Pia, Ripoti ya Polisi nchini, inaonyesha kuwapo ongezeko la asilimia 25.95 ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na kinamama, katika mwaka 2020 kulipokuwapo mikasa 7388, kutoka 5,803 ya mwaka 2015.
Ili kupambana nayo mkoani Shinyannga, Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) imekuwa ikishirikiana na Klabu ya Waan dishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) kukabili madhila hayo.
Ofisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Aisha Omary, anasema wananchi wanakosa imani pale mtuhumiwa anapokamatwa na kufikishwa kituoni na baadae anaachiwa, ilhali hawatambui haki ya kisheria ilivyo katika mkasa huo.
Anasema, watendaji wa kata wana wajibu wa kutoa mrejesho kwa wananchi kuhusu mashauri mbalimbali yanayoendelea, wananchi ili kujua yamefikia hatua gani kupitia vikao na mikutano vyao.
Pia, anawasihi wazazi na walezi kuacha tabia kukutana na kumalizana kwa kulipanana ama kwa mifugo au fedha, kwani anayeumia ni mtoto aliyefanyiwa ukatili huo na sio wao, hali kadhalika ni kosa kisheria.
Mratibu wa Ukimwi wa Halmashauri hiyo, Happynes Misaeli, anasema ni mazingira yanayoendana na kushamiri maambukizi ya virusi vya ukimwi, huku nao wakichukua hatua ya kutoa elimu, kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Rafiki-SDO.
Anataja makundi wanayoyafikia ni vijana wa umri miaka 15 hadi 24, kwamba wapo hatarini, hivyo wanapatiwa elimu ya kutumia kondomu, ujasiriamali na kuwaandaa kuwa baba na mama bora. Zaidi inafanyika katika maeneo ya mikusanyiko kama Mwakitolyo na Tinde, kunakoongoza kwa maambukizi hayo.
Lyamidati ni kati ya kata 26 za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambazo zimeshamiri matukio ya ubakaji. Hapo,Veronica Nduta, Diwani wa kata ya Lyamidati, anakiri changamoto hiyo, akifafanua hatua wanazochukua.
Anataja mwananchi akifanyiwa ukatili, wanaripoti na watuhumiwa wengi wamekuwa wakitoweka, huku muathirika akibaki na maumivu moyoni.
Anasema, mikakati waliyo nayo ni kutenga eneo la kujengwa kituo cha polisi, pia zahanati wakiandaa wodi ya kinamama na watoto, ili kuwaondolea adha wajawazito kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za kiafya.
Ofisa Mtendaji Joyce Mahina, anawashauri wananchi kuondoa woga wa kutoa taarifa kwa ofisi yake, kwani inabaki siri baina ya ofisi na mtoa taarifa, wao wakichukua hatua kuripoti polisi katika kata jirani ya Mwakitolyo, kupata msaada zaidi, huku
wakiwapatia elimu na uwezo wa kujiamini watoa taarifa.
KUTOKA KWA WANANCHI
Anita Joramu, kutoka kijijini Ihungi kwenye halmashauri hiyo, anasema hawafahamu namna sahihi ya kutoa taarifa ya ukatili wanapofanyiwa ukatili, wakibaki nayo moyoni, ndicho kinatawala kwa familia nyingi.
“Matukio ya ubakaji yanapojitokeza wakati tunajiandaa kwenda kutoa taarifa kwa watendaji wetu, tunaoga kwanza na tunapofika tunaambiwa tumeharibu ushahidi,” anasema.
Pia, anaeleza kuna wakati baba katika familia hufika hatua wameshachukua mahari ya binti tangu akiwa masomoni.
Chausiku Vumilia, anakiri hayo, akiongeza kuwa hawafahamu hata namna ya kuwasilisha ushahidi wa matukio ya ukatili kijinsia kwa vyombo vya sheria, ikwamo mahakamani, hivyo wanapotakiwa kutoa ushahidi, ama wanajificha au kutoroka, kwa sababu ya woga, hivyo anaomba kuwapo msaada kuwasimamia kisheria.
Mkazi Ramadhani Juma, anasema kukabiliana na matukio hayo ya ukatili huo, kunastahili kuendana na kupewa elimu ya ilivyo huduma za kisheria, kuanzia na kituo cha polisi.
Hangwa Anthony anasema, kukosekana kituo cha polisi pia ni sababu ya kukithiri matukio ya kikatili kwa wanawake na watoto, kwani kunakosekana kinga ya kisheria na inaishia kwa wenyeviti wa vitongoji na vijiji.
Anataja gharama, kupeleka malalamiko kwa dawati la jinsia kituo cha polisi, inatajwa usafiri wa gari ni Sh. 4,000 na pikipiki Sh.1, 000, huku vituo vingine inawagharimu kati ya Sh.4 ,000 na 30,000.
Mkazi mwingine, Dorice Lugina, anasimulia wamekuwa wakitelekezwa na waume zao baada ya kuivisha mazao shambani, kuuza, kupata fedha na kwenda kuoa wanawake wengine na wanashindwa kutoa taarifa kwa sababu vituo vya polisi wanavyotegemea viko mbali na makazi yao.
Kijiji hicho sasa kimepitisha azimio, kwa anayetaka kuoa au kuolewa ni sharti kupima virusi vya Ukimwi.
Ofisa kilimo kata katika eneo hilo, John Shilinde, anasema kila msimu wanaume baada ya mazao kukomaa, huyauza na kutelekeza familia walizokuwa nazo awali.