Athari hizo zimeharibu maisha ya mamilioni ya watu na kuwaweka katika hatari zaidi ya kukabiliwa na njaa, kudhoofika kiafya na kusababisha migogoro kama vile ya wafugaji na wakulima wakigombea maji, ardhi ya kilimo au malisho ya wanyama wao.
Athari hizo pia hazijawaacha watoto ambao kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF), karibu kila mtoto duniani yuko hatarini kutokana na moja ya hatari zitokanazo mabadiliko ya hewa na mazingira kama mafuriko, joto, vimbuka, ukame na magonjwa ya kuambukizwa.Februari mwaka jana, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, anazindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 mjini Dodoma, inayosisitiza uhifadhi mazingira kwa kulenga kulinda vyanzo vya maji, misitu na upandaji miti.Katika uzinduzi huo upandaji wa miti unatajwa kuwa endelevu ili kuibadili nchi iwe ya kijani kwa kurejesha hali ya asili ya mazingira iliyoharibika kutokana na shughuli mbalimbali na mabadiliko ya hali ya hewa moja ya changamoto inayorudisha nyuma utunzaji wa mazingira na kutokuwapo na elimu ya kutosha kuhusu dhana ya mazingira ikiwamo athari za mabadiliko ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nayo.Kwa kuona umuhimu huo Taasisi ya Utu na Mazingira (HUDEFO), kupitia mradi ‘Child Art Café’ inatembelea klabu za mazingira kwenye shule za msingi na kufundisha wanafunzi namna ya kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kupitia sanaa ya uigizaji na uchoraji.Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Sarah Pima, anasema elimu hiyo wanaitoa kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba, ambapo huwafundisha somo moja kisha huwaongoza wachore au kulingana na walivyoelewa.Anasema wanatumia sanaa hizo kwa sababu wanaamini kuwa mtoto anaelewa kwa njia ya vitendo hivyo somo hilo litakaa kwenye akili zao kwa muda mrefu.“Somo la mazingira lina vitu vingi na vyenye mrengo wa kisayansi, kwa hiyo unapolipeleka kwa watoto unahitaji kutumia njia yenye burudani ili waelewe zaidi, ndio maana tunatumia sanaa ya uchoraji na maigizo au wakati mwingine nyimbo,” anasema Sarah.Mkurugenzi huyo anasema lengo la programu hiyo ni kuandaa vijana watakaoendeleza mapambano dhidi ya athari ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa njia ya upandaji na utunzaji wa miti pia kuwapa fursa ya kutoa mchango wao juu ya namna kukabiliana na janga hilo.“Samaki mkunje angali mbichi, ukiangalia vijana wa sasa wengi hawana mwamko wa kutunza mazingira kwa sababu hawakufundisha tangu wakiwa wadogo, programu hii inalenga kurekebisha makosa hayo, tunaandaa askari wa mazingira wa hapo baadaye waje waendeleze pale tutakapoishia,” anasema Sarah.Mratibu wa Mradi wa HUDEFO, Zainabu Mzirai, anasema mafunzo hayo pia yanaambatana na mashindano ya sanaa ya mazingira yatayokutanisha shule zote wanazozitembelea na mwishoni wa mwaka watamtangaza mshindi na kumpa zawadi.Anasema mradi huo unashirikisha shule zote za serikali na binafsi na mpaka sasa wamezifikia shule sita na wanafunzi 30 kati ya shule 20 na wanafunzi 600 waliopanga kuwafikia mpaka mwishoni mwa mwaka huu.“Mwishoni mwa mwaka huu tunatarajia kufanya maonyesho ya sanaa za mazingira kwa kuwashirikisha watoto na wazazi jijini Dar es Salaam, ambapo kazi ya wanafunzi hawa zitaonyeshwa na kushindanishwa mshindi atakabidhiwa zawadi, lengo ni kukuza hamasa kwa watoto kupenda utunzaji wa mazingira,” anafafanua Zainab.Anaongeza kuwa lengo la kuzifikia shule zote za msingi nchini, ikiwamo kuanzisha klabu za mazingira kwenye shule ambazo hazina ili kila mtoto apate nafasi ya kushirikiana katika kuboresha ustawi wa mazingira yake ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.James Bitisigirwe ni Mkuu wa Shule ya Msingi ya Kibangu inayonufaika na mradi huo, anasema kuwa wanaona fahari kufikiwa na shirika hilo kwa kuwa wanawaongezea ujuzi kwa namna ambayo wao hawawezi kufanya kutokana na uelewa wao.“Mashirika kama HUDEFO anapokuja kufundisha watoto masuala ya mazingira tunajisikia furaha kwa sababu tunaamini watoto wenu watapata elimu zaidi, watu hawa wamebobea katika mazingira wanafahamu vitu vingi kuliko sisi,” anafafanua James.Anasema tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo wamepata mafanikio makubwa ikiwamo wanafunzi kubadili mitazamo yao kuhusu mazingira na kuyachukulia kama ni kitu kinachohitaji kutunzwa na kuthaminiwa kwa manufaa ya baadaye.“Mtoto aliye katika klabu ya mazingira akiona mti umenyauka unamuona anaonyesha kujali, atakufuata na kukwambia mwalimu ule mti unahitaji mbolea na maji maana unaelekea kufa, tofauti na mtoto ambaye hayupo kwenye klabu hiyo,” anasema.Alisema ukiacha klabu ya mazingira shule hiyo ina klabu nyingine nyingi ikiwamo haki za binadamu, kupika, kuchora na hisabati lengo ni kuwapa watoto nafasi ya kukutana nje ya darasa kujifunza na kujadili mambo mbalimbali ya kijamii yanayotendeka nje ya masomo ya darasani.James anasema kuna faida kubwa za elimu ya ikolojia shuleni ikiwamo wanafunzi kujifunza kwa ushirikiano, kufikiri kwa makini na kufanya majadiliano na wengine.Anasema pia wanafunzi hushiriki katika shughuli za kikundi ambazo huongeza uvumilivu na kuelewa uwezo wa kila mwanafunzi, ambazo ni sifa muhimu za uongozi.Anasema klabu hizo pia zinasaidia kukuza vipaji vya watoto na kuwatambulisha kwenye shughuli za kijamii ili wanapokuwa wakubwa wajiendeleze na kufanya shughuli hizo.“Kupitia klabu hizi wanafunzi huja na mikakati ya utekelezaji inayohusiana na matumizi ya ulimwengu halisi, hivyo kuboresha ujuzi wa kijamii na mazungumzo,” anasema.










