Moyo ameamua kutafuta mustakabali wa mgogoro huo huku wananchi wa Zanzibar wakiwa katika matayarisho ya kushiriki uchaguzi wa marudio uliopagwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.
Mazungumzo ya awali yalianza kufanyika Zanzibar Novemba mwaka jana chini ya Rais wa Zanzibar DK. Ali Mohamed Shein, lakini yakavunjika baada ya Makamu wa kwanza wa rais, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza kujitoa kwa madai yalikosa tija.
Hamad katika mazungumzi hayo aliwasilisha vielelezo vya madai yake kuwa alishinda katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.
Hata hivyo, kabla ya Makamu wa Pili wa rais, Balozi Seif Ali Idd hajawasilisha vielelezo vyake vilivyoonyesha namna uchaguzi ulivyoharibika, Seif alijitoa katika mazungumzo hayo.
Wajumbe wengine katika mazungumzo hayo walikuwa marais wastaafu wa Zanzibar ambao ni Dk. Salmin Amour Juma, pamoja na Dk. Amani Abeid Karume, lakini walishindwa kupata muafaka katika mazungumzo hayo.
Wakati Hamad akitetea uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana ukamilishwe na matokeo yatangazwe pamoja na mshindi wa urais viongozi wa CCM waliungana na msimamo wa tume wa kurudiwa uchaguzi huo.
Moyo amesema mjini Zanzibar kuwa ameamua kufufua mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mgogoro wa Uchaguzi wa Zanzibar.
Anasema kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Zanzibar kabla ya kupatikana kwa maridhiano siyo ufumbuzi wa kumaliza mgogoro wenyewe wa uchaguzi Zanzibar.
Waziri huyo wa zamani wa Katiba na Sheria baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, anasema kunahitajika mazungumzo ya haraka ya kutafuta muafaka wa mgogoro wa uchaguzi mkuu kutokana na makundi mawili ya wananchi kugawanyika Zanzibar tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Oktoba 28 mwaka jana.
Moyo anasema siasa za chuki na uhasama zimeanza kufufuka Zanzibar na kusababisha kutetereka kwa misingi ya kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).
Mwanasiasa huyo pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya maridhiano ya mwakia 2009, ambayo yalifanikiwa kumaliza mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar na kuzaliwa kwa SUK na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad kuwa makamu wa kwanza wa rais.
Anasema ameamua kukutana na wazee maalum Tanzania Bara na Zanzibar ili kujenga mtandao wa kuanzisha mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi kabla ya kufanyika marudio yake Machi 20 mwaka huu.
Hata hivyo, anasema kazi hiyo inafanyika kwa uangalifu mkubwa na umakini kutokana na kuwapo wahafidhina Zanzibar ambao hawataki kuwepo maelewano Zanzibar.
Moyo anaeleza kuwa ni jambo la aibu kuona Tanzania ikiwa na sifa kubwa ya kushughulikia migogoro ya kisiasa barani Afrika na ukanda wa maziwa makuu kuona ikishindwa kutatua mgogoro wake wa ndani kabla ya kutokea madhara kwa wananchi wake.
Anasema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli haikuwa muafaka kuamua kujiweka kando kwa kusema hawezi kuingilia mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar wakati yeye ndiye mkuu wa nchi.
Anasema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa uwezo wa kuingilia mambo ya ndani ya Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa usalama wa Zanzibar na wananchi wake.
“Tanzania tuna wazee wenye hekima na busara wenye uwezo wa kumaliza mgogoro wa uchaguzi kwa wakati kabla ya kuleta madhara muhimu, viongozi wafungue mlango wa mazungumzo kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake,”anasema Moyo.
Anawataka wazee wenye uwezo wa kumaliza mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar ,Waziri Mkuu mstaafu Joseph Sinde
Warioba, Waziri Mkuu mstaafu Salim Ahmed Salim, Katibu wa Rais mstaafu Jeseph Butiku, Rais mstaafu Benjamini Mkapa pamoja na kada wa CCM Mzee Ndejembi wafanye mkakati wa kumaliza mgogoro.
Ansema kuwa wazee hao kama wataungana na wenzao kutoka Zanzibar akiwamo Rais Dk. Shein makamu wake Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na wazee wengine muafaka wa uchaguzi utapatikana Zanzibar.
Anasema kamati ya maridhiano chini ya uongozi wake ilifanikiwa kumaliza mpasuko wa kisiasa kwa sababu wajumbe wote walikuwa na nia moja ya kuwaunganisha Wazanzibari chini ya Rais mstaafu Amani Abeid Karume.
"Viongozi waliopo madarakani wakubali kufungua mlango wa mazungumzo kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake, kurudia uchaguzi kabla ya maridhiano siyo ufumbuzi,”anaonya Moyo.
Ansema bila ya kupatikana ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi, SUK ipo katika hatari ya kufa Zanzibar na kama hilo likitokea makovu ya uhasama uliokuwapo siku za nyuma yatarudi.
Anakumbusha kuwa SUK ipo kwa mujibu wa marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar mwaka 2010 na haiwezi kuundwa bila ya wapinzani kuwa na viti vya majimbo ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW).
Anasema kwa mujibu wa mashariti ya Katiba ya Zanzibar, CCM haiwezi kuunda serikali peke yake kama vyama vidogo vidogo vitashindwa kupata viti baada ya Chama cha Wananchi (Cuf) kuamua kususia uchaguzi wa marudio wa Machi 20 mwaka huu.
Moyo ambaye alifukuzwa uanachama CCM kutokana na msimamo wake wa kukosoa siasa za Muungano, anasema mgogoro mkubwa wa kikatiba utaibuka kama vyama vingine vitashindwa kupata viti na kukamilisha mashariti ya kuingia katika kuunda SUK.
Anasema kifungu cha 39 (i) cha Katiba ya Zanzibar kinaeleza iwapo chama kilichoshika nafasi ya Pili katika matokeo ya uchaguzi wa rais na kupata asilimia 10 ya kura zote za uchaguzi wa rais kitatoa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Lakini anasema kama chama hicho kitapata chini ya asilimia kumi ya matokeo ya urais basi makamu wa kwanza wa Rais atapewa chama chochote cha upinzani kilichotokea cha pili kwa wingi wa viti vya Majimbo katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar(BLW).
Bahati mbaya anasema vyama vilivyobakia havina historia ya kupata hata asilimia moja ya kura, kiti cha diwani au jimbo moja zaidi ya CCM na CUF.
Moyo anasema kama CCM itashindwa kuunda SUK baada ya uchaguzi wa marudio hatua hiyo itazua mgogoro mwingine mkubwa wa kikatiba na kutaka juhudi za mazungumzo kufanyika kwa maslahi ya Zanzibar.
Anasema siasa za chuki na uhasama zinazojitokeza Zanzibar zinahitaji kuangaliwa kwa umakini kabla ya kubomoa msingi wa kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010.










