Mwakilishi UNFPA: Kinga ya vifo wajawazito, ‘vichanga’ ni wakunga

11May 2023
Yasmine Protace
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwakilishi UNFPA: Kinga ya vifo wajawazito, ‘vichanga’ ni wakunga

WAKUNGA kitaaluma wanaangukia kundi la wauguzi wanaopatiwa mafunzo maalum, kuwahudumia wajawazito wakati wa kujifungua na katika kuthamini utaalamu wao, wana siku maalum wanayosherehekea kimataifa, kila Mei, 5 ya mwaka.

 

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Mark Bryan Schreiner, anasema dunia inashuhudia mwanamke akifa kila baada ya dakika mbili kutokana na ama ujauzito au kujifungua.

Schreiner anasema, UNFPA wanachukua hatua kupigania wakunga wajuzi, ikiwa ni njia muhimu ya kuepusha vifo vinavyozuilika vya uzazi na watoto wachanga. Hapo anafafanua:"Ikiwa kila mwanamke mjamzito angeweza kupata mkunga aliyefunzwa vizuri, anayejali, tungekuwa karibu zaidi na ulimwengu ambapo kila uzazi ni salama."

Anasema, kuna uhaba wa wakunga 900,000 duniani, huku kukiwapo dhana kwamba hao si wafanyakazi muhimu wa afya, lakini yeye anawasifu kuwa ndio wanaotoa taarifa muhimu za kiafya afya ya ngono na uzazi, kupanga uzazi na kuwasaidia wanakabiliana na masuala nyeti ya uzazi.

Pia, anawataja wakunga mara nyingi ndio wahudumu wa afya muhimu katika maeneo magumu kufikiwa, huku akiangalia upande wa pili wa shilingi,

kwamba madhara ya kuwakosa yanatisha ikiwamo vifo vya uzazi imesimama.

"Kila mwaka, wanawake 287,000 duniani kote hupoteza maisha wakati wa kujifungua; watoto wachanga milioni 2.4 hufa na wengine milioni 2.2 huzaliwa wakiwa wamekufa." anasema.

Anasema nchini Tanzania, wanawake 8,000 hadi 11,000 hupoteza maisha wakati wa kujifungua kila mwaka (takriban 30 kwa siku) na zaidi ya watoto 40,000 wanaozaliwa hawataona siku yao ya kuzaliwa.

"Haifai kuwa hivi! Upatikanaji wakunga kwa wote unatoa suluhisho bora na la gharama nafuu kukomesha vifo vya uzazi vinavyoweza kuzuilika. Kwa kufunga nakisi ya idadi ya wakunga, tunaweza kuzuia theluthi mbili ya vifo vya uzazi na watoto wachanga, kuokoa maisha ya zaidi ya milioni 4.3 kwa mwaka ifikapo 2035," anasema, akitaja kaulimbiu ya mwaka huu “Pamoja tena: kutoka kwa ushahidi hadi uhalisia.”

Anafafanua kwamba nchini Tanzania, UNFPA imeendelea kushirikiana  serikali kupitia Wizara ya Afya Bara na Zanzibar kuimarisha elimu ya ukunga, udhibiti, ushirika na mazingira wezeshi kwa vitendo vya ukunga, ikijumuisha uboreshaji vifaa vyao kwa vituo 64, mapitio ya mitaala ya uuguzi na ukunga na nyenzo za usaidizi.

Anaongeza kuwa UNFPA kwa kushirikiana na wadau wa TAMA, Wizara ya Afya, na Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto, Mtoto na Vijana (RMNCAH) wanaadhimisha tukio hilo kwa kufanya mjadala huo wa Jedwali la Duara kuhamasisha uwekezaji na kusaidia kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga nchini Tanzania.

"Kupitia kuimarisha elimu na mafunzo ya ukunga kwa kuzingatia waelimishaji wakunga ni matumaini yangu kwamba jedwali hili la mzunguko litaongeza dhamira ya serikali na washirika kuwekeza katika uzalishaji, usambazaji na uhifadhi wa waelimishaji wakunga waliohitimu na wenye uwezo," anasema.

RAIS WA WAKUNGA

Rais wa Chama Cha Wakunga Tanzania, Freddy Mwanga, anasema maana ya Siku ya Kimataifa ya Wakunga, wanakusanyika kusherehekea taaluma na kutambua jukumu lao katika kuhakikisha uzazi salama na wenye afya kwa wanawake na watoto wachanga wanaozaliwa kote duniani.

Anasema ni tukio la kuthibitisha uhusiano na wadau na washirika, akiitaja kaulimbiu ya mwaka huu ‘Pamoja Tena kutoka Ushahidi hadi Uhalisi,’ inayozungumzia umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano, ili kuziba pengo kati ya ujuzi wao; bora wa ukunga na uhalisia wa kinachopatikana kwa sasa katika sehemu nyingi za dunia.

Mwanga anasema Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea, elimu na huduma ya wakunga inakabiliwa na changamoto ya ubora wa huduma hizo, akitaja suala la kukubalika kwao  tata na hivi karibuni kumekuwapo maendeleo wakunga wengi wakipewa mafunzo na kupelekwa vijijini, maeneo yenye uhitaji.

"Kwa ujumla, nchini Tanzania wakunga wanaohitimu kutoka shule za uuguzi na ukunga wanahitaji mafunzo ya ziada ya huduma na ushauri, ili kupata umahiri unaohitajika na kufanya mazoezi ya ukunga kwa usalama. Kwa hiyo, katika hatua hii tujikumbushe kwamba si kila anayejifungua ni mkunga (kama ilivyozoekeka)…”

Anasema, mkunga sahihi anapaswa kuwa na ujuzi ulioainishwa na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Shirikisho la Kimataifa la Wakunga na kukidhi Fasili ya Mkunga na ICM iliyoidhinishwa na Shirika la Afya Duniani.

“Mkunga ni mtu ambaye amemaliza kwa mafanikio programu ya elimu ya ukunga ambayo imezingatia umahiri muhimu wa ICM kwa mazoezi ya ukunga na mfumo wa ‘ICM Global Standards for Midwifery Education’ na inatambulika nchini ilipo, ambaye amepata sifa zinazohitajika ili kusajiliwa,” anasema.

Anafafanua kwamba inamaanisha si tu kuwapa maarifa na ujuzi muhimu, bali na kuwatayarisha kuwa watoa huduma wenye huruma, na wanaojali utamaduni. Anaendelea: "Ili kufikia lengo hili, ni lazima tuwekeze katika maandalizi ya walimu wakunga bora ambao nao watazalisha wakunga wenye uwezo.

“Tunahitaji kuhakikisha kwamba walimu hawa wanapata fursa zinazoendelea za maendeleo ya kitaaluma na waweze kuendana na maendeleo ya hivi punde katika utunzaji wa wakunga."

Anaongeza kwamba, wanahitaji kutambua kwamba utunzaji wa wakunga hauwezi kuwapo kwa kutengwa na kunahitajika kufanywa kazi kwa karibu na watoa huduma wengine wa afya, watunga sera na viongozi wa jamii ili kuandaa mazingira wezeshi kwa huduma ya wakunga.

"Hii ni pamoja na kushughulikia masuala ya kijamii, kiutamaduni na kiuchumi ambayo yanaweza kuzuia upatikanaji wa huduma kwa wanawake, pamoja na kutetea sera na programu zinazounga mkono elimu na mazoezi ya ukunga,” anaeleza Rais huyo wa wakunga.

Mwanga anafafanua hoja yake kwamba, lengo ni kuwaandaa wakunga wenye uwezo watamkaofanya utambuzi wa ama kupunguza au kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika vya uzazi na watoto wachanga.

Anatumia mfano wa takwimu za Utafiti wa Afya ya Demografia Tanzania (TDHS), unaotaja mwaka 2022 vifo vya watoto wachanga vilikuwa 24 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai.

Kurejea Mwenendo wa Makadirio ya Uwiano wa Vifo vya Uzazi (MMR), na UNDESA/Divisheni ya Idadi ya Watu Kanda, mwaka 2000 hadi 2020, vifo vya uzazi vilikuwa 429 kwa mwaka 2015 na mwaka 2020 vilikuwa 351, vifo vingi ni vinavyozuilika, kama vile kuvuja damu, shinikizo la damu  na maradhi maambukizi.

 

"Hali hii inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa mzigo mkubwa wa vifo vya uzazi na watoto wachanga. Ingawa kiwango cha utoaji wa huduma katika vituo vya kutoa huduma kimeongezeka kutoka asilimia 60 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 80 mwaka 2021 (Ripoti ya DHIS2), wanawake wanaojifungua katika vituo vya afya mara nyingi hawapati huduma bora zinazohitajika kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO),” anasema.