Ndiyo ujumbe wa wakulima,  wazalishaji mbegu kwa SMZ

27Jul 2023
Zuwena Shame
Aliyekuwa Zanzibar
Nipashe
Ndiyo ujumbe wa wakulima,  wazalishaji mbegu kwa SMZ
  • *Washangaa mchakato wa sheria  unachelewa, wataka ulinzi Vs GMO

MBEGU ndiyo mwanzo wa uhai, ni muhimu kwenye kuzalisha chakula, ndiko iliko lishe na maendeleo ya kilimo yanayowapa maisha wengi mijini na vijijini ni chache kati ya sifa nyingi za mbegu.

Bila kuwa na sheria za kulinda na kutunza mazingira ya asili ni vigumu kuwa na mbegu bora zenye ladha na vionjo watu walivyovizoea kwenye matunda, mboga, ndizi, miwa na mahindi. 

Ikumbukwe kuwa wakulima ndiyo walinzi wa kwanza wa mbegu, wanazihifadhi na kuzitunza  hasa za asili bila malipo, kwa karne nyingi. 

Ndiyo maana wakulima na wadau wa kilimo Zanzibar wanaiomba serikali yao kuharakisha mchakato wa sheria ya mbegu ili waweze kuzilinda na kutunza mazingira.

Ni ombi linalotolewa wakati wa mkutano wa wakulima wadogo kutoka Bara na Zanzibar, wazalishaji wadogo wa mbegu na asasi za kirai zinazohudumia wakulima.

Wanaamini sheria ni ulinzi wa haki zao kwenye ugunduzi, kutumia, kubadilishana na kuendeleza mbegu za asili.

Mkutano huo unaoandaliwa kwa ushirikiano wa Taasisi za Mtandao wa Vikundi Vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), African Centre for Biodiverity (ACB) na Umoja wa Walima Mboga na Matunda Zanzibar (UWAMWIMA), unahimiza ujio wa sheria hiyo.

Wanasema rasimu ya sheria ya mbegu visiwani haijafika hadharani hivyo kufanya wakulima wadogo kuwa na hofu wa haki zao za msingi katika kulinda na kuziendeleza mbegu zao pamoja na ugunduzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA, Stephen Ruvuga, anasema wakulima wadogo visiwani humo wana hofu ya kupoteza mfumo wao wa kilimo uliopo unaowapa uhuru wa kubadilishana, kuuziana na kupeana mbegu za asili bila mipaka.

Anawaambia washiriki, kuharakisha mchakato wa sheria hiyo ni muhimu kwani Zanzibar ina wakulima wengi wadogo ambao sheria hiyo inawalenga, pia kukamilika kwake kutawawezesha kujua haki zao za msingi ikiwamo kuzihifadhi na kuziendeleza.

Aidha, wakulima wanaitaka SMZ kuiga sheria nzuri za mbegu za mataifa mbalimbali ya Afrika kama Uganda na Ethopia na pia Venezuela huko Amerika Kusini.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI) na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) zinawagusa wakulima, wakizisifia kuwa zimetoa kipaumbele katika kilimo ikolojia na kutambua mbegu za asili zilizopo visiwani humo kwa kuzitafiti. 

Ruvuga anaeleza kuwa dhana kuu ya sheria ya mbegu ni kuongoza, kusimamia na kudhibiti biashara yake, hivyo mfumo mbadala ambao sio wa kibishara unatakiwa ili kuzilinda hasa zile za asili ili zisopotee na kwamba ule utamadauni wa kubadilishana mbegu unaheshimiwa, unathaminiwa na kulindwa na ikiwezekana pia miongozo iliyopo itambue.

Mkurugenzi wa Umoja wa Wakulima wa Mboga na Matunda Zanzibar- UWAMWIMA, Khamis Juma, anawataka wajumbe kutumia mkutano huo kujifunza kutoka pande zote mbili za Muungano masuala ya sheria na sera.

Juma anasema: “UWAMWIMA husaidia wakulima kimapato kwa kuuza mazao na mbegu ila sheria na sera zinazomgusa mkulima moja kwa moja zinambana.”

“Baadhi ya mbegu zinaingizwa visiwani humo kwa sheria na mamlaka na kusimamiwa pia hivyo kutawala na kuzifunika zile za asili, hata hivyo nyingi hazina ubora zikilinganishwa na mbegu za asili zenye ladha halisi.”

Mwanaharakati wa  kilimo hai – Zanzibar, Mwatima Juma, anasema mbegu ni suala pana hivyo kuweka sheria ngumu kunaweza kuwaathiri wakulima hasa wadogo kwani mbegu ni biashara, akionya kuwa wakulima wengi visiwani humo hawajafikia kuwa na upeo wa kuzalisha kibiashara.

Anatoa mfano kuwa si vyema sheria hiyo itakayotungwa kuwa na ajenda za nje mfano mbegu za mkulima lazima ziwe na lebo na kuthibitishwa ili iwe ya kibiashara kwani wakulima wengi wadogo wamezoea kupeana na kubadilishana mbegu wenyewe kwa wenyewe.

“Sheria ya mbegu isiwe kwa wote (uniform) na kuwabana wakulima wadogo. Ilenge zaidi katika makampuni yanayotuletea kutoka nje tena ambazo si bora na hazijakubaliwa na taifa kama zilizobadilishwa nasaba za GMO.” anasema Mwatima.

 Asia Thani, kutoka Wizara Ya Kilimo Zanzibar anaelezea suala la kuchelewa kwa sheria hiyo kuwa kunafanya wafanyabiashara wengi kuingiza kila aina ya mbegu visiwani humo na kufanya kama dampo la kuzitupia.

 “Kila mtu anaingiza mbegu zake ambazo hazina sifa wala ubora kwani baadhi hazioti na zimechanganyika na hakuna sheria wala chombo cha kuwashtaki, shida zote hizi zitaondoka kwa sababu kutakuwa na mamlaka ya kusimamia sheria za mbegu,” anasema Asia.

Ofisa Tafiti na Utetezi kutoka Shirika la African Centre for Biodiverity (ACB), Sabrina Masinjila, anaueleza mkutano kuwa sheria ya mbegu visiwani humo ni lazima kuangalia baadhi ya mikataba ya kimataifa mfano International Union for the Protection of New Varities of Plants (UPOV).

Mkataba huo moja ya sheria zake hazimruhusu mkulima au mtu kutumia mbegu kijamii kitu ambacho wakulima wengi wameshazoea kwa kubadilishana na kupeana bila mipaka.

Anaeleza kuwa UPOV isiwe ni kipimo cha kuendeleza kilimo kwa nchi kama Tanzania kwani kiuhalisia Zanzibar, Tanzania Bara na nchi nyingine nyingi bado hazijafikia malengo wala mahitaji hayo.

Anasema rasimu hiyo inapaswa kukwepa mapungufu ya wazi ikiwamo kutohusisha baadhi ya vifungu katika sheria ya mbegu ya Tanzania Bara ya mwaka 2003 ambavyo vimeshindwa kutoa ulinzi kwa wakulima wadogo ili wawe wanauziana na kubadilishana mbegu zao kwa uhuru.

Mkuu wa Program kutoka MVIWATA, Theodora Pius,  anasema ni wakati muafaka kuwatambua wazalishaji mbegu zinazotumika katika kuzalisha chakula.

Theodora anasema kuwa MVIWATA hasa mkoa wa Dodoma wameweza kuendesha programu kubwa kwa wakulima wa mbegu ili waweze kuzalisha mbegu za asili katika vikundi, lakini baadhi ya wazalishaji wakubwa wamekuwa wakiwalaghai kwa kununua mbegu na kuziwekea vibandiko vyao ili zionekane kuwa wao ndiyo wazalishaji.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Seif Mwinyi anawaambia washiriki kuwa serikali  imechukua mapendekezo yaliotolewa na wadau hao hasa ikiwamo mfano wa sheria ya mbegu ya nchi za nje ambazo hutambua haki za mkulima na kuthamini mbegu za asili. 

“Rasimu ya sheria imejikita sana katika kuongeza uzalishaji, ajira kwa vijana na akina mama na masoko na kutanua wigo wa bidhaa zetu. Tumeona kwamba ili kuwe na uzalishaji mbegu ndiyo msingi mkubwa,” anasema Mwinyi.