Atafungiwa kwa mchezo wa pili iwapo atafanya ukiukwaji wowote zaidi kati ya sasa na mwisho wa msimu ujao.
Klopp alimbwatukia Tierney kuwa ana historia mbaya na Liverpool, baada ya kuoneshwa kadi ya njano kwa kusherehekea mbele ya ofisa wa nne, John Brooks baada ya bao la ushindi la dakika ya mwisho la Diogo Jota katika mchezo dhidi ya Aston Villa, Machi.
"Tuna historia yetu na Tierney, sijui ana nini dhidi yetu," alisema Klopp akiiambia Sky Sports.
"Amesema (hakuna) matatizo lakini hiyo haiwezi kuwa kweli. Jinsi anavyonitazama, sielewi. Huku Uingereza hakuna mtu anayepaswa kufafanua hali hizi, ni ngumu sana kuelewa. Alichoniambia aliponipa kadi ya njano si sawa."
Pep Guardiola aliepuka kufungiwa kutokana na matamshi aliyotoa kuhusu mwamuzi kabla ya mechi ya dabi ya Manchester mwaka 2018, lakini Klopp hayuko peke yake linapokuja suala la makocha wa Ligi Kuu England kufungiwa kwa mambo wanayosemwa kuhusu waamuzi.
5. Jose Mourinho - mchezo 1 (2016)
Jose Mourinho alifungiwa mchezo mmoja Novemba 2016 wakati wa msimu wake wa kwanza Manchester United, baada ya kumkabili Mark Clattenburg wakati wa mapumziko katika suluhu dhidi ya Burnley. Wakati huohuo, alipigwa faini ya pauni 50,000 kwa maoni aliyoyatoa kuhusu Anthony Taylor kabla ya pambano kati ya timu yake ya United na Liverpool.
Katika matukio mengine, Mourinho alipigwa faini ya pauni 10,000 wakati akiwa kocha wa Chelsea mwaka 2014 kwa maoni yake kuhusu Mike Dean baada ya kufungwa na Sunderland - msaidizi wake, Rui Faria aliishia kufungiwa michezo sita kwa kugombana na mwamuzi uwanjani baada ya mchezo huo huo.
Mwaka 2015, alitozwa faini ya pauni 50,000 na kufungiwa mchezo mmoja, baada ya kupendekeza kwamba Robert Madley 'aliogopa' kuipa Chelsea penalti katika kipigo cha nyumbani dhidi ya Southampton.
4. Harry Redknapp - michezo 2 (2003)
Katika kipindi chake kama kocha wa Portsmouth, Harry Redknapp alifungiwa mechi mbili baada ya kumkosoa mwamuzi Andy D'Urso na kuwasilisha malalamiko yake kwa ofisa wa nne, Lee Mason.
"Nilitilia shaka uchezeshaji wa mwamuzi, ambao nilifikiri haukufaa," alisema Redknapp. "Sikupiga kelele au kumtusi mwamuzi, nilitoa maoni kwa ofisa wa nne. Asilimia 99 ya maofisa wa nne wangesema 'Mimi nakubaliana na wewe' au 'Keti chini, Harry.' Nadhani alikuwa kijana ambaye labda alikuwa akijaribu kujipatia jina."
Mwaka 2010 akiwa Tottenham Hotspur, Redknapp alifanikiwa kukwepa kufungiwa, baada ya kutishia kuwa hatafanya tena mahojiano baada ya mechi, kwa maoni yaliyotolewa na mwamuzi, Mark Clattenberg.
3. Mauricio Pochettino - michezo 2 (2019)
Mike Dean alisema kuhusu kocha wa Tottenham Hotspur wa wakati huo, Mauricio Pochettino katika ripoti ya baada ya mechi mwaka 2019: "Hataacha kusema 'unajua ulivyo, unajua ulivyo'. Nilimwomba anieleze na akarudia 'unajua. wewe ni nini."
Mchezo huo ulikuwa wa kichapo cha Tottenham dhidi ya Burnley na Pochettino alijibu kwa hasira kwa kile alichoamini kuwa uamuzi usio sahihi wa kutoa kona ambayo ndio iliwafanya Burnley wapate ushindi.
2. Arsene Wenger - michezo 3 (2018)
"Wewe sio muungwana...wewe ni aibu," ni maneno ambayo yalitoka kinywani mwa Arsene Wenger kuelekea kwa mwamuzi Mike Dean baada ya mchezo wa Arsenal dhidi ya West Brom katika mkesha wa mwaka mpya 2017.
Mfaransa huyo alikasirishwa sana na mkwaju wa penalti wa dakika za lala salama uliotolewa kwa West Brom na baadaye aliingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo ili kukabiliana na Dean.
Wenger alikosa mechi tatu mwanzoni mwa 2018 na alipigwa pia faini ya kulipa pauni 40,000.
1. Sir Alex Ferguson - michezo 5 (2011)
Kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson aliishia kufungiwa michezo mitano kufuatia kumkosoa mwamuzi, Martin Atkinson baada ya kufungwa na Chelsea mwaka 2011.
"Unataka mwamuzi wa haki, au mwamuzi mwenye nguvu, hatukupata hilo. Lazima niseme, nilipoona mwamuzi ni nani niliogopa. Niliogopa sana," alisema Ferguson wakati huo na kusababisha FA kumfungia.
Raia huyo wa Scotland alifungiwa mechi tatu kwa matamshi hayo. Lakini sababu iliyomfanya aongezewe mechi mbili zaidi ni kwa sababu FA ilimpiga marufuku michezo miwili aliyosimamishwa tangu mwaka 2009 baada ya kuhoji hadharani utimamu wa mwili wa mwamuzi, Alan Wiley.










