Utapeli na kughushi nyaraka, ni kati ya vikwazo katika sekta ya ardhi, vimekuwa vikisababisha kutokuelewana kati ya jamii moja na nyingine, hata kukosekana maendeleo ya jamii kwenye maeneo yao.
Mkoa wa Pwani ni sehemu mojawapo ambako migogoro imesheheni, ikiwamo maeneo; Kibaha, Bagamoyo eneo la Mapinga na katika Halmashauri ya Chalinze.
Hapo na kwingineko mkoani Pwani, migogoro yake imejikita kwenye uvamizi wa maeneo yenye hati miliki, msuguano kati ya wakulima na wafugaji kuingiliana kwenye maeneo ambayo tayari ina mipango ya matumizi tofauti kisheria.
Kinachotokea, baadhi ya wananchi wamekuwa wakivamia maeneo yenye hati miliki na kujigawia, bila kufuata sheria na kanuni, huku wakiwatupia
lawama wamiliki kwamba wameyatelekeza kwa muda mrefu, pasipo kuyaendeleza. Pia, kuna kundi la matapeli wanaojivika kazi za
udalali, wamekuwa wakiyauza maeneo hayo na kuchangia kuwapo migogoro isiyoisha.
Kikwazo kingine kinatajwa, ni cha eneo la mazingira na
jamii kuwapo wanawake wachache wanaomiliki ardhi na ushirikishwaji duni wa wadau, hasa jamii za kifugaji na makundi maalumu.
HATUA YA KISERIKALI
Kukithiri kwa hali hiyo kumeifanya serikali kutafuta fedha kutoka Benki ya Dunia, kuandaa mradi wa kumaliza shida hiyo, ikilenga usalama wa milki za ardhi, utekelezaji wake miaka mitano kuanzia Mei mwaka jana, ukitarajiwa kukamilika Mei 2027.
Mratibu wa mradi huo, Joseph Shewiyo, kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, anasema utekelezaji wa mradi huo, pia utaongeza uelewa na usalama wa ardhi, kwa kuzingatia nafasi ya jinsia na kuongeza idadi ya Watanzania wanaomiliki nyaraka za umiliki, huku wakipunguza muda unaotumika kupata nyaraka hizo.
Shewiyo anataja mambo mengine ni katika malengo yake mahususi, kwenda sambamba na kuongeza idadi ya miamala itokanayo na nyaraka za umiliki, iendane na
ufanisi katika uandaaji wa nyaraka hizo.
Shewiyo anataja maeneo ya mjini wanakotekeleza hilo ni katika halmashauri za; Jiji Dodoma, Chalinze, Mafinga, Rungwe, Korogwe, Tarime, Nzega, Kigoma Ujiji, Kibaha Mjini, Bariadi, Iringa, Tanga, Tabora na Geita.
Pia, anataja halmashauri za; Shinyanga, Kahama, Jiji la Mbeya, Moshi, Kondoa, Bagamoyo, Kilolo, Kaliua, Bukombe, Musoma, Kishapu na Wilaya ya Moshi.
Hilo linaendana na mradi katika maeneo ya vijijini, anakokutaja kuwa ni Mbinga, Tanganyika, Songwe, Chamwino, Maswa, Mufindi na Longido.
KAZI ZITAKAZOFANYIKA
Akizungumzia kuhusiana kazi zitakazofanyika katika mradi huo, ni utoaji wa hatimiliki milioni mbili katika
maeneo ya mjini.
“Tutatumia asilimia 20 ya watumishi wa serikali na kampuni zilizosajiliwa zitafanya kazi za kupanga na kupima kwa asilimia 80 na kazi ya mfano imeanza katika jiji la Dodoma na kata tatu zimechaguliwa” anaeleza.
Shewiyo anasema, kuna halmashauri nane zinaanza kwa mwaka wa kwanza wa mradi ambazo ni
Dodoma Jiji, Chalinze, Mafinga, Rungwe, Nzega, Tarime, Korogwe na Kigoma Ujiji.
Anagusia pia kutatolewa hatimiliki za kimila 20,000,
kazi inayofanywa na watumishi wa serikali na taasisi zisizo za kiserikali, akitaja kazi zitakazofanyika katika maeneo hayo ya vijijini, ni, kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya wilaya sita.
Mratibu huyo wa Ardhi, anasema kuna jumla ya
vijiji 250 vitakavyopimwa mipaka yao, pia mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 250, ikiandaliwa mipango ya kina katika vitovu vya vijiji tajwa.
Anaeleza kuwapo maandalizi ya ramani za msingi
itakayofanyika, kwani ramani zilizopo sasa ziliandaliwa zama za miaka ya 1990, ikiwamo wastani wa miaka 30 sasa, hivyo zinahitaji maboresho, kazi itakayofanywa kwa uwezo wa ndani ya nchi.
Anasema, uboreshaji wa alama za msingi, pia utafanyika kwa kusambazwa maeneo ya mradi, ili kuongeza ufanisi wa upangaji na upimaji nchini.
MIRADI ILMS
“Uboreshaji wa mfumo wa ILMIS utafanyika ili uweze
kutumika nchi nzima baada ya kujaribiwa mikoa ya Dar es Salam na Dodoma,” anasema.
Ni mradi utakaokaribisha ujenzi wa ofisi za ardhi mikoa 25, ukarabati wa ofisi ardhi katika halmashauri 41, kukarabati masijala ardhi za vijiji 250, kujenga jengo la kumbukumbu za ardhi nchini na madarasa makubwa mawili.
Anasema, mradi huo pia una utaratibu wa
kuandaa nyaraka mbalimbali na utekelezaji wa usimamizi wa mazingira na masuala ya kijamii, pia utafiti na kuandaa miradi.
Kwa mujibu wa Shewiyo, inayaangalia pia kuwezesha
wanawake na haki za ardhi, pia ushiriki wao kwenye masuala ya kukabili ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Mratibu anataja eneo lingine la kutekeleza malengo ya mradi ni mifumo ya utawala wa ardhi, ili kupunguza gharama na muda wa upatikanaji wake, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku kukipunguzwa kasi ya ukuaji wa makazi holela.
NAIBU WAZIRI
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete, anasema ni
mradi unaoelekea kumaliza migogoro ya ardhi, inayojitokeza kila mara.
Ridhiwani, ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze, anasema serikali imetambua uwapo wa migogoro isiyoisha katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo imefikia hatua ya kutenga kiasi Sh. bilioni 345 za kupima ardhi nchini.
Anasema, katika hatua ya awali kuna halmashauri 41 nchini ikiwamo Chalinze, akiahidi suluhisho la migogoro kati ya kata, pia vijiji, hata inakwamisha maendeleo ya kijamii.
“Tunakwenda kutambua maeneo ya wakulima na wafugaji na katika hili, shughuli ya upimaji itafanywa na wenyeji kwa kuwahusisha vijana katika upimaji huo, huku wazee nao wakipewa nafasi kutokana na kuwa na historia za mipaka kwenye vijiji vyao,” anasema.
Naibu Waziri huyo anayetumikia sasa nafasi hiyo katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), akaahidi Wizara ya Ardhi kuwaletea wataalamu kuwapimia, kisha vijana watapewa mafunzo kwenye kazi hiyo, vikitumika vifaa vya kisasa.
“Mkichukua watu ambao sio wenyeji kwenye eneo husika, mtasababisha migogoro, kwa maana watakuwa hawajui vizuri eneo hilo. Zingatieni kutoa
kipaumbele kwa vijana wa eneo husika, ambao wataambatana na wataalamu kufanikisha kazi hii na kumaliza migogoro kwenye maeneo yetu.
“Rais Samia Suluhu Hassan amechoshwa na migogoro ya ardhi, ameamua kufikia hatua hii kutenga fedha kwa ajili ya kupima maeneo yetu, kila mtu atapimiwa eneo lake na kila kijiji na kata watapimiwa kujua mipaka yao na baada ya hapo kutatengenezwa ramani,” anasema.
Anasema kumekuwapo migogoro mingi ikiwemo ya wakulima na wafugaji na mipaka na ili kuondoa migogoro hiyo ni kupima ardhi jambo ambalo serikali iko mbioni kulifanya.
Ridhiwani anakiri Chalinze ni kati ya halmashauri zenye migogoro ya ardhi lukuki.