Hapo kunatajwa vazi liitwalo ‘Batiki Mshumaa’. Hakika lilipendezesha na kupamba Siku ya Wanawake Duniani, hivi karibuni. Cha mvuto ni ushuhuda, kinamama wengi wakiwa wamejikuta wakikosa vazi hilo, ingawa walihamasika, sababu kuu ni wauza vifaa na malighafi kumaliza bidhaa zao.
Ni zao la ukubwa wa mwitikio wake, katika kupamba sikukuu hizo. Mbali na vazi hilo kupendezesha sikukuu za kitaifa, tayari linachukua sura ya kuwa rasmi, kutokana na ukweli wa mwitikio hadi namna linavyopendezesha sikukuu za kiserikali, kukawapo juhudi kubwa za kutetea ukuaji wa soko hilo.
KINACHOFANYIKA
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi Royal Progress Centre, Rose Urio, ndiye amejikita mstari wa mbele katika dai hilo la vazi na soko, ambalo linainua maradufu juhudi za matumizi ya batiki ndani na nje ya nchi.
Hadi sasa inatajwa, wameshafanikisha kwa kiasi kikubwa kutokana na uhalisia, tayari serikali imeshalikubali vazi hilo katika sikukuu za kiserikali nchini na kwa mwaka huu, sikuuu hiyo ya wanawake ndio imefungua mlango katika vazi hilo.
Rose anaiambia Nipashe kwamba, wamepambania hilo kwa kiasi kikubwa kukua kwa vazi hilo na sasa wanaishukuru serikali iliyopo madarakani, imeitikia wito, vazi batiki livaliwe kitaifa katika sikukuu hizo.
Sasa anatoa wito kwa Rais Samia, awe balozi namba moja katika vazi la batiki, alisimaie na kulitumia katika safari zake za nje ya nchi na kubeba kiasi kadhaa, anazotoa zawadi.
Anatoa mtazamo wake, kwamba mkuu wa nchi atakapofikia hatua hiyo, itakuwa na maana kubwa inayoleta tija kwa soko la batiki ya Tanzania duniani, ikiwamo kuwainua wanawake wazalishaji kiuchumi.
Pia, anafafanua kwamba, binafsi hakuona haja ya kuzalisha nguo za batiki na kuzipeleka katika soko la dunia, pale alipoenda nchini Marekani mwaka 2021.
Anafafanua kuwa, hatma hiyo inatokana na pale akagundua batiki nyingi alizoziona madukani, nembo zake zinaonyesha kutoka nchi jirani na za Tanzania zilikuwa chache.
Rai yake ni kwamba, hadi sasa umefika wakati Watazania wachangamkie fursa, kwani walitaka kuanza na soko la Agoa, lakini wamegundua pia, soko kubwa pia liko ndani ya nchi.
MWANZO WA MAFANIKIO
Kwa mujibu wa Rose, hadi kufika Julai 8, mwaka jana, walishazindua Siku ya Batiki katika Viwanja vya Maonyesho vya Sabasaba, Dar es Salaam, lengo ni kuitangaza batiki katika soko la dunia kwamba, mradi huo upo Tanzania Bara na Visiwani.
Hapo anawasilisha shukurani zake kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, kwa kuwapatia ridhaa ya kuvalisha batiki hilo la kitaifa.
Kwa mara ya kwanza katika sikukuu hiyo ya wanawake, kumetokea mafuriko ya wateja wa soko hilo, kwa kuwa waliweza kuzalisha zaidi ya nguo milioni nne na bado hazikutosha mahitaji.
“Matarajio yetu makubwa kila mwezi tuwe tunazalisha batiki zisizopungua milioni nne, ziende kwenye masoko ya kimkakati Afrika Mashariki, lenye watu milioni 283.7, soko la SADC lenye watu 379.67, soko huru la Afrika na lenye watu bilioni 1.3, soko la Agoa” alisema.
Kuelekea Miaka Miwili ya Rais Dk. Samia, Ruswe anasema wameshapata mafanikio makubwa yanayovunja rekodi, kupata upenyo wa kuvaliwa vazi hilo, huku masoko mengine yakianza kufunguka.
Anasema, mafanikio hayo yana sura kwamba batiki ilianza Tanzania tangu miaka ya 1960, lakini ushuhuda wa sasa umeweka rekodi.
Rose anaeleza hatua wanazochukua katika soko hilo la batiki, ni kwamba wameshafanya mawasilinao na wazalishaji mavazi ya kiubunifu kutoka nchi za Marekani, Uturuki na Vetenam, kuangalia namna ya kupenyeza soko lao huko, kwa kuwa maonyesho ya mavazi hufanya vizuri sana duniani kibiashara.
Rose anaiomba serikali na sekta binafsi, ziwekeze kwa kuwajengea wanawake uwezo wa kutayarisha batiki, ikiwamo kuweka mfumo mzuri wa kupunguza madalali sokoni, ili kuwawezesha wanawake wapate kipato stahiki kinachowaletea tija.
Pia, anasema serikali inapaswa kuwawezesha na kuwaridhia watumie maeneo ya viwanda yasiyotumika sasa, ili kuleta tija katika ubora wa batiki kwa kuwa soko la batiki Tanzania, bado liko chini, kutokana na changamoto ya kutumia majiko ya kuni na mkaa.
Mama huyo anasema, pale ikiridhia kutumika maeneo hayo yanayoombwa, kutawezesha kuletwa tija na batiki itatoka katika ubora stahiki, kwa kuwa watazalisha batiki kwa nishati safi, pia majiko sahihi akitaja ni LPG.
Hapo ana ufafanuzi kwamba kutumia nishati safi kutaleta tija katika soko la dunia kuliko batiki ya sasa inayopikwa kwa majiko ya kuni na mkaa.
MZALISHAJI MSHIRIKI
Anna Harold, ni mzalishaji batiki kutoka soko la batiki Mchikichini, Dar es Salaam, aliyepata nafasi ya kuzalisha batiki katika sherehe hizo zilizopita, anasema alifanikiwa kuandaa pisi 1900.
Anasema, mwaka huu kumekuwapo mafuriko ya wateja katika soko hilo, kwamba haijawahi kutokea tangu waanze, akiunga mkono ushuhuda wa awali.
Mama huyo anasema, imewezesha kuzalisha ajira nyingi za muda, kupitia sikukuu hizo kwa kuwa wanawake waliweza kujipatia kipato jumla shilingi 200 katika kusuuza na kuanika kila vazi , ikiwa ni sehemu ya maandalizi.
Anna anaiomba serikali kupitia vyuo vya kati vya ufundi, kuanzisha masomo ya ufundi ikiwamo na upishi wa batiki, kwa kuwa soko kuu la Afrika Mashariki lina idadi kubwa ya watu, kwa hiyo ili kuendeleza soko hilo ni busara kukawepo mfumo bora wa kuleta tija, pia kuwapo wazalishaji wapya,badala ya kuendelea kutegemea waliopo sasa.
UONGOZI MKOA DAR
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Rehema Madenge, anasema mwaka huu serikali inatambua mchango wa wanawake wajasiriamali na imeelekeza vazi batiki litatumika katika sherehe za kiserikali, ili kuwainua kiuchumi wanawake nchini.
Anasema, kutokana na kaulimbiu ya maadhimisho ya siku hiyo ya wanawake kitaifa ‘Ubunifu na mabadiliko ya teknolojia ni chachu ya kuleta usawa wa kijinsia’, hapo ndipo dhamira kuleta mabadiliko teknolojia jumuishi, serikali inatambua wanawake wajasiriamali wanachangia pato la taifa.
Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala na akawataka wanawake kutokukatishwa tamaa na baadhi ya wanasiasa wanaobeza kuwa vikoba na biashara ni upuuzi.