Kumbe kifuu ndiyo mbadala zebaki migodi ya dhahabu

04Apr 2023
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kumbe kifuu ndiyo mbadala zebaki migodi ya dhahabu
  • Ni dawa kusafisha madini,maji taka, mbunifu ataka mil 36 kumaliza shida

NI tunda lenye mamia ya faida, ukianza na kulitafuna kama chakula, ni kiungo hunogesha vyakula, machicha kulisha mifugo, ni kipodozi kwenye ngozi na nywele, pia huchanganywa na viambato vingine kutengeneza dawa.

Kabon au mkaa unaotengenezwa na vifuu unaosafisha dhahabu. PICHA: MTANDAO

Makumbi yanasukwa kupata kamba, makuti huezeka makazi na maeneo ya burudani, huku vifuu vikibadilishwa kuwa urembo na mapambo, mti wake ni mbao na hata kuni pia, hiyo ndiyo Nazi.

Ukikiangalia kifuu pekee kuna matumizi yenye faida tele kama kutengeneza vyombo mfano upawa, vijiko na bakuli, vyungu vya kupandia maua yote hayo hupendezesha nyumba na kuongeza kipato kama bidhaa zikiuzwa.

Mtafiti na mbunifu wa teknolojia ya kuzalisha hewa ukaa au kabon, Tiberius Mario, anasema kifuu ni fursa kubwa ya kiuchumi akitaja, kutengeneza kabon inayotumika kuchenjulia (kusafisha) madini na maji.

Akizungumza kwenye semina ya wanahabari inayoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Jijini Dar es Salaam, Mario anaeleza namna anavyotumia vifuu kubuni biashara inayomwingizia kipato, anayoifanya pia kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa vile vifuu vinaweza kuwa mazalia ya mbu wanaoleta malaria.

“Nimebobea kutengeneza kabon au mkaa unaotumika kuchenjua dhahabu kusafisha maji taka, ninabadilisha kifuu cha nazi kwenda kwenye kabon ambayo kwenye migodi yote Tanzania hauwezi kupata dhahabu bila ya kuwa na gesi hii baada ya kusafishwa dhahabu lazima ipitishwe kwenye kaboni ili dhahabu zitoke kwenye udongo,”

Anasema hakuna kiwanda cha kuzalisha mkaa huo na kwamba zinazotumika zinatoka nje akiongeza kuwa mikoa ya pwani na kusini kuna nazi nyingi zaidi ya tani 350,000 kwa mwaka na huzalisha vifuu vingi.

Baada ya kuviona vinazagaa kwenye majalala na havina kazi, anaibua fursa ya kutengeneza kabon na kwamba alianza biashara hiyo kwa kukusanya vifuu mwenyewe katika maeneo mbalimbali.

“Nilifanya utafiti wa kuzalisha, kidogo sasa nazalisha kwa wastani nilishapeleka kwenye baadhi ya migodi na viwanda vya maji, Inatumika kusafisha maji kwa kupunguza chlorine kwenye maji na kuondoa harufu,” anafafanua

“Indonesia inaongoza kwa kuzalisha nazi, pia  India na Tanzania ni namba 16 ambako inazalisha tani 382,164 kwa mwaka kiasi ambacho kinaweza kuzalisha vifuu vingi. Kwa kuangalia wingi huo naona fursa kubwa ya kutimiza ubunifu na kufikia malengo ya kumiliki kiwanda.” Anasema Mario.

Mtafiti huyo anasema takribani tani 1,500 za mkaa inayotumika nchini huagizwa nje ya zikigharimu dola Milioni 6.7 karibu Shilingi bilioni 16.1 na kwamba kabon hiyo inaweza kupimwa katika maabara na utendaji wake ni asilimia 98 katika madini na maji pia.

 “Nilipeleka Mbeya, Shelui na STAMICO na nilifikisha sampuli Tume ya Madini, matokeo yaliyotoka ni mazuri imekamata dhahabu kwa kiwango kikubwa

Pia ninaweza kuirudisha tena kwenye mfumo kabon ambayo inatumika kwa sababu ikitumika haitakiwi kutupwa ila zinahifadhiwa ili kuondoa mlundikano hivyo narudisha kwa kurejeleza”.

 

VIKWAZO

Anataja mtaji na kwamba anachozalisha ni kilo 100, huku kiwango cha uhitaji kikiwa kikubwa zaidi, anatumia makaa ya mawe kama chanzo cha joto na kuni pia, kitaalamu anahitaji joto zaidi ya nyuzi 300,000 lakini kuni zinatoa joto la nyuzi 4,000 kwa kilo moja ili kupata nyuzi 300,000 anatumia kuni nyingi na muda mrefu.

“Nikipata Diesel Burn, joto lake ni kubwa ikilinganishwa na kuni na kifaa kinachotumika kutengeneza na kutoa bidhaa ninayotoa mimi ifike hata asilimia 90 sasa ni asilimi 50 nikiwezeshwa ninaweza kuchukua vifuu vyote na kutengeneza kabon na hatutaagiza nje nahitaji Shilingi Milioni 36,”anaeleza.

Anasema mfuko wa Kabon wa kilo 25, huuzwa Shilingi 250,000 hadi 400,000 inategemeana na nchi inakotoka ila kwa China wanauza kati ya Sh 250,000 na 280,000 na Amerika ni Sh 400,000 lakini rejareja kilo moja ni 20,000 hadi 25,000.” Anasema Mario.

“Ni kitu cha gharama inaweza kuhitaji hata kilo 500 lakini uwezo wangu ni mdogo nikipata mtaji nitafanya vizuri, sio Nazi peke yake hata Mchikichi naweza kuutumia,” anasema mbunifu huyo.

Mratibu wa Mafunzo ya Uandishi wa Habari za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka COSTECH, Deusdedith Leoanaed, anasema lengo la kuwakutanisha wanahabari na watafiti ni kupata ongezeko la uhasilishaji wa teknolojia kati ya watafiti na jamii kuwajengea uwezo wanahabari ili waweze kuandika taarifa hizo kama ilivyo katika maeneo mengine ikiwamo siasa na michezo.

AJIRA MADINI

Takwimu zinaonyesha kuwa sekta ya wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini inatoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu milioni 1.2 na kwamba ajira zisizo za moja kwa moja zinawahusu watu milioni 7.2 ikiwa ni sawa na asilimia 13 ya idadi ya Watanzania.

Tathmini hiyo inaonyesha kuwa wachimbaji wadogo wa dhahabu hutumia tani 13.2 na 24.4 za zebaki kwa mwaka kusafisha madini hayo na kwamba kemikali hiyo ni sumu na kitisho kwa afya na mazingira.

Shirika la Afya Duniani (WHO),linaeleza kuwa ukitumiwa bila kuzingatia utaalamu huharibu ubongo na mfumo wa mishipa ya fahamu, figo, husababisha watoto wenye ulemavu, kupoteza kumbukumbu ikiwamo kushindwa kupumua.

Mbadala wa kemikali hiyo ni karbon kwa sababu ni salama zaidi ikilinganishwa na hiyo zebaki ambayo inaingizwa nchini kwa kificho huku watumiaji wakubwa ambao ni wachimbaji wadogo wakiiitumia bila kufuata taratibu za ulinzi wa afya na mazingira.

Kwenye Mpangokazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu kwa mwaka 2020-2025 ambao umeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, inaelezwa kuwa tani 24 za kemikali hatari ya zebaki hutumika kwa mwaka katika shughuli za uchenjuaji wa dhahabu unaofanywa na wachimbaji wadogo.

Mpango Kazi huo, umekuja baada ya Jumuiya ya Kimataifa wa mwaka 2013 kupitisha Mkataba wa Minamata, wenye madhumuni ya kulinda afya ya binadamu dhidi ya madhara ya uchafuzi wa mazingira unaotokana na zebaki, ambao Tanzania iliusaini mwaka 2020.