“Haya mchele (samaki) huo chukua 30,000 hapa 45,000 mpatie huyo 50,000 kabeba yule 53,000 mpe…lete mzigo mwingine, tumalize…”
Ukifika eneo la soko la samaki Kunduchi, kwa usiye mwenyeji, sauti hizo zitakuchanganya na utajiuliza wauzaji na wanunuzi wanaelewana! Unapoingia kwenye eneo la ndani ya soko, unapita kwa makini, ukinyata, kuepuka utelezi.
Ni takribani wapigadebe watatu, wakiwa wamepanda juu ya baraza lililojengwa kwa saruji au unaweza kuita meza, kizimba ambacho huwapo kwenye masoko mengi nchini, lengo ni kwa ajili ya kupanga bidhaa mezani zinazouzwa.
Nipashe inakutana na hali tofauti katika soko la Kunduchi, matumizi ya meza hizo hubadilika kulingana na muda na mara nyingine huwa jukwaa, mpigadebe hupanda juu, akisimama ili aonekane na anaowapigia debe, yaani wanunuzi.
Mwandishi wa habari aliyedumu hapo kwa takribani saa tano, anashuhudia mengi, ikiwamo mazingira ya shughuli hizo sokoni hapo, kundi la kinamama wengi wenye vazi maarufu katika ukanda wa pwani, dera, wakiwa wamekaa ndoo zao za plastiki za ujazo tofauti, lita 10 na 20.
Baadhi yao wana chupa ndogo za plastiki zenye maji, si ya kunywa bali kwa shughuli maalum na dharura, iwapo akashika samaki ajisuuze mikono kuondokana na shombo yao.
Pembeni ya kinamama hao, kuna kijana aliyevalia fulana ya mikono wazi, ameshika fagio akifanya kazi ya kusukuma maji (waiper), anasukuma tope la maji kuelekea, ulikolalia mteremko wa maji.
Kinamama hao kazini wapatao 20, nao wamewazunguka wapigadebe hao waliopanda juu na kusimama juu ya meza ya ‘vizimba’ vya samaki, kila mmoja akisikiliza kwa makini kila bei inayotajwa, akiwa na uwezo nayo ananyoosha mkono juu, asipopata mpinzani, bahati yake, anachukua mzigo wa samaki.
Pembezoni mwa soko yaani ulipoishia ukuta wa jengo hilo, wapo vijana kadhaa maalum kwa ajili ya kuparua samaki. Wapo wanaofanyia shughuli hiyo mezani, au sakafuni, wakitanguliza kibao kidogo chini cha ukubwa wa inchi mbili.
“Mazingira bado, hapa uje siku mvua imenyesha au msimu wa mvua ilipochanganya Februari hadi Aprili, hapatamaniki, tope maji hakuna. Unakuwa na chupa ya plastiki zilizotupwa uchota maji baharini ili ukishauza samaki, ujisuuze,” anatamka mmoja wa wavuvi, anayejitambulisha kwa jina moja Issa.
Kwa muda Nipashe, inakaa sokoni hapo inaanza mahojiano na wavuvi, ambao kwa majira hayo ni wanaofika na samaki kutoka baharini, baada ya safari ya saa tatu au sita baharini kutafuta kitoweo hicho chenye umaarufu kwa wakazi wa ukanda wa pwani.
Katika mahojiano na baadhi yao ambao walifika kwa awamu, hawakutaka kupoteza muda, pamoja na kukubali kuhojiwa na kuelezea shughuli zao mafanikio kiuchumi na changamoto wanazokumbana nazo.
WADAU WAFUNGUKA
Salum Mohamed (25), mvuvi na mkazi wa Kunduchi asili yake ni kisiwani Pemba, Zanzibar ana simulizi kwamba. Na muda mrefu kwenye uvuvi, akisema wavuvi huhama kutoka fukwe au soko tofauti kulingana na maslahi.
“Nilihama Pemba kipato kilikuwa kidogo, unaweza upate samaki ila usipate fedha. Bei ilikuwa ya chini. Nilikuwa nauza kwa mafungu na fungu moja lina samaki watano au sita, hatupimi kwa kilo…
“Ukitoka baharini kuvua mvuvi kuna dalali unampatia, anauza, mvuvi hapati, mi kwa siku napata 20,000 au 30,000 inategemeana. Samaki maarufu kupatikana hapa (Kunduchi) ni kolekole, taa, changu.
Salum anaendelea kuelezea huku mavazi yake bado yakiwa na ubichi kutokana na maji ya baharini, anasema pamoja na kuchukua saa nne au tano baharini, ipo siku hata nyumbani kwake kitoweo cha samaki hukosekana kutokana na hali ya bahari.
“Kutokana na upepo wa bahari, au shwari, unaweza usipate kitu, ila ulipata pesa unaotumia mahitaji ya nyumbani tu. Ila pesa ninayopata huwezi kuiweka akiba. Utakuta mmeenda uvuvini wawili, au watatu mnagawa fedha mliyopata.
Anasema zana za uvuvi wanazotumia ni ngalawa anayoitegemea kwa asilimia 90 ikitembea kwa upepo na kadri na anavua kwa kwa kutega ndoano majini akikadiria kikapu kimoja au nusu humchumkua nusu kutwaa.
“Bahari yaani hapa tulipo ufukwe ulikuwa mbali, miaka mingi lakini, ila sasa umesogea. Sijui ni kwa nini? Tunapokuwa baharini, upepo ukiwa mdogo ujue hii chombo chako kitatumia saa nyingi kufika eneo lako, anaeleza.
Hali ya baharini, Salum anaifafanua kwamba, joto linaongezeka na ufukweni ni kawaida kukutana na taka aina tofauti hasa za plastiki za chupa za maji, juisi au kimiminika chochote.
“Mfano siku bahari ni shwari kabisa hakuna upepo, kwetu sisi wavuvi si shwari kwa sababu chombo changu kinaendeshwa na upepo, hapo itanipasa nipige makasia hadi nifike na safari itachukua saa tano badala ya tatu au nne.
“Lakini, iwapo chombo kimeungwa mashine (motor) tungeweza kupata zaidi sababu tungeenda mbali, samaki wengi wapo kina cha mbali ukivua jirani na ufukwe unapata kidogo. Ila mashine hizo pia zingetusaidia siku ambazo bahari ni shwari yaani hakuna upepo,” anasema Salum.
“Mwandishi kwanza unatumia muda kunihoji, wavuvi tuna changamoto nyingi, ushuru boti inapoingia tu tunalipa, ila mazingira si mnayaona, kila siwezi kuzimaliza sina muda, nataka nikaswali,” anasema Salum muda mfupi baada ya kukutana na mwandishi wa makala, akiwa katika unadhifu anakipunga upepo na wenzake ufukweni, kandoni ya ngalawa yake.










