Anakizungumza na Nipashe, hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, anaeleza wazi na kutaka kuacha somo kwenye jamii kwamba mtoto wa kike anahitaji kulindwa na familia, jamii na taifa.
Akieleza yaliyomfika kwa ujasiri anatoa hadithi ya maisha yake hatua kwa hatua, akisema maisha yake yanajaa juhudi za kuhamasisha mabadiliko na kwamba ni ‘young reporter’, mtoa taarifa na mwanaharakati kutoka Mwanza, akifanya kazi na Shirika la Kiota Women's Health and Development (KIWOHEDE).
Debora Timothy, aliyezaliwa mwaka 2000 mkoani Mwanza, miaka saba baadaye mama yake mzazi alifariki dunia. Malezi yake yakahamishiwa kwa bibi mzaa baba yake, ingawa hadi anafikia umri huo, hakuwahi kumfahamu baba yake.
“Nimelelewa na bibi peke yake, simjui baba yangu, nakumbuka siku moja nilisikia ndugu zake wakipiga simu, wakimwambia wewe mke wako kafariki, unakuja lini. Sikujua alichowajibu, ila nilikuwa nawaona ndugu zake baba mdogo na wengine wakija kwa bibi,” anasema Debora.
Alianza shule, ingawa baada ya miaka michache, bibi yake aliyekuwa anamlea alifariki dunia akisimulia kuwa alipenda kusali na kila alipokwenda kanisani kwa siku za ibada na nyinginezo aliongozana naye.
“Nafikiri kadri siku zilivyokuwa zinakwenda aliibaini siku zake za kuishi zinapungua, alikuwa anamwomba mchungaji wake kuwa iwapo atakufa anichukue, anilee,” anakumbuka Debora.
Anakumbuka kuwa tangu bibi alipowasilisha ombi hilo kwa mchungaji haukupita mwezi akafariki. Hata hili jina la Timothy, si la baba yake ni la mchungaji, ambaye alichukua majukumu ya baba mlezi, kumsomesha hadi hapa alipo akikaribia miaka 23.
Debora anasema baada ya bibi yake kufariki, kikao cha ndugu kikakaa: “Kilipofanyika kikaamua kila mtu achukue familia yake nikachukuliwa na baba mdogo, nikawa nazunguka kwa jamaa zangu, nakaa miezi michache kwa kila ndugu.
Anasimulia kuwa baba yake mkubwa alimpokea, moyoni akajua huyu atakuwa mtu sahihi lakini naye baada ya mwezi akamtafutia kazi za ndani licha ya kwamba wakati huo ni mdogo bado lakini pesa za mshahara alizokuwa analipwa akawa anazichukua.
“Akaja mwajiri wangu nilipokuwa nafanyakazi kwake, akasema jiandae unarudi kwenu, akanipa hela na nauli nafika tu kwa dada akaniambia nina habari njema kwako kuwa unaolewa, licha ya kwamba nilikuwa na miaka 14. Na huyo mchumba niliambiwa alikuwa ni mtu mzima. Nikamwambia siwezi kabisa kufanya hivi, wakanishauri lakini nikakataa kuolewa.”
Anaongeza kuwa baba mkubwa alimwadhibu na usiku huo aliondoka na kutembea usiku kucha hadi akampata mchungaji akamtetea na ndugu wakawa hawamtaki tena kumsikia.
“Mchungaji akanichukua na kunilea mpaka sasa na nikawa nawaza nitapata wapi muda na mimi nije nitoe au nipaze sauti kwa mabinti wenzangu, ili wasaidiwe, nikawa napata semina nafundisha kitu kilichonipata nikiwa na ukweli ndani ya moyo kwa sababu nimepitia changamoto hiyo.”
Aidha, anasema tangu darasa la tatu anaishi kwa mchungaji na alipomaliza la saba, alianza masomo ya QT hadi kidato cha nne na kushiriki mafunzo ya kompyuta na sasa anafanya kazi kwenye kituo cha kulea watoto ‘day care’ iliyoanzishwa na mchungaji.
ALIPO LEO
Debora anasema mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia ulianza mwaka 2009 ukiwa na mabinti 30 wakifanya kazi kwenye kata nne na kwamba wanatoa elimu kwenye shule, zahanati majumbani na sehemu zenye mikusanyiko ya watu mbalimbali kwenye kata za Buzuruga, Kisesa, Buhongwa na Mhandu.
“Mradi huu unapambana kutokomeza rushwa ya ngono na kimtandao Mwanza pia tunatoa elimu na kufanya kazi kwa vitengo mfano kwa kata ya Buzuruga wanafanya siku yao na kata zingine pia vivyo hivyo,” anasema Debora.
“Kikubwa kazi ifanyike kwa wakati, tuna vitu vingi ambavyo tunavipeleka katika jamii na kupambana navyo usiku na mchana hususani kwa wale waandishi wadogo mmoja wapo ni mimi na hapo wapo mabingwa na sisi wadogo.”
CHANGAMOTO
Ukatili kwa watoto hasa kubakwa ni changamoto anazozitaja, akitoa mfano dereva wa bodaboda katika kata mojawapo alimnajisi mtoto aliyekuwa akienda shuleni mwenye miaka 10.
Anaeleza kuwa dereva huyo alimwambia binti mwanafunzi huyo anampeleka shuleni lakini alikataa lakini bodaboda akatumia mbinu nyingi, akamwambia kitu kilichomvuta mtoto akakubali, na huo ukawa mwanzo wa kunajisiwa kwa mtoto huyo mwenye miaka 10 mwanafunzi wa darasa la nne.
Baada ya kupakiwa kwenye pikipiki hakupelekwa shuleni ila kwenye jengo ambalo halijakamilika kamfanyia ukatili na kelele za binti huyo zikamshtua mpitanjia aliyekwenda moja kwa moja kuangalia ndani ya jumba na kumnasa bodaboda akitenda ukatili na kufanikisha kumkamata na kesi ikafikishwa kwao na kuna baadhi ya wanaharakati wanatoa elimu kuhusu ukatili.
Debora, anaeleza kuwa kesi imefika mahakamani lakini wakaanza kupigwa tarehe na changamoto ikawa baba mtoto hataki kesi ifike mbali na wakati huo, mama yeye anasema lazima haki ikitendeke na kwamba hofu yao baba amepokea kitu kidogo kutoka kwa mshtakiwa.
“Mama akahakikisha kesi inasonga mbele na sisi tukasimama upande wa mama na mashtaka yanasonga mbele ikaenda na kupangiwa tarehe na mtu wa kundi letu akafika mahakamani na baba akikazana kesi iishe na tukafika mbali, huku chini kabisa ushirikiano ukawa unapotea.”
Anatoa ushauri kwa wazazi akisema wakumbuke kuwapa fursa wasichana, kielimu na kuonyesha vipaji vyao, badala ya kufikiria ndoa ni muhimu katika umri mdogo ili wasichane wasiwe wahanga wa mimba za utotoni.










