Mtu akisafiri kwa anga iwe kwa helikopta au aina nyingine ya ndege, anapoanza ama kupaa au kutua, anaona mandhari ya eneo husika jinsi ilivyo, kama imepangwa au iko kwa muundo wa ‘bora liende.’
Mpangilio wa mji huvutia kutazama kwa kuwa kama ni eneo lenye ghorofa huonekana hivyo, kama ni nyumba za kawaida unazikuta katika eneo husika zikiwa kwa muundo huo.
Mpangilio wa aina hiyo huupendezesha mji au jiji na kurahisisha huduma mbalimbali za kijamii kama miundombinu ya maji safi na salama, gesi, umeme, ikiwa ni pamoja na kurahisisha kunapotokea majanga ya moto.
Miji ambayo haijapangwa huwa vigumu kukabiliana na majanga mbalimbali hasa ya moto, kwa kuwa kila mtu hujenga nyumba kwa kadri anavyoona inafaa na siyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Hiyo inakumbusha wakati Fulani, aliyekuwa Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana alipolalamika kwamba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, hupata shida kubwa kukabiliana na mjanga ya moto wakifika wamechelewa, kutokana mpangilio usiofaa wa jiji.
Ipo taarifa kwamba asilimia 70 ya jiji la Dar es Salaam, halipo katika mpango mji na kuangukia katika lile kundi la pili la ‘bora liende.’
JIJI LA JOHANNESBURG
Unapotembelea mji wa Johannesburg, nchini Afrika Kusini utajionea jinsi gani mipango miji inapaswa kuwa, ukiwa angani na utafurahi kuendelea kuwepo huko kuangalia mji ulivyopangwa.
Ukiwa kwenye ndege wakati wa kupaa na kutua utaona mji ulivyo na mpangilio na barabara zake zinaonekana vizuri, kwani kama eneo fulani lina aina fulani ya nyumba eneo hilo zinafanana na hakuna mtu kujiamua kufanya atakavyo.
Kama eneo limekubaliwa kujengwa nyumba za ghorofa mbili huwa hivyo na kama eneo ni la nyumba za kawaida huwezi kukuta ghorofa imeota katikati,kama eneo limekubaliwa kuwa la viwanda ni viwanda pekee na kama ni maduka inakuwa ni maduka pekee.
Kwa ujumla, ni mji wenye wa kuvutia hata kwa muonekano au kutembelea. Ni mpangilio unaorahisisha utendaji kazi kuanzia kusafisha, kushughulikia majanga yanapojitokeza na kupanga miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa ni kipimo cha maendeleo ya nchi husika.
Kipimo cha kwamba mji au jiji limeendelea, ni jinsi miundombinu yake ilivyopangwa na mipango miji yake, kwa kuwa huwezi kukuta mpangilio wa ovyo.
Mtu anayezuru nchini ya Kiafrika kama vile Afrika Kusini kwa mara ya kwanza, atavutiwa sana kuona ni mji wa nchi ya dunia ya tatu, lakini umepiga hatua kubwa.
Hilo linamfanya aendelea kukaa humo kwa kuwa miji yake yote imepangwa kwa utaratibu wa mipango miji kuonyesha kuwa sheria, taratibu na kanuni zinafuatwa na siyo kila mtu kutumia misuli ya fedha kufanya jambo fulani.
Miji imepangwa kuanzia miundombinu ya barabara ikiwa ni barabara za juu na za chini na yote ikiwa na mpangilio sahihi na hakuna waliojenga karibu na hifadhi ya barabara na kusubiri kuondolewa na serikali. Pia nyumba zimejengwa kwa utaratibu maalum unaofuata sheria.
Kutokana na mpangilio huo, usafi wake umekuwa rahisi kufanyika mji muda mwingi kuonekana ni safi, pia vifaa vya kuhifadhia taka vimewekwa kila eneo na hivyo siyo rahisi kukuta uchafu umezagaa na hivyo kuwa kipimo cha nchi kipiga hatua ya maendeleo.
Mpangilio uliopo Afrika Kusini siyo rahisi kuukuta Tanzania au nchi nyingine za Afrika. kwa miundombinu na mipango miji ilishaingiliwa kwa kiasdi kikubwa.
ULINGANISHI NA TANZANIA
Kulikoni nchini Tanzania? Bado kunaonekana kushikwa na ugonjwa wa kushindwa kuheshimu sheria na taratibu za mipango miji na badala yake, ukiukwaji na ujenzi wa ‘nguvu ya fedha’ imetawala.
Hiyo ndiyo inafanya hata mtu anapotembea kwenye jiji kama Dar es Salaam, kuna upungufu dhahiri wa mipango miji, ikiwamo udhaifu kama vile kukosa mpangilio kwa wasimamizi wa sheria kushindwa kutekeleza wajibu wao na wananchi kufanya watakavyo.
Awali taratibu za ujenzi nchini Tanzania haikuzingatia kwa mwenye kiwanja kuwa na kibali cha kumruhusu ujenzi, baada ya mpango wake kuthibitishwa na mamlaka husika. Hivi sasa kuna mabadiliko na hilo limeanza kufanyika.
Mwaka 2003, serikali ilibuni utaratibu maalum ulioitwa Mradi wa Viwaja 20,000. Hiyo ilikuwa ni pale serikali ilipokopa kiasi kikubwa cha fedha na kupima idai hiyo ya viwanja jijini Dar es Salaam na kuanza kuuzia wananchi.
Mradi huo ulipanuliwa zaidi nje ya Dar es Salaam kwa halmashauri husika kujipanga na kukopa fedha hizo maalum na kisha kuuzia wakazi wake na fedha zinazopatikana, zinarudishwa kwenye mfuko maalum zilikoKopeshwa.
Kuna halmashauri mbalimbali ambazo zimezipa kasi baadhi kampuni kupima na kuuza viwanja kwa utaratibu maalum. Yote hiyo inaangukia katika taratibu za kuboresha mipango miji, ikiwemo kuruhusu mtu mmoja mmoja kupimiwa kiwanja.
Kwa sasa, serikali ya awamu ya tano inapambana na mipango miji kwa kuwataka wote waliojenga nje ya mpango mkuu wa upangaji mji, kuanza kubomoa na lazima ufuatwe na kuheshimiwa.
Wakati serikali inatangaza hayo tayari miji na majiji mengi hayajapwanga na ujenzi umefanyika holela kiasi cha kufanya utendaji kazi yanapotokea majanga, kupitisha miundombinu ya barabara, maji safi na majitaka kuwa mgumu.
Kwa ujumla, mtu anapokuwa angani na kuiangalia Dar es Salaam jinsi ambavyo imejengwa ni ‘ili mradi.’ Hakuna mpangilio.
Licha ya kila manispaa kuwa na mipango miji, lakini usimamizi ni wa kusuasua na ndiyo maana kila mtu ameamua kujenga kwa kadri anavyoweza ikiwa ni ghorofa au nyumba ya kawaida.
Pia, wengine hubadili matumizi ya eneo husika na kujenga ghala la kuhifadhia mzao au bidhaa nyingine, kuanzasha gereji na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake.
Hilo ni tofauti kwa nchi kama Afrika Kusini ambayo mtu anapojenga, ni lazima awe na kibali kwa kuwa sheria zinafanya kazi hazijabaki kwenye makaratasi na kujazwa kwenye makabati ofisini.
Neema Ole Nasha, ni Mtanzania anayeishi Afrika Kusini katika mji wa Sandton. Anasema sheria na taratibu katika kupata ardhi ya kumiliki zinafuatwa, ikiwa ni pamoja na hatua za ujenzi.
“Huku huwezi kuwa na kuwanja ukaanza kujenga utakavyo kama ilivyo nyumbani (Tanzania), lazima ufuate sheria za mipango miji na wanapobaini umekwenda kinyume huvunja mara moja. Rushwa haina nafasi kabisa na ndiyo maana unaona mji wa wenzetu umepangwa vizuri,” anasema.
Nasha aliyeishi nchini humo kwa miaka mitano, akijishughulisha na kuwezesha wanawake na urembo, anasema iwapo nchi za Afrika zingeiga uendeshaji huo kwa misingi ya sheria, ni wazi zingepiga hatua kimaendeleo.
Hiyo ni kwa sababu mpangilio wa mji wake, hakuna anayeruhusiwa kwenda kinyume kwa kutumia fedha zake.
“Angalia mji huu ulivyo hata kama eneo ni lako lazima ujenge kwa jinsi ramani za eneo husika zilivyo na siyo unataka kujenga ghorofa basi unafanya hivyo, hata kama unafedha kiasi gani kinachoangaliwa ni mipango miji iliyopo,” anafafanua.
Anasema mpangilio huo umerahisisha kwa kuwa ramani za maeneo husika zipo, barabara zimepangwa, nyumba zimepangwa na mji unapendeza, miundombinu ya maji na umeme imepangiliwa ipasavyo na hakuna majanga kama ya moto, uchafuzi wa mazingira kwa maana ya maji kuchafuka kwa kuwa watu wanaweza kuingila mtandao wa maji kwa lengo la kujiunganishia.
Anasema nchini humo kama mtu hawezi kuendeleza eneo kwa kadri ya ramani ya eneo husika, anapaswa kupisha na siyo kujenga utakavyo.










