Mbinu ya kuishi bila ya msongo wa mawazo

17Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbinu ya kuishi bila ya msongo wa mawazo

KUUKABILI msongo wa mawazo kwa ufanisi ni lazima kuwa makini na kila kinachotokea ndani ya miili yetu.

Mtu akiwa na msongo wa mawazo. (PICHA NA MTANDAO).

Haya siyo mawazo ya mwandishi wa makala haya bali ni matokeo ya utafiti mpya wa ubongo yanayobainisha sababu za baadhi ya watu kuonekana kuwa na ujasiri wa kukabiliana na changamoto kadha wa kadha kuliko wengine.

Hakuna ubishi kwamba tunaishi katika nyakati ngumu na hata wasomaji wa gazeti hili wanajua vizuri. Ugumu wa maisha umejikita katika mambo mengi ikiwamo wasiwasi kuhusu hali ya dunia yetu, usalama wetu, fedha zetu na afya; mambo ambayo yanaweza kusababisha athari za kisaikolojia.

“Tunapokabiliwa na matatizo, mathalani ikiwa ni kutoa hotuba mbele ya mamia ya watu au tukitamani kupata medali ya pili ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki, tunapata mabadiliko katika mwili wetu," anasema Dk. Lori Haase, mwanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha California, San Diego; na mwandishi mkuu wa utafiti huo mpya.

“Mapigo ya moyo hupanda, pumzi na mzunguko wa damu huongezeka na kuzalisha kemikali zinazochochea msongo wa mawazo,” anasema.

Dk. Haase anasema: “Hivyo wakati miili yetu ikikabiliana na hali ya hatari au wasiwasi, majibu yetu ni kuhakikisha tunasahau haraka iwezekanavyo.”

Unaweza kujiuliza inawezekanaje? Wanasaikolojia wanakuambia kwamba ni katika hali hiyo ndipo ujasiri unaingia.
Kwa lugha ya kisayansi ni kwamba ujasiri ni uwezo wa kurudi haraka kwenye hali ya kawaida, kimwili na kihisia, baada ya kupatwa na tukio la kushtusha.

Wanasayansi na wanasaikolojia wanaeleza kuwa baadhi ya watu wana uwezo wa kukabiliana na matukio hayo kuliko wengine, lakini hawajabaini sababu za kuwapo kwa tofauti hizo.

Katika miaka ya karibuni, Dk. Haase na wataalam wenzake wameanza kudadisi na kueleza kuwa sehemu ya jibu inahusiana na uwezo wa watu kusikiliza miili yao.

Hadi kufikia hitimisho hilo, watafiti wamechunguza namna safari za mapumziko na baadhi ya kazi kama za askari zinavyojenga ujasiri unaoleta matokeo chanya kwenye afya ya mwili na hisia.

Watafiti waliwataka wanaume na wanawake kulala katika mashine ya kuchunguza ubongo wakiwa wameziba uso (face masks) na wakagusa kitufe kilichowasababisha wapumue kwa tabu hali iliyoshtua mwili na ubongo wao.

Wanasayansi walibaini mfumo wa shughuli za kawaida unaofanana katika ubongo miongoni mwa watu hao, kwani sehemu ya ubongo ilipokea ishara za kufanana kutoka mwilini, ikiwamo mabadiliko katika kiwango cha mapigo ya moyo na kupumua.

Wanasema mbali ya hilo, mtiririko wa ujumbe kutoka kwenye ubongo kwenda kwenye maeneo mbalimbali ya mwili ulifanana kwa kiasi.

Aidha, wanasema bongo za watu hao zilipokea mshtuko wa mwili, lakini hazikutilia maanani na kwamba walipata mshtuko ila hawakushtuka kupita kiasi na hivyo kurejea haraka kwenye hali ya kawaida kimwili na kiakili.

Utafiti huo mpya uliochapishwa mwezi huu kwenye jarida la Saikolojia ya Kibaolojia, watafiti walihusisha watu wazima wenye afya njema 48 na kuwataka wajibu dodoso lililohoji kiwango cha ujasiri wao kihisia na kimwili. Kulingana na alama zao, wanasayansi waliwafanyia tathmini kulingana na waliopata alama za juu, wastani au chini za ujasiri.

Kisha waliwaingiza kwenye mashine ya kuchunguza ubongo wakiwa wamevaa aina moja ya ‘mask’ za kuziba uso.

Kwenye utafiti huo, watu waliokuwa na alama za juu za ujasiri walionyesha uwezo mkubwa wa ubongo kupokea taarifa za mwili kama ilivyo kwa askari na wanariadha, ikilinganishwa na watu walioonyesha wastani mdogo wa ujasiri.

Lakini bongo za watu waliopata alama za chini za ujasiri zilikuwa kinyume kabisa kwani kadiri mask zao zilivyofunga, uwezo wa ubongo kufuatilia ishara kutoka kwenye mwili ulikuwa mdogo.

Wanasayansi wamehitimisha kwamba kwa matokeo hayo, imebainika kuwa mwitikio wa ubongo wa watu waliopata alama za chini unadhoofisha ujasiri na hivyo kufanya vigumu zaidi kwa mwili kurudi katika hali ya utulivu.

"Kwangu mimi, utafiti huu anasema kwamba ujasiri unategemea kwa kiasi kikubwa mwamko wa mwili na siyo fikra," anasema Dk. Martin Paulus, Mkurugenzi wa Taasisi ya Laureate Institute for Brain Research in Tulsa, Okla, ambaye pia ni mwandishi mwandamizi wa utafiti huo.

Anasema: “Hata watu makini kama hawawezi kusikiliza miili yao, hawawezi kurudi nyuma na kurejea haraka kutoka kwenye shida.”

Naye Dk. Haase anasema: “Kuboresha mawasiliano ya ndani ya miili yetu inaweza kuwa rahisi kwa kutumia dakika chache kila siku katika kupumua kwa umakini.”

“Baada ya muda, zoezi hili lazima litufundishe kuvuta pumzi wakati wa wasiwasi na hali ngumu ili kuondoa msongo,” anasema Dk. Haase.