Maendeleo kutoka miaka 10 ya Uhuru,

24Dec 2022
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Maendeleo kutoka miaka 10 ya Uhuru,
  • hadi ilikogota leo kwenye miaka 61 * Pantoni Rufiji hadi daraja, mabehewa ya 'uswazi', hadi digitali...

NAKUMBUKA mzee wetu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, alipokuwa kwenye uongozi wa Taifa, alikuwa mtu wa wosia sana na staili yake alitumia ama lugha ya kiswahili ambayo unaweza kusema ni sebuleni kwake, au anatumia misemo ambayo ukiunganisha ujumbe unajitosheleza hauachi hata pengo.

1.Treni: Abiria wa treni yenye mabehewa ya zamani, wakisubiri kupanda. PICHA ZOTE: MAKTABA.

 

Alikwishatutamkia 'kila zama na azma zake'. Nani anaweza kubisha hilo? Hebu jikumbushe wewe, mzee wa leo mkaka ambaye utotoni kwako kidali pooh! ndiyo ilikuwa mpango mzima, huku dada yako ambaye leo ameingia kwenye zama za ubibi, humwambii kitu kwa 'babua ea.' Thubutu, leo hii umwambie mtoto wa leo akacheze michezo hiyo, utazua gumzo na kupondwa mpaka basi na kali zaidi wengine watashangaa na kukuuliza 'ndiyo nini hiyo?'

Vivyo hivyo, serikalini kwa awamu na muda husika, huwa kuna mahitaji yake, hasa ya maendeleo na aina fulani ya maendeleo hayo huibuka kipindi fulani yuko kwenye kiti; yaleyale ya kila zama na azma zake.

Naam! Lazima nikiri katika safari za awamu hizo mbalimbali, tunapoeleza kukomboa sekta ya usafiri na miundombinu, mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, zama na azma zake, ziliangukia hapo, sambamba na afya akizindua Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM). Nikunong'oneze kidogo, ile barabara iliyofungua ukanda wa Tabora hadi Kigoma, mabasi yanakatiza tu leo hii, akiipigania kwa nguvu zote.

Kutoka Masasi hadi Tunduru, kutokezea Namtumbo Ruvuma ni kichekesho kidogo mabasi leo yanakatiza kilaini, thubutu ungekuja na msamiati huo siku zile anaingia madarakani. Ushahidi ninao!

Nenda pale Temeke Sudan, Dar es Salaam, mabasi kibao kwenda Tunduru hadi Songea kupitia njia hiyo ya Masasi. Jamani! Inanirudisha nyuma tena zama zile, mzee Mwinyi akahamisha barabara ya mlima Lukumburu, sasa leo hii waendao Songea kupitia Njombe, mambo safi tu. Maana yake nini? Kuna kazi inafanyika. Tusiwe wataalamu wa kubeza tu.

Hebu niwape mchapo kidogo kwa kionjo cha safari ya Kusini zama hizo. Ukitoka Dar es Salaam, na ukafika kwenye kivuko cha Mto Rufiji, uvukaji wake unapata salaam kamili, mara pantoni mbovu, mara hiki na kile, inakula siku mbili. Pantoni hiyohiyo Feri Dar imeshatuachia majonzi, tena huduma zake mwisho saa sita usiku.

Tumshukuru mzee Benjamin William Mkapa, aliliona hilo, tena analijua fika njia ya nyumbani kwao pale Ikwiriri Rufiji, akajenga daraja linalojitosheleza, sijui wale wazaliwa wa miaka ya 1990 wanalijua hilo?

Unatoka hapo, unasonga hadi Nangurukulu, Kilwa kwa shida, ukianza tu uelekeo wa Lindi na mvua ikinyesha, imekula kwako, lazima mnase kwenye matope, kigezo na masharti kutoka hapo, ni jua kuwaka na tope kukauka. Wanaoishi vijiji jirani kama Mavuji, mkoani Lindi wanajua vizuri kilichoendelea hapo, leo hii ikibaki kuwa hadithi.

Naam, simulizi ni ile ile ndiyo umefika Masasi na kulala, asubuhi unaanza na mabasi kuelekea Tunduru, shughuli nzito kweli kweli. Maana nakumbuka kuna siku tulianza saa nne asubuhi, stendi ya Masasi nilikolala baada ya safari kutwa nzima kutoka Dar es Salaam, wakati leo hii anayetoka jiji hilo asubuhi anawahi kuona mechi ya soka alasiri mwanzo hadi mwisho, basi tukasonga huku mvua inanyesha kidogo yaliyotukuta ni mazito hasa, hadi kufika Tunduru stendi ilikuwa siku iliyofuata alfajiri.

Nilidiriki kukufuru kwa kujiuliza, ni Tanzania hii hii au kwingine? Maana nilipoangaza stendi zima yamejaa magari aina ya Land  Rover tena aina ya 109. Wazaliwa wa 1990 mnayajua? Shughuli ikawa pevu vilevile wakati wa kuondoka, niliposema safari hiyo nipitie Tunduru hadi Namtumbo Songea, nako ikawa kutwa nzima, tena gari aina ya 'pick up', hadi nakuja kuiona Namtumbo Ruvuma, nguo zote zimejaa udongo mwekundu mithili ndiyo rangi yake ya asili.

Lakini maendeleo yakaja, Rais Kikwete, mnano Aprili 2006, nikamsikia ziarani Tunduru akiahidi kukomboa barabara yao kwa mradi maalum, kwani ilipita miaka mingi? Eti leo hii, basi linatoka Temeke Sudan mapema asubuhi, saa 9:00 alasiri linakatiza Masasi, usiku watu waangalia TV mjini Songea. Mbona raha!

Zama hizo hizo, waendao mkoa wa Mara kutoka Dar, sharti wakatize Arusha, kupitia nchini Kenya na alfajiri siku inayofuata wanaibukia Sirari Tarime kule kwa jamaa zetu, mchana wapo mjini Musoma. Waendao Bukoba nao kutoka Dar, njia hiyo hiyo wanapita Kenya hadi mpaka wa kuingia Uganda kuvuka hadi mpaka wa Mutukula kuja kuitafuta Bukoba mjini, kama siyo siku tatu ni nini hapo? We uliyopo Dar, ukifikiria kwenda nyumbani Bukoba, unawaza nauli, safari siku kadhaa na pasipoti juu.

Turejee kwenye safari za mabinamu zetu wale wa treni kwenda kuisaka Kigoma, Mwanza, Tabora na Mpanda. La kwanza kabisa, tenga siku mbili hadi tatu upaone uendako.

Sasa mabehewa yenyewe, siyo haya mnayoyajua nyinyi au kuyaona kwenye mitandao, labda kwa mbali ni kama yale yanayotumika daladala Dar es Salaam, au mabinamu zangu wanaosonga kwenda mwisho wa reli. Nikumegee kidogo, maana huwa sichoki kusimulia kipengele hiki kinanikumbusha mbali kweli kweli! Mpaka tiketi ipatikane abiria keshasota wiki mbili  stesheni. Ukiingia kwenye mabahewa ya daraja la tatu unakutana na siti ambazo hazina sponji, feni na hata baadhi ya madirisha hayafungi.

Ukikuta juu kuna feni hilo litakuwa limeharibika. Sijajua kama yaliyokuwa yakiharibika ndiyo yanahamishwa daraja la tatu au vipi, lakini msamiati wa feni tu haukuwapo.Tofauti kubwa wa wakati ule wa daraja la kwanza la pili na la tatu ilikuwa ni idadi tu ya watu chumbani. La kwanza kulikuwa na wachache ambao wana uhuru wa kukaa bila bughudha, utaratibu wa kulala; la pili kukulikuwa na watu wengi kidogo kama sita hivi, angalau wakikaa kwa utulivu. Shughuli ilikuwa huko daraja la tatu. Kwanza kulikuwa na mabehawa machache, hivyo abiria walikuwa wengi kiasi kwamba wengine siti hazikutosha, wakakalia mizigo yao, wengine chini ya sakafu, wapo waliokaa mpaka vyooni.

Kutokana na nyomi hiyo, wizi nao ulikuwa mkubwa wa mizigo, pia ilikuwa ngumu na jopo la watu kujishauri kwenda chooni hasa kinamama. Kusema kweli hadhi ya mabehewa na mazingira yalikuwa magumu, sijui enyi wa zama hizo mnajua?

Nikifikiria hapo, ndipo huwa napanda mashetani, mtu anapokosa mshipa wa aibu eti haoni maendeleo wala maboresho yoyote kwenye barabara, treni hata usafiri wa majini. Jamani, tema mate chini!  Mtu anaibuka waziwazi kwamba haoni tofauti kati ya karabai na taa ya umeme, au simu ya kiswaswadu na ya kupangusa kidole. Jamani, haya makubwa, mbona madogo yana nafuu!