Michezo ya watoto iliyopotea

02Apr 2022
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Michezo ya watoto iliyopotea

Ukiangalia zamani na sasa, utagundua kuwa watoto na vijana wa miaka ya nyuma walikuwa wanacheza michezo mingi iliyosababisha kuwa imara kiafya, pamoja na utimamu wa mwili. 

Leo tunaangalia michezo ya watoto kuanzia miaka ya nyuma hadi katikati ya miaka ya 1990, ilipoisha nguvu. Tunaanza na michezo ya watoto wa kike.

Kwanza kabisa kulikuwa mchezo wa kipande. Huo ulichezwa kwa kuchora kwenye ardhi mistari mingi mfano wa boksi. Sehemu moja ya boksi ilikuwa tupu na nyingine imekatwa kati na mstari mwingine.

Mchezaji anatakiwa kukanyaga mguu mmoja kwenye boksi ambalo liko tupu na miguu miwili boksi ambalo katikati litakuwa limepigwa msitari.

Mchezo mwingine maarufu ni 'rede'. 

Wanawake, kuanzia watoto wa miaka mitano, saba na kuendelea wakati mwingine hata mpaka miaka 25, walikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza mchezo huo.

Ulichezwa kwa mmoja kukaa upande huu na mwingine upande wa pili, mmoja akiwa kati. Hawa wa pembeni wanakuwa na mpira mmoja, kazi yao ni kurusha ili kumbabau au kumpiga yule wa kati.

Wa kati kazi yake kubwa ni kukwepa mpira ambao wenzake wanawania kumbabua nao. Burudani ya mchezo huo kwa waangaliaji ipo zaidi kwa yule wa kati, kwani walikuwa na staili mbalimbali za kuukwepa mpira huo, ambao ndiyo unaosisimua na kuchangamsha mchezo mzima.

Ataruka juu mpira upite kati. Atanyumbulika kama mcheza sarakasi, atainama, atapiga magoti, au kuanguka chini, ili mradi tu mpira usimpige.

Kujipikilisha pia ni mchezo wa watoto wa kike ambao walikuwa wakiigiza mama zao kupika. Kuna wadogo zaidi waliopika kwa kutumia michanga, makopo, au sufuria ndogo na moto wanaochukua kutoka kwa mama zao.

Wakati mwingine wanachezea mwanasesere, na vitambaa, wanajenga nyumba kwa kutumia michanga na udongo, huku wakiigiza kama wao ndiyo mama wenye nyumba na wanasesere ni watoto. Basi watawaogesha na kuwavisha nguo nzuri kama binadamu, na hata kuwakaripia, wakiiga yale yale yanayofanywa na mama zao, kwao.

Kulikuwa na michezo ya kuruka kwamba. Yote hiyo ni kwa watoto wa kike.

Michezo ya kiume kwanza kabisa ilikuwa ni mpira wa miguu, sarakasi, na kuna michezo hatari ya kujivingirisha katikati ya gurudumu, huku watoto wengine wakiwa wanaliendesha.

Michezo mingine ya hatari ambayo hii ilikuwa ikikatazwa na wazazi, lakini watoto walikuwa wafanya kwa uficho ni kudandia magari.

Kombolela ni mchezo mwingine ambao wengine wanakwenda kujificha, mmoja anakuwa analinda chupa moja ya plastiki isipigwe teke na yeyote aliyekuwa amejificha.

Kanuni ni kwamba wa kwanza kutajwa ndiye anayelinda au kusafa kama lugha ya mchezo inavyosema.

Msafaji atamtaja mmoja mmoja atayejitokeza kwa lengo la kutaka kubutua, au kupiga teke chupa ile kabla hajaifukia. Chupa ikipigwa teke kabla hajataja jina, basi wote waliotajwa watarudi tena kujificha na yeye ataendelea na kazi ile ile, hadi atakapofanikiwa kutaja wote. Hii inamfanya msafaji awe makini mno. Huu ni mchezo wa watoto wa jinsia zote.

Michezo mingine ya watoto wavulana kwa wasichana ni ‘tayari bado’, kucheza kwenye mvua, ukuti ukuti, kioo alikivunja nani, na hata kula mbakishie baba, ambao mtu akiangusha kijiti, anachezea kichapo hadi aende kushika kitu walichoahidiana kama mtu, nyumba, au chochote kile ambacho ukikifikia na kukishika umeua adhabu ya kupigwa kwa kosa la kuangusha kijiti.

Michezo mingine ya wavulana ni goroli na kutengeneza magari kwa kutumia mabua ya mti mbalimbali kwa wale wa vijijini, lakini kwa mijini watoto walitumia sana maboksi na makopo.

Kuendesha magurudumu ya gari, pikipiki, basikeli, au ringi, na hii iliwafanya watoto kupendwa kutumwa na mtu yoyote yule wa jirani, si lazima awe mzazi wake, ili aende dukani au sehemu yoyote ile mbali, apate nafasi ya kuendesha au kusukuma gurudumu lake.

Pia kulikuwa na mchezo wa watoto kuchukua mbwa na kwenda kuwinda. Kwao ulikuwa ni kama mchezo na ilikuwa ni kama furaha tu kwao kufanya hivyo na wala hawakuwa wanaichukulia kama ni lazima warudi na mnyama.

Ilikuwa ni kama mtoko tu. Na hata wanachokwenda kuwinda ni ndezi, sungura. Wakati mwingine wanarudi nao, wakati mwingine hawaambulii chochote, lakini wanakuwa wamechoka na kuchafuka, huku mioyo yao ikiwa imeridhika na shughuli walioifanya.

Inayofanana na hiyo ni ile ya kwenda kukamata wadudu kama panzi wa aina mbalimbali kama baranguru, au 'balale' kama walivyokuwa wakiita wenyewe.

Hiyo na mingine mingi ndiyo ilikuwa michezo ya watoto wa zamani ambayo iliwaweka 'bize' kweli kweli kiasi cha kuwa hawakutegemea akili za shuleni tu kwenye maisha yao, lakini pia kuwa na elimu ya kujitegemea kwani waliweza kufanya, kutengeneza au kuwa na ujasiri wa kufanya kitu chochote kikubwa chini ya umri wao, kiasi cha kuweza hata kuanza kuondoka kwa wazazi wao wakienda mbali kutafuta maisha na kujitegemea wenyewe wakiwa kwenye umri mdogo, bila kuwa tegemezi kwa wazazi wao kwa muda mrefu.

Tuma meseji 0716 350534