Misemo 'utakiona cha mtema kuni', 'ulimi uliponza kichwa', ilipoanzia

04Mar 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Misemo 'utakiona cha mtema kuni', 'ulimi uliponza kichwa', ilipoanzia

NIMEPOKEA simu na meseji nyingi sana baada ya makala iliyopita yenye kichwa cha habari 'hadithi za zamani bila sungura hainogi.'

Watu wengi waliowasiliana na mimi, walisema wamekumbuka mengi, wengine wakinikumbusha vitu vingine ambavyo vilisahaulika kuwekwa.

Kwa kukumbushia tu nilieleza kuhusu watoto wa zamani kupigiwa hadithi na babu na bibi zao, au watu wengine waliowazidi umri.

Hadithi hizo zilizoitwa za mapokeo zilizokuwa zikirithishwa kutoka kizazi hadi kizazi, zililenga kuelimisha.

Nikaeleza lengo lilikuwa ni  kuwaburudisha, kufundisha, kudumisha tamaduni, ikiwemo kuwaepusha watu na matatizo yanayoweza kuwakabili kwa kuwatia hofu.

Ndiyo maana likabuniwa jitu la kutisha lililopachiwa jina la zimwi. Lengo ni kuwafanya watoto wawe waoga kwa kile ambacho wazee wanaona watoto hawatakiwi kufanya, ama kwa wakati wa utoto wao, au maisha yote kwa ujumla.

Wengi walinikumbushia hadithi mbalimbali za wanyama na zingine za wafalme na masultani.

Kwa sasa hakuna wasimuliaji hadithi tena wala wasikilizaji. Wazee wamekuwa na mishemishe nyingi, huku watoto nao akili zao kwa sasa zipo zaidi kuangalia katuni za wanyama, au filamu kwenye televisheni.

Tangu miaka na miaka hadi kizazi cha sasa kumekuwa na misemo mbalimbali inayotumika, lakini asili yake ni kwenye hadithi za mapokeo.

Mfano ni ule unaosema 'utakiona cha mtema kuni.' Huu ni msemo maarufu sana. Ukimfanyia mtu ubaya na akataka kulipa kisasi anaweza kukwambia kwa hasira kuwa 'utaona cha mtema kuni.' Yaani ni lazima tu alipize.

Pale nyumbani mtoto akivunja sahani na mama yupo kazini, dada  au kaka  atamwambia  kwa kumtisha, utaona cha mtema kuni mama akirudi. Maana yake ni kwamba atakaporudi mama utachapwa au kupewa adhabu. Shuleni wanafunzi wamewahi namba, halafu wengine wakachelewa, basi waliowahi watawaambia wenzao kuwa kwa sababu wamechelewa, basi watakiona cha mtema kuni, ikiwa na maana. Una kesi mahakamani, kabla ya kusomwa, anakuja asiyekupenda au ambaye yupo upande wa pili wa kesi hiyo, atakwambia "yaani leo, lazima utakiona cha mtema kuni, lazima ufungwe."

Mtema kuni ni nani? Nadhani wengi wao kizazi hadi kizazi wanautumia msemo bila kujua ulitokea wapi. Leo utajua.

Pia upo msemo mwingine maarufu unaosema 'ulimi uliponza kichwa.' Huu unawahusu watu wanaopenda kuongeaongea sana, au kuropoka vitu visivyowahusu, vile vile kufanya umbea. Nao pia si wengi wanaojua msemo huu umeanzia wapi.

Misemo hii yote imetokana na hadhithi moja tu inayoitwa 'kisa cha mtema kuni.'

Mtema kuni ni mtu anayekata kuni. Hadithi hiyo ya mapokeo inasema hapo zamani alitokea mtema kuni ambaye kazi yake kubwa inayompatia kipato yeye na familia yake ni kwenda porini kukata kuni, halafu akirudi mjini anauza kwa watu mbalimbali kwa ajili ya kushughuli mbali mbali za kupikia.

Siku moja akiwa porini kwa shughuli zake hizo, alifika kwenye mti mmoja ambao alipotaka kuukata ukaomba auache, asiukate.

Mtema kuni alishangaa sana kwa sababu haikuwa jambo la kawaida mtu kuongea kama binadamu. Kwanza alishtuka, mshangao ukafuata baadaye. Lakini akatekeleza ombi la kutoukata. Akakata miti mingine na kuni akazipeleka kuuza mjini kama kawaida.

Siku ya pili akiwa tena porini, alipita pale pale kwenye ule mti. Alipopita tu, ulianza kuongeza. Safari hii si kumuomba usikatwe, bali uliongea maneno yafuatayo."Ulimi uliponza kichwa." Mti ukawa unayarudia maneno hayo mara kwa mara mpaka alipopita.

Tukio la mti kuongea, tena siku mbili mfululizo liliendelea kumfanya mtema kuni awaze sana. Hakumwambia mkewe wala mtu yoyote, lakini ni kama vile alikuwa na dukuduku.

Siku ya tatu akiwa kazini kwake, baada ya kukata kuni zake na kuzibeba akirejea mjini, alipita tena pale pale. Mti uliendelea kuongea maneno yale yale ya siku ya pili, "ulimi uliponza kichwa."

Safari hii hakuvumilia tena, alipofika mjini alianza kuwasimulia majirani wa himaya hiyo anayoishi juu ya kuwepo kwa mti unaoongea kwenye pori lililo kwenye himaya yao.

Na hata siku ya nne alipokwenda hali ikawa vile vile. Mfalme wa himaya hiyo akasikia habari ambazo zimeanza kusambaa juu ya kwenye himaya yake kuwa kuna mti unaoongea kama binadamu.

Akataka kujua chanzo cha habari hii na ni nani mtu wa kwanza kuiwasilisha. Akaletewa taarifa kuwa hakuna mtu yoyote kwenye himaya hiyo ambaye amewahi kuusikia mti huo zaidi ya jamaa mmoja mtema kuni ambaye kuingia porini kwa ajili ya kukata kuni na kuziuza.

Akaamuru aletwe mbele yake. Watumishi wakampeleka mbele ya mfalme. Akaulizwa kama yale yanayosemwa na yeye ndiye chanzo kiasi cha kuvuma kwenye himaya yake ni ya kweli.

Mtema Kuni alikiri kuwa ni kweli kwenye pori ambalo huwa anakwenda kukata kuni, kuna mti ambao unazungumza yeye ameusikia sasa zaidi ya mara nne kwani hupita hapo hapo kila siku anapokwenda na kurejea kwenye kazi zake.

Mfalme anakamwambia yeye, walinzi, watumishi na baadhi ya mawaziri wake wanataka kwenda kuuona mti huo na kuusikia jinsi unavyozungumza. Lakini kama maneno anayosema hayo si ya kweli, ni lazima apate adhabu. Na hiyo si nyingine bali ni kukatwa kichwa.

Mtema Kuni hakuwa na wasiwasi kwa sababu jambo hilo ni la kweli, akakubali. Safari ilianza, lakini walipofika hapo na kuwaonyesha mti ambao unazungumza kama binadamu haikufanya hivyo.

Zaidi ya masaa mawili mti haikuzunguza lolote. Mfalme akakasirika akaamuru waondoke. Hakutaka kumuadhibu Mtema Kuni, akasema na kesho watarudi tena. Waliporudi hali ikawa ni ile ile. Hii ilimtisha sana Mtema Kuni, kwani sasa alionekana muongo, tena mbaya zaidi mbele ya mfalme.

Siku ya tatu walikwenda tena, ule mti haukuzungumza. Mfalme akamwambia Mtema Kuni angeweza kumkata kichwa siku ya kwanza tu, lakini amemuacha ili kutoa muda kama jambo lile ni la kweli au la. Na kwa jinsi ilivyo, akamwambia kuwa ni muongo, amewaongopewa watu wote wa himaya yake, pamoja na yeye mfalme, hivyo hukumu yake ni kukatwa kichwa, tena pale pale porini na maiti yake iachwe hapo hapo.

Amri ikatekelezwa. Mlinzi mmoja akamkata kichwa Mtema Kuni kwa kutumia jambia. Kichwa kinatenganishwa na kiwiliwili. Cha ajabu ni kwamba baada ya tukio hilo, Mti ulianza kuongea hapo hapo. Na maneno yalikuwa ni yale yale."Ulimi uliponza kichwa."

Mfalme na ujumbe wake ulilia sana, kwani ilionekana kumbe Mtema Kuni hakuwa muongo. Hakupaswa kufa. Akachukua maiti ya Mtema Kuni kwenda kumzika kwa heshima kubwa. Hadithi hii ndiyo iliyozaa misemo miwili maarufu. "Utakiona cha mtema kuni', na,"ulimi uliponza kichwa."