Ndivyo nyuki alivyo mali kila kitu chake ni cha bei, thamani kubwa

02Aug 2023
Christina Mwakangale
MBEYA
Nipashe
Ndivyo nyuki alivyo mali kila kitu chake ni cha bei, thamani kubwa
  • *Anayo tiba ya uzee, anaumaliza ugumba sumu yake ghali hukaribia nusu milioni

MWAMBOGELA Gabriel, ni mwanasayansi, msomi anayetoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye amejikita katika kuyaendeleza mazao ya nyuki, kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali  na kuziingiza sokoni, ikiwamo asali, chavua, sumu, maziwa, jeli na mafuta.

Unaweza kujiuliza sumu ya nyuki ikoje? Gabriel anajibu kuwa ni iliyosababisha upate maumivu makali. Kuvimba na wakati smwingine hata kifo.

Anajiita mwanasayansi wa nyuki na teknolojia yake, lakini ni mwatamizi na mhitimu wa Shahada ya Sayansi na Teknolojia ya Ufugaji Nyuki.

 

Anazungumza na Nipashe kwenye Banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakati wa Maonesho ya Sabasaba, akibainisha namna alivyojiajiri huku akizalisha bidhaa nyingi zinazomwingizia kipato.

 

"Ni mwanasayansi wa nyuki na teknolojia yake imebuni utaalamu wa kuvuna mazao yake. Kwanza inavyofahamika tunapozungumzia nyuki watu wengi wanawafahamu katika kutengeneza asali pekee lakini kuna zaidi ya hilo ni zao moja.”

"Kitaalamu nyuki anatengeneza mazao sita, tunazungumzia wanaofugwa kwa sababu kwenye taaluma hii tuna aina 20,000 za wadudu hao, lakini katika aina hizo tunapata tatu  ambazo mara nyingi wanafugwa,” anabainisha msomi huyo.

Anasema katika ukanda wa Afrika, hususan Tanzania kuna aina kuu mbili za nyuki wanaofugwa, ambazo ni wanaodunga wakijulikana kisayansi kama nyuki wakubwa na aina ya pili ni wale ambao hawadungi wasio na mwiba, hao huitwa nyuki wadogo.

Tukumbuke kuwa kiumbe kinachouma kina meno lakini nyuki hawana meno badala yake wana mwiba hivyo hudunga na kuacha ‘kisindano’ hicho kwa aliyeumizwa.

"Kitanzania tumewatenga kama nyuki wadogo na wakubwa, lakini kuna aina nyingine ya nyuki ambao wanapatikana ukanda wa Mediterranean wapo pia mataifa ya Afrika Kaskazini hawa wanasifika kwa kuzalisha chavua nyingi," anaeleza.

Gabriel anasema ameamua kufuga akisaka faida, ikiwamo kupata asali, gundi, mafuta, lishe na tiba ambayo humuongezea binadamu kinga na homoni na kuimarisha uzazi akiongeza:

"Tunafuga nyuki kwa ajili ya kupata mazao yake kama asali na pia nta tukija kwa huyo  anayedunga, au nyuki mkubwa anazalisha chavua, nta, asali, sumu ya nyuki ambayo mtu akidungwa anavimba hii ni bidhaa. Pia  anatupatia  maziwa ya nyuki na gundi ya vyote vina thamani na huhitajika sokoni.”

Akizungumzia maziwa anasema nyuki wana tezi maalumu la kuzalisha maziwa ambayo ni chakula cha malkia na nyuki wachanga.

Anakumbusha kuwa malkia hula maziwa maisha yake yote na kwamba wanamtengenezea chakula hicho mahususi na wafugaji wanapotaka kuyazalisha wanatengeneza seli za maliki ambazo zitawavuta kuongeza uzalishaji, kazi inayofanywa kitaalamu.

Gabriel anaongeza kuwa maziwa yake yanachanganywa kwenye asali na yana virutubisho vinavyozuia kuzeeka, huongeza kinga ya mwili na anayaelezea kuwa ni mazito yako kama ‘cream’.

 

"Mazao ambayo nyuki anazalisha yote yana faida kubwa katika lishe, lakini kwenye tiba tukianza katika lishe kuna mazao kama asali, watu wengi wanatumia kama chakula ukiila unapata faida za kilishe, lakini faida za kiafya," Gabriel anaeleza.

 

Anatolea mfano kwa asali inayozalishwa na nyuki wadogo, ikitumiwa humwongezea mtumiaji virutubisho kwa kuwa wana sifa ya kipekee wakati wa kutengeneza asali hiyo na kuongeza:

"Asali ya nyuki wadogo, inasifika sana kitiba kutokana na aina ya virutubisho au vitu ambavyo vimesheheni. Wanaoitengeneza ni wale wasiodunga ambao kiumbo ni wadogo ndiyo maana wanapewa jina la nyuki wadogo.”

Anawasifia kuwa wana uwezo wa kupenya katika maua ambayo ni madogo sana yanayowashinda wakubwa hawawezi kupita, hivyo wanakuwa na wigo mpana wa kutembelea mimea na maua tofauti tofauti na kukusanya maji maji ua malighafi zinazokuwa na faida kubwa  kitiba. Asali hii ina kiwango kikubwa cha 'biotic compound' ambazo zinasaidia katika mfumo wa chakula lakini imesheheni  utajiri."

Anafafanua kuwa  ‘biotic compounds’ ni vitu vilivyo hai katika mimea na viumbe hai ambavyo vina sifa ya kutibu  na kusema  asali ya nyuki wadogo inasaidia umeng'enyaji wa chakula na sukari  inayopatikana ndani yake  ina utajiri wa sukari ambayo haipatikani sana katika nyuki wakubwa na kwamba  husaidia kudhibiti ongezeko la kiwango kikubwa cha sukari kwenye mwili wa binadamu.

Kadhalika, Gabriel anasema, kwa watu wenye kisukari wanashauriwa kutumia asali ya nyuki wadogo, kwa sababu aina zake za sukari hazisababishi kuongeza kiwango cha sukari kwenye damu.

"Asali ya nyuki wadogo pia ina sifa nyingine, ambayo ni uwezo wa kupambana na vijidudu vidogo kama virusi, bakteria na fangasi mwilini, pia ina uwezo mkubwa sana ukilinganisha na asali ya nyuki wakubwa," anafafanua mwanasayansi huyo na kueleza kuwa mbali na faida hizo nyingine ni nyuki kwa ujumla huzalisha chavua na kuchavusha mimea hivyo kuwa muhimu kwenye michakato ya kilimo.

 

Anasema maua  yanakuwa na mbegu za kiume, ambazo  nyuki anazichukua na kuzichanganya na  mwishowe inapatikana chavua ambayo sifa yake kubwa katika mwili wa binadamu kama ataitumia wanasayansi wanasema  imeonyesha kuwa ikatumika ina uwezo kuongeza, kiwango cha mbegu za kiume.

 

Gabriel anasema ushauri ni kutumia bidhaa za nyuki mfululizo na kuwa ni utaratibu wa mlo wa kila siku au kutumia kama vile mafuta ya kupaka au jeli ili kupata matokeo chanya akiwashauri unapokuwa unatumia bidhaa za nyuki usitumie mara moja na kuacha, ili uone matokeo unatakiwa kutumia kama chakula tunasema utumie hizi bidhaa kama chakula usizitumie tu kama dawa siyo kwa muda mfupi.

 

"Inatakiwa utumie mara kwa mara na chavua inapatikana katika maua ya kiume na maua ya kike ili mmea uweze kuzaliana inabidi zile mbegu za kiume kutoka kwa mmea wa kiume ziende kwenye ua la kike moja kati ya kazi ya nyuki ni kufanikisha uchavushaji au 'pollination'.

 

"Nyuki anavyokwenda kuhamisha zile mbegu za kiume kwenda ua la kike anahamisha na zingine kutumia kama chakula chake hizi zikiwa kwenye mmea zinaitwa 'pollen flower' lakini akishazichukua akachanganya na vitu vingine kutoka kwake tunaziita chavua.”

Anasema pia chavua husaidia na kuimarisha afya ya ubongo kwa watu wenye matatizo ya kupoteza kumbukumbu na kwamba vifaa vya kuvunia mazao ya nyuki, amevibuni pia na vinamwezesha kuvuna sumu ya nyuki ambayo huuzwa kwa bei kubwa kwenye soko la dunia na vilevile bidhaa zinazovunwa hutunzwa kitaalamu, ili zisiharibike.

 

Anasema gramu moja ya jeli itokanayo na maziwa ya nyuki, huuzwa kati ya Sh. 30,000 hadi 50,000 na kwamba matumizi ya bidhaa hiyo ni katika kusaidia kupunguza kasi ya kuzeeka, ikiwamo mikunjo wa ngozi.

 

"Kwa ujumla nyuki wa kufugwa bidhaa zake zote zina thamani na ni faida kwa binadamu, kwa sababu asali inasaidia kuponya vidonda vya nje na ndani ya utumbo, yaani vidonda vya tumbo. Pia anachavusha mimea mashambani, na mengi mengine,” anasema Gabriel na kwamba bidhaa zao zinapatikana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.