Ibada inafanyika nyumbani kwake Chato mkoani Geita kwa maombi na sala. Magufuli mhandisi na daktari msomi mbobezi wa kemia, Naibu na Waziri wa Ujenzi kwa miaka mingi, kadhalika Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Mifugo na Uvuvi na kubwa zaidi Rais wa Tanzania kuanzia 2015 hadi 2021, alitwaliwa akiwa katika awamu ya pili ya uongozi wake.
Ijumaa iliyopita, Watanzania, serikali, wana CCM, marafiki zake, wadau mbalimbali wanatoa heshima zao kwa shujaa aliyetamani kuiona Tanzania yenye maendeleo endelevu .
Shujaa aliyepigania kuwa na uchumi imara , ameondoka amewaachia Watanzania urathi (legacy) wakiendelea kuamini kuwa kwa juhudi na kufanyakazi kwa nguvu na bidii zaidi, kila kitu kinawezekana kufikiwa.
La, msingi ni jitihada, maarifa, kujitoa na wakati mwingine kuacha hofu na kuwa jasiri katika kutaka kuwa na kasi ya maendeleo, akitumia kibwagizo cha hapa kazi tu.
Kazi zake zinaonekana kuanzia kuimarisha usafiri kwa kujenga miundombinu imara, kuhimiza viongozi kujituma kuhudumia na kutatua matatizo ya watu, kujenga shule nyingi za msingi na sekondari, kuanzisha viwanda na kujitoa mhanga kuhoji mikataba, kazi za uwekezaji na kutaka rasilimali za taifa zilete maendeleo ya nchi.
Ndivyo vilikuwa vita vya Magufuli kila siku mpya inapoanza na ndoto alizokuwa anaziota na kuona dhahabu, tanzanite, almasi na wanyama wa Tanzania wanaiondoa nchi kwenye umaskini.
Katika hamu yake ya kuwaandaa Watanzania wenyeji na wageni kuona ambacho hawajakiona na kula ambacho hawajakionja, aliongeza kasi ya kufanikisha ziara za utalii.
Kusafiri kwa wepesi nje na ndani ya Tanzania ndicho , alichokifanya kwa kusimamia ununuzi wa ndege na kukamilisha ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa Dar es Salaam.
Magufuli alitamani kuona maelfu ya wasafiri wa kimataifa, wakitua Dar, kutembelea vivutia watalii na wengine wakiunganisha ndege kuelekea mataifa mbalimbali.
Alitaka watimize ndoto yao ya kuona kile ambacho hawajawahi kukiona kwa kufika Serengeti, Selous, Manyara, Mkomazi na Ngorongoro huku wakila na kunywa vyakula ambavyo hawajawahi kuvionja na kuifanya nchi kuwa moja ya mataifa barani Afrika yapendwayo na kutembelewa na wageni wengi.
Nguli huyu wa usafiri alipigania kuwapo na uwanja wa ndege wa kisasa wa Msalato International Airport mkoani Dodoma, ambao awamu ya sita inaendelea kuujenga.
Hakufanya ajizi alipambana na ujangili akiukomesha na idadi ya tembo ikaongezeka , inaelezwa na Taasisi ya Africa Wild Life Foundation kwamba tembo waliongezeka kutoka mwaka 2014 wakiwa 43,000 na kufikia ndovu 60,000 mwaka 2021.
2019, Magufuli anaagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya ‘Nyerere National Park kwenye ukanda wa juu wa pori la Selous lengo ni kuenzi mawazo na kazi kubwa ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kualinda na kuhifadhi mazingira na kuwa na utalii bora.
Katika juhudi za kulinda na kutunza wanyama adimu ambao hawapatikani popote kwingine kama nzohe, pongo na tohe, alianzisha pori la Burigi ambako wanapatikana kwa wingi.
Pori la Burigi linaanzia hifadhi ya taifa Rubondo, iliyo kwenye Ziwa Victoria kukiwa na wanyama wa aina mbalimbali.
KUKOMESHA FOLENI
Magufuli hakupenda kuona foleni barabarani . Alianza kukinai kilichokuwa kinatokea kwenye barabara za Dar es Salaam, kuanzia Ubungo hadi Chalinze.
Licha ya kuwa barabara muhimu kwa wachukuzi wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, Barabara ya Morogoro ilikera kila mtumiaji kutokana na kuwa na foleni siku zote 365 za mwaka. Lakini Tinga Tinga kama alivyokuwa anitwa kwenye mataifa jirani alimaliza tatizo hilo.
Akiharibu kwa muda mfupi kazi zote za kiuchumi na uwekezaji zilizofanyika ndani ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, Magufuli alilaumiwa kubomoa nyumba, viwanda, vitega uchumi vyote upande wa kulia na kushoto wa Barabara ya Morogoro, kuanzia Kimara hadi Kimara, akisafisha mita 241 za hifadhi ya barabara aliyodai ilivamiwa.
Ni kutoka Kimara Stop Over hadi Kibaha Maili moja na kuvunja msongamana akijenga barabara yenye njia nane ikijumuisha ya mwendo kasi ambazo zimeondoa foleni kwenye barabara ya Morogoro hasa kuanzia Mailimoja hadi Mbezi.
Wakazi wa Mbagala zote ikiwamo Rangi Tatu , maeoe ya Kilwa Road , Kurasini na ukanda wa bandarini waliokuwa wanachoshwa na foleni hakuwaacha, aliwagusa kwa kuanzisha mradi wa mabasi yaendayo haraka.
Kuanzia Mbagala hadi Kariako, Kivukoni kashi kuungana na yale yanayohudumu barabara za Morogoro na Kawawa kote wakifurahia mabasi ya mwendo kasi.
Kadhalika, ilikuwa nia yake kuufikisha mwendo kasi Tegeta Nyuki kwenye Barabara ya Bagamoyo na kufuta kilio cha foleni jijini Dar es Salaam ambacho watafiti wanasema ililigharimu jijini mabilioni ya hasara za kiuchumi na kijamii.
Mkoani Arusha wanapokumbuka kifo cha Magufuli wanafahamu kuwa anaishi wanasherehekea uwepo wa barabara ya mzunguko ya bypass ya Arusha Tengeru ambayo ni kubwa kwa Afrika Mashariki.
Kadhalika, Dodoma, Mbeya na Dar es Salaam, ni miji ambayo ilikuwa kwenye ramani za kuwa na barabara za mzunguko.
Magufuli hata kabla hajawa Rais alisikika akisema kuwa ujenzi wa barabara imara ni kufunga mlango wa umaskini.
Akisimamia Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kuonoda Umaskini (MKUKUTA), aliamini kuwa uwepo wa barabara bora utawaondoa kwenye umaskini maelfu ya Watanzania mijini na mashambani kwa kulima, kununua, kusafirisha na kuuza bidhaa za aina mbalimbali bila kukwama.
Alijipatia sifa ya kuitwa mmoja wa askari shujaa wa miavuli kutokana na kuchapa kazi heshima anayopewa na Benjamin Mkapa, Rais wa awamu ya tatu.
Ni kiongozi aliyeendeleza dhana ya kuwa na nchi inayopitika, inayosafirika wakati wote kwa kusimamia uwapo wa Tanzania iliyoungana na wananchi wake wasafiri kutoka Mtwara hadi Mara halafu Tanga mpaka Tabora kwa taksii.
AITIKISA AFRIKA
Ujenzi wa miundombinu kuanzia madaraja, makalvati, kuunganisha mikoa yote kwa lami pamoja na baadhi ya wilaya , kujenga reli ya kisasa ni mambo ambayo ulimwengu wa Afrika haukuyafumbia macho.
Ni katika mkutano wa Umoja wa Afrika unaofanyika mwaka jana, Rais wa Samia Suluhu Hassan, anapokea Tuzo ya Maendeleo ya Ujenzi wa Miundombinu, Tanzania ikiwa mshindi wa mwaka 2022 wa ‘Africa Road Builders–Babacar Ndiaye Trophy.’
Ni tuzo inayotolewa kwa viongozi wakuu barani Afrika ambao wameonyesha uthabiti wa kujenga na kuwa na maendeleo ya miundombinu ya usafirishaji kwenye nchi zao.
Moja ya kazi za kukumbukwa na ujenzi wa daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 513.5 (nusu kilometa) na barabara ya kuunganisha ya kilometa 3.8 iliyokamilika mwaka jana . Ujenzi huo umeondoa kero ya miaka kadhaa ya kuzunguka kona nyingi za korongo la mto Wami, zinazpfanana kama herufi ‘S’ zilizotesa madereva, abiria na magari kwa miongo mingi.
Rais Samia anapoipokea Tuzo ya Afrika, anakiri kuwa ni heshima ya taifa inayopatikana kutokana na kazi kubwa aliyoifanya mtangulizi wake John Magufuli, aliyeaga dunia Machi 17, 2021.
Magufuli anayetimiza miaka miwili tangu kuondoka duniani aliyaishi mafanikio na juhudi ambaozo hata sasa zinaonekana. Katika imani yake aliamini Waraka wa Wafilipi 1:21-27,kuwa ‘kwangu, kuishi ni Kristo na kufa ni faida zaidi, afurahie uzima wa milele na Kristo. Amina.










