibuni, karibu vyombo vyote hapa nchini vimekuwa vikimtaja kama ni jipu linalosubiri kulipuliwa.

Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake , alisema mnyonge mnyongeeni lakini haki yake mpeni, kisha akamalizia kwa maneno ya kizalendo akasema kuwa ni kawaida kwa watu wenye michango mikubwa kusahaulika wakati wa mafanikio.

Hakika nimemkubali Rais Magufuli kwamba anatambua mchango wa kila mmoja. Mtu yeyote mwenye nia nzuri na nchi hii akipita kwenye daraja lile, sina shaka atamuunga Rais Magufuli mkono kwamba Dk. Dau anastahili kupewa tunzo ya kitaifa.

Inawezekana ni kweli kwamba Dk. Dau kama alivyo viongozi wengine, kuna miradi aliyosimamia wakati akiwa mkuu wa NSSF ikaingia dosari za uchakachuaji. Hata hivyo, ujenzi wa daraja la Nyerere linafuta madhambi yote aliyoyafanya. Wahenga walinena “Chema chajiuza kibaya chajitembeza”.

Naungana na Rais Magufuli kwamba “mnyonge mnyongeeni ila haki yake mpeni”. Mimi ni shuhuda wa lile daraja. Nilihamia kurasini mwaka 1992, pale pale ambapo daraja limepitishwa. Wakati huo ikijulikana kama Kurasini Rugwe.

Nilibahatika kuchaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Kurasini mwaka 1994, ikiwa ni uchaguzi wa kwanza baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini. Hatimaye mwaka 1999 nilichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Temeke baada ya Augustine Mrema (TLP) kuachia ngazi.

Siku ya uzinduzi nilipita eneo hilo kwa mara ya kwanza tangu tubomolewe nyumba zetu. Sikuamini niliyoyaona. Pale nilipojenga nyumba yangu sikupakumbuka tena. Nilidhani nimefika Ulaya.

Hakika Dk. Dau amefanya kazi kubwa na anastahili kupewa tuzo ya heshima. Rais Magufuli nakuunga mkono, huyu ni shujaa aliyeiletea Tanzania mafanikio.

Mawasiliano: 0714-399004 / 0767-399004,jmkibasso@gmail.com