Katikati ya ukweli huu tunafahamu pia kuwa hata binadamu wenyewe tunatofautiana mno kati yetu, kama tunavyofanana kwa vitu vingi pia.
Moja ya mambo yanayotutpfautisha kati yetu ni namna ambavyo binadamu mmoja anaweza kufikiri, kubuni na kutengeneza vitu ambavyo wenzake hawakuwahi kuviwazia au kudiriki kuvitengeneza.
Mara nyingi tunatumia maneno kama ubunifu, kipaji na kadhalika kumtambulisha Yule ambaye amethubutu kufanya jambo ambalo kama lisingefanyika pengine lingeonekana ni kama ndoto.
Baadhi ya mifano halisi ya kazi za ubunifu wa binadamu unajidhihirisha katika vyombo vya kisayansi kama magari, ndege, meli, treni, kompyuta, simu za mezani na za viganjani, televisheni (luninga) na friji (majokofu).
Mifano mingine ni mashine za kutolea fedha (ATMs), programu za kompyuta na tovuti za kijamii kama facebook, whatsapp, instagram, na kadhalika. Angalia pia ubunifu wa madawa kama Asprin, Panadol na Viagra, viatu, nguo, viberiti, taa za umeme, tungo na santuri za muziki na kadhalika.
Mara moja utagundua pia kuwa yote hayo yalitokana na uwekezaji uliofanywa na mtu, kikundi cha watu, kampuni na hata nchi katika kukifanya hicho kilichofanyika. Uwekezaji huu huhusisha muda mrefu wa kutafakari, kupanga na kufanya jambo hilo, na pia matumizi ya jitihada za kimwili na fedha.
Kwa hivyo basi, utaona kuwa ni lazima kungehitajika sera na sheria za kuwalinda wale wanaotumia muda, akili, nguvu na fedha zao nyingi kuvumbua au kutengeneza vitu ambavyo vinazidi kuyarahisisha maisha yetu. Hiki ndicho tunachokizungumza hapa kwa sasa, yaani ni sheria zipi zinamlinda mtu wa aina hii.
Ndugu wasomaji, sheria zinazolinda kazi za ubunifu wa akili (kimombo intellectual property laws) zinaangukia katika makundi takribani matatu hivi, kama si manne, japo tumezoea kuziita kwa ujumla kwa jina la sheria za Hakimiliki.
Tanzania tuna sheria mahsusi za jambo hili na taasisi ama mamlaka kama COSOTA na BRELA zinahusika kwa karibu.
Mosi, sheria zinazolinda uvumbuzi wa kazi za kisayansi kama mashine, program za kompyuta, fomula za madawa ama vinywaji na kadhalika. Hizi zinajulikana kimombo kama Patent Law na bahati mbaya sijapata neno mbadala la Kiswahili.
Basi kama unatengeneza aina moja ya kitasa cha mlango, unavumbua dawa ya kutibu malaria, au kinywaji chenye ladha mpya, basi eneo hili linakuhusu.
Kundi la pili katika sheria zinzaolinda kazi za ubunifu ni lile linaloitwa copyright laws kwa kimombo na linalinda kazi kama za utunzi wa vitabu na riwaya, tungo za muziki ama filamu. Zungumza na wataalam walioko COSOTA ama wanasheria waliobobea katika kazi hizi, watakupa mwanga mpana zaidi.
Kundi jingine ni lile linalolinda ubunifu wa majina, nembo na alama za biashara. Yaweza pia kuwa ‘logo’ ama kauli mbiu. Mathalani, kauli mbiu za kibiashara ama kisiasa (motto) kama ‘IPP Cares for You’ ya makampuni ya IPP ama ‘Hapa Kazi Tu’ ya John Pombe Magufuli zimewahi kuvuma sana hapa nchini na zinamtambulisha kirahisi anayehusika katika jitihada zake za kujitofautisha na wengine. Ndiyo kusemaa zaweza pia kusajiliwa ili mtu ama taasisi mwingine asiitumie.
Tuseme tu kuwa pia kwamba, hakuna sheria inayokulazimisha mfanyabiashara usajili alama fulani ya biashara, mathalani nembo na kadhalika.
Na kwa vile sheria hukua na kubadilika kila siku, yawezekana kabisa yapo maeneo ambayo mfanyabiashara ama mtoa huduma akashurutishwa kufanya hivyo, lakini iwapo hili lipo basi ni katika maeneo machache sana na hilo litakuwa eneo lenye tofauti ndogo sana kutoka kanuni ya jumla na iliyozoeleka na wengi (Exception to the General rule) kwamba kusajili mambo hayo ni suala la hiari lisilohitaji shuruti. Labda tufafanue kidogo hapa.
Kabla ya mfanyabiashara kujikita katika uuzaji wa bidhaa (vocha za simu, magazeti, chakula, duka, uuzaji magari, n.k) ama biashara ya kutoa huduma (mathalani usafirishaji wa abiria, utabibu, ufundishaji wanafunzi, ama utoaji ushauri kwa fedha), basi yumkini ni lazima kwanza usajiliwe na mamlaka husika za Serikali (yaweza Kuwa Serikali kuu, Serikali za Mitaa, ama kupitia kote huko).
Mathalani, iwapo unataka kujihusisha na uchimbani na uuzaji wa madini itabidi kwanza usajiliwe na poia kupata hati safi kutoka mamlaka husika kama BRELA, Kamishna wa Madini, Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), mamlaka ya Mapato (TRA), Leseni ya biashara katika Halmashauri husika ama pia moja kwa moja kutoka Viwanda na Biashara, na kadhalika.
Tuchukulie sasa umeshakidhi matakwa yote hayo na ukaanza biashara, zipo changamoto kadhaa ambazo mara moja hujitokeza na ambazo zitakulazimu uwe na hekima ya kuisajili (kama ni moja) ama kuzisajili (kama ni zaidi ya moja) nembo ama alama fulani fulani ambazo zitakusaidia kuitambulisha biashara yako mahali biashara ilipo, kote Tanzania na hata katika soko la ulimwengu. Basi mada hii ndiyo inahusika hapa.
Labda waweza kujiuliza: Kuna faida ama hasara zipi za kusajili ama kuchelea kusajili nembo ama alama za biashara katika biashara ninayoimiliki ama niliyopewa jukumu la kuhakikisha inanawiri (hapa yawezekana ni kijana ama binti ambaye kaaminiwa na mzazi wake kusimamia raslimali za familia)?
Faida zipo nyingi na hasara hivyo hivyo. Hatutazizungumzia hasara hapa kwa sababu iwapo tunazitaja faida, basi hasara ujue ni kile kinyume cha kukosekana kutumika kwa fursa ziwezazo kuleta faida zilizoainishwa.
Faida kuu ya kusajili alama ya biashara ni kuitambulisha kwa haraka na uhakika zaidi biashara yako.
Wataalam wa masuala haya (Branding Experts) wanatueleza kuwa bidhaa au huduma inayofanikiwa na kuleta faida kubwa ni ile iliyo bora kuliko nyingine, inayotolewa kwa kuwajali wateja, na zaidi ni ile ambayo ina vitambulishi mahsusi vinavyoifanya isimame peke yake sokoni na rahisi kukumbukwa na mteja wa nyuma na pia yenye uwezo wa kumshawishi mteja mpya kuisogelea pale ilipo.
Alama za biashara kama nembo za kibiashara (logos) na hata jina lenyewe hucheza nafasi kubwa katika kuifanya biashara fulani isisahaulike haraka miongoni mwa wana-jamii walioizunguka.
Baadhi ya mifano ya makampuni ambayo nembo zao za biashara zinafahamika sana ni kama Coca-Cola (soda); Pepsi Cola (Soda), Toyota (magari); Mercedes Benz (magari), Oxford na Longman (Uchapishaji/Vitabu), Boeing (ndege), CNN (Televisheni), ITV (televisheni), Nike na Adidas (Viatu), Sony (Bidhaa za Electroniki); Microsoft na Dell (Kompyuta); BP (Mafuta ya Petroli na vilainisha mitambo), Hyatt, Holiday-Inn na Days-Inn (Mahoteli), Western Union na Money-Gram (Utumaji fedha kimataifa kwa haraka), VISA na MASTERCARD (Kadi za plastiki zenye kubeba fedha ndani yake badala ya kubeba lundo la minoti) na kwa sasa hapa Tanzania, huduma kama M-PESA.
Yawezekana kabisa umewahi kutumia moja ya huduma hizi lakini fahamu pia kuwa, hadi kufika hapo zilipo kamuni hizo ziliwekeza mamilion ya fedha, miaka mingi, na ujasiri na uboreshaji wa mikakati kiasi cha kufikia kiwango cha juu kabisa na kutambulika kwa haraka, kukua kwa kasi na kujipatia maelfu (kama si milioni) ya wateja.
Baada ya maelezo hayo, yatafakari tena majina na alama za biashara (zikiwemo nembo) za makampuni haya. Utaona kuwa, alama za biashara za makampuni haya zimetengenezwa kwa ufundi na ubora wa hali ya juu na wamiliki walitumia kiasi kikubwa cha fedha kuandaa tu alama hizo, jambo ambalo kwa wafanyabiashara tusio na upeo hatuthubutu kulifanya kwa kisingizio cha kukosa mtaji, japo ungeweza kuanza na logo hata ya laki 1 (100,000/=) na bado ikawa nzuri tu kuitambulisha biashara yako.
Faida nyingine ya kusajili alama hizi (kama majina na maumbnile yake katik ukubwa na fonts (maumbile ya herufi) maalum za kompyuta ama za kuchora), picha na nembo (logo) ni kwamba zinasaidia sana mmiliki wa kampuni/bidhaa/ama huduma kuilinda biashara yake dhidi ya makampuni yanayokuja baadaye kutaka kuvuna kwa kupitia mgongo na jitihada za huyu aliyetangulia.
Katika Sheria za Hakimiliki yapo mashaui mengi tu yaliyofikishwa mahakamani pia kutolewa hukumu kuhusiana na udanganyifu utokeapo ambapo kampuni fulani hujaribu kutengeneza bidhaa inayofanana na ya yule aliyetangulia na ambaye bidhaa ama huduma yake imefikia kiwango cha juu cha ubora na kukubalika na wengi kiasi cha wafanyabiashara wengine wanaokuja baadaye kutaka kuinakili kwa faida zao.
Mara nyingi ghiliba hutokea ambapo mchakachuaji anayedurufu bidhaa ya mwingine hufikia hata hatua ya kusajili jina linalofanana na la yule wa awali kisha kupeleka katika soko (madukani/mitaani) bidhaa ambayo watumiaji wasipokuwa makini huweza kuamini kuwa wananua bidhaa ile ile waliyoizoea. Dhana hii huitwa ‘Passing off’ katika Sheria zinazohusika na wizi wa kazi za ubunifu zilizofanywa na wengine.
Ndiyo maana basi utaona kwamba ni vizuri sana ukaisajili biashara yako ama bidhaa yako ili kukulinda dhidi ya hujuma hizi. Hii ni hasa pale ambapo biashara yako inakua kwa kasi ama imeishashamiri na unaamini kwamba inashika usukani ama inakaribia kushika usukani katika soko la ushindani.
Haijalishi kama ni mabasi, huduma kwa watalii, unga wa mahindi, korosho zilizobanguliwa, juisi ya maembe, na kadhalika. Na kwa wale wanaoanza, usajili ni muhimu kwa sababu utaitambulisha haraka zaidi biashara yako. labda nikuulize? Bila kuwa na nembo ama alama nyingine ama jina la kuvutia la biashara, biashara yako unaamini imefanikiwa kiasi gani?
Tuishie hapa ila makala yanayokuja tutaangalia ni wapi unasajili mambo hayao na taratibu gani unapaswa kuzifanya kishera.
*Denis Maringo ni Mwanasheria/Wakili wa kujitegemea aliyeko jijini Dar es Salaam. Simu: 0719270067. Barua-pepe: dnmaringo@gmail.com










