Kutana na jitu lishibalo, Power Mabula

01Apr 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kutana na jitu lishibalo, Power Mabula

UNAFUNGUA gazeti, unakutana na picha ya mtu mmoja mrefu, aliyejengeka vema na kujaa misuli mikononi na kifuani. Mtu huyo ana nywele nyingi zenye rasta mbili ndefu, kiunoni hadi kwenye mapaja amevaa kitu mfano wa ngozi, akijifunga mithili ya msuli mfupi mgumu na kuacha eneo kubwa la mwili wake wazi.

Halafu unakutana na maandishi ya 'Kutana na jitu lishibalo Power Mabula.'

Lilikuwa ni tangazo la mbabe huyo likionyesha ni wapi siku hiyo atafanya maonyesho yake. Huyu ndiye Power Mabula ambaye hakuna mtoto, mzima, au kijana wa kuanzia miaka ya mwanzoni mwa 1980 hadi mwanzoni mwa 1990 ambaye hamfahamu.

Alikuwa maarufu sana kwa michezo ya kutumia nguvu. Baadhi walimuona laivu akifanya maonyesho hayo, akizunguka Tanzania nzima. Wengine walimsoma na kuona picha zake kwenye magazeti na wengine wakasimuliwa na waliomuona.

Alikuwa na uwezo wa kuizua gari aina ya Land Rover lisiondoke, akitumia kamba kubwa ya katani au mnyororo kuizuia. Alikuwa pia ana uwezo wa kuzuia magari mawili aina ya na 404 Peugeot au 505 wakati huo yasiondoke kwa wakati mmoja, mmoja ilifungwa upande huu na lingine upande mwingine, yeye akiwa katikati. Wakati mwingine aliweza kulivuta gari kwa kamba akitumia meno.

Power Mabula pia, alikuwa na uwezo wa kuizuia pikipiki ishindwe kuondoka kwa kutumia nywele zake. Akifunga kamba ilifungwa kwenye pikipiki kwenye rasta zake, huku mwendashaji akijitahidi kutia gia na kuondoka, lakini wapi.

Jitu hilo, pamoja na michezo mingi, ikiwemo kubeba mifuko kadhaa ya simenti kwa kutumia meno, alikuwa na uwezo  wa kupitisha gari kifuani kwake, bila kupata madhara yoyote.

Usisahau pia na kuvunjiwa jiwe kubwa kama yale yanayopatikana Kunduchi kifuani kwa kutumia nyundo. Aliweza pia kunyanyua matofali kadhaa makubwa yaliyofungwa kwa kamba, akitumia meno.

Ilikuwa ni kitu cha hatari kukiona, lakini ni kama watu walikuwa hawaamini macho yao, lakini ni kweli mwamba huyo alikuwa anafanya kwa malipo madogo tu wakati huo, kwani hata wanafunzi walikuwa na uwezo wa kwenda kulipa na kuangalia michezo hiyo.

Wakati mwingine aliweza kufika hadi mashuleni na kufanya michezo yake hiyo.

Huyu ndiye aliyekuwa mchezaji wa kutumia nguvu maarufu zaidi nchini Tanzania wakati huo.

Baadaye walikuja wengine, lakini hawakuweza kumfikia mwamba huyu, kwa kile alichokuwa akifanya kwenye maonyesho yake na hata umaarufu.

Baadaye kukaja michezo ya kupigana, maarufu kama mieleka. Power Mabula yeye hakujishughulisha kabisa na michezo hiyo. Yeye aliendelea na michezo yake ya nguvu tu ambayo baadaye ilianza kushuka chati, michezo ya mieleka  nafasi yake.

Ikaanza kutoa wanamieleka wazuri na waliotokea kuwa maarufu nchini Tanzania wanaokumbukwa mpaka sasa.

Kwanza walitaka kupigana, matangazo yanaanza kutoka kwenye magazeti. Kunakuwa na picha zao, halafu kila mmoja anampa 'mkwara' mwenzake.

Yale maneno wanayotishana ndiyo yanayovuta mashabiki wengi kujazana kwenye kumbi mbalimbali kushuhudia mapambano yao.

"Njoo na jeneza kabisa, hautorudi nyumbani ukiwa hai". Mwinngine naye anajibu "Leo nitakutwanga hadi ndugu zako wakuulize, umegongwa na treni au umepata ajali ya ndege kuanguka na wewe ukiwemo?"

Haya yalikuwa ni baadhi ya maneno ambayo mashabiki na wasomaji walikuwa yakiyapenda sana kuyasoma kwenye gazeti kabla ya mapambano.

Kuna mtu aliniambia siku hizi michezo hiyo haipo kwa sababu kila mtu anataka kujifanya 'sharobaro.

Akasema, hata wale wachache wanaokwenda 'gym' wanafanya hivyo ili watishe na kupiga watu mitaani, wakae milangoni kwenye kumbi ya starehe au kwenye vituo mbalimbali vya mabasi kwa ajili ya kukatia watu tiketi.

Baadhi ya wanamieleka maarufu waliopata kutokea nchini ni Power Vuru Mroma, Power Bukuku 'Sumu ya Mamba', Power Savimbi, Power Tx Chaka, Power Banardo 'Tai Kichaa', Power Ngeta 'Super Kibonge', Power Iranda, Power Mwanakulya.

Wengine ni Power Sangandele, Power Nyati, Power Mwanza, Power Nassor, Power Liston Dudu na Power Masai ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa michezo hii ya mieleka nchini.

Mmoja wa wanyanyua vitu vizito ambaye ameshastaafu na hakutaka jina lake lichapishwe, alisema  hakuna ushirikina wowote kwenye mchezo huo wa kutumia nguvu isipokuwa ni sayansi ya akili na nguvu ndiyo inayosababisha waonekane wao ni watu tofauti.

Anasema, ndiyo maana hakuna aliyesikia 'power' yoyote anapitisha lori kifuani kwake, mara zote ni magari ya kawaida kama vile Land Rover na magari mengine madogo ambayo yanaendana na uzito wa mhusika.

Kuhusu chakula alisema kulikuwa na uvumi kuwa wanakula chakula kingi zaidi kama vile mbuzi mzima peke yao na kilo tano za ugali, kitu ambacho si kweli.

"Huo ni uroho. Power anakula chakula cha kawaida ambacho wengine wanakula, ila anashauriwa ale nyama kwa wingi, mboga za majani, mahagare, japo atakula kwa kipimo cha juu zaidi kwa sababu anafanya kazi za nguvu na mazoezi magumu, lakini si kwa kiwango kinachozungumziwa mtaani. Maharage na mboga za majani zinajenga na kulinda mwili na hiyo ndiyo inashauriwa zaidi," alisema Power huyo ambaye  kwa sasa ni mwanajeshi Mstaafu. Unafahamu nini kuhusu watu hawa wa kazi?

 

Tuma meseji 0716 350534