Klabu zilizotoka kusaka 'ubani' msimu 2023/24

25Jul 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Klabu zilizotoka kusaka 'ubani' msimu 2023/24

KIPINDI hiki cha maandalizi ya msimu mpya wa mashindano, kila klabu ya Ligi Kuu imekuwa na mipango yake.

"Pre season' hii tumeshuhudia timu nyingi zikiamua kuondoka sehemu ambayo zimezoea kwenda kuweka kambi mbali na yalipo makao makuu yao, ingawa zipo zilizoamua kuendelea kukaa hapo hapo kutokana na mipango yao.

Viongozi kadhaa walipohojiwa sababu za kwenda kuweka kambi mbali, walisema ni kuwafanya wachezaji wawe watulivu, kubadilisha mandhari na kutosumbuliwa na ndugu na jamaa kwa shida ambazo wakati mwingine hazihitaji hata mtu kutoka kambini kwenda nyumbani. Wengine wakasema wanatafuta maeneo yenye vifaa bora, hali ya hewa, viwanja na hata kupata mechi bora za kirafiki.

Katika makala haya tumekusanya taarifa za vikosi mbalimbali ambavyo vimeamua kwenda mbali na kwao kwa ajili ya maandalizi ya msimu unajao...

 

Simba - Uturuki

Ilikuwa ni Julai 10 wakati wachezaji wa Simba, benchi la ufundi na baadhi ya viongozi walipoondoka nchini kwenda Ankara, Uturuki kwa ajili ya kambi ya siku 21.

Ingawa walioondoka awali walikuwa ni 17 tu, lakini mpaka kufikia jana karibuni wachezaji wote walikuwa wameshawasili kambini isipokuwa Luis Miquissone.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amebainisha kuwa leo hii kikosi hicho huenda kikawa na mechi ya kwanza ya kirafiki.

Simba ndiyo timu pekee nchini kwenye 'pre season' ya msimu huu ambayo imekwenda kupiga kambi barani Ulaya, ikijiandaa na michuano ya African Football League, Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara, Ngao ya Jamii, Kombe la FA na lile la Mapinduzi.

 

Azam FC - Tunisia

Azam FC ilikuwa ndiyo timu ya kwanza kuanza 'pre season' msimu huu, ikiondoka nchini kwenda Tunisia kwenye Jiji la Sousse kwa ajili ya maandalizi yake msimu ujao.

Iliondoka nchini Julai 8 ikiwa na watu wasiopungua 40, wakiwamo wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na wafanyakazi na tayari imeshacheza mechi tatu za kirafiki.

Mechi ya kwanza ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan na ikachapwa idadi ya mabao kama hayo na Esperance ya huko, kabla ya juzi usiku ikiichapa US Monastir mabao 2-1.

Ofisa Habari, Hasheem Ibwe amesema aina ya mechi wanazocheza ndiyo sababu iliyowafanya wao kusafiri kutoka Tanzania kwenda Tunisia.

"Tunacheza na timu kubwa barani Afrika ambazo zinafanya vema kwenye michuano ya kimataifa, hivyo tulihitaji kujipima nazo nguvu kwani nasi tunakwenda kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika," alisema Ibwe.

Wakati Simba ikiwa timu pekee nchini kwenda kuweka kambi Ulaya, Azam nayo ni timu pekee iliyoweka nje ya Tanzania, Tunisia.

 

Singida Fountaine Gate - Arusha

Wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye michuamo ya Kombe la Shirikisho, Singida Fountaine Gate, wao wakaamua kutoka kwao Singida kwenda kuweka kambi jijini Arusha.

"Tunaweka kambi hapa kwa siku 14, programu ya mwalimu Hans Van Pluijm ni ya wiki mbili kwa mujibu wake tukiwa hapa, baada ya hapo tutarudi Singida kwa ajili ya tamasha la Singida Day, halafu tunaanza safari ya Tanga kwenda kwenye Ngao ya Jamii," alisema Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hussein Massanza.

"Kwanza hata msimu uliopita tulifanyia mazoezi hapa hapa, kwa hiyo tuna uzoefu napo, tutafanya maandalizi yaliyokuwa mazuri pamoja na hali ya hewa yake kuwa ya baridi sana naamini mambo yatakwenda sawa tu," alisema winga wa timu hiyo, Deus Kaseke.

 

Namungo FC - Arusha

Kikosi cha Namungo chenye maskani yake mkoani Lindi nacho kikaamua kuondoka kwenye Makao Makuu yao kuelekea jijini Arusha kuweka kambi kwenye kituo cha Black Rhino Academy.

Namungo ina kazi kubwa ya kurejesha makali yake ya misimu kadhaa iliyopita, kwani haikuwa na matokeo ya kuridhisha msimu uliomalizika.

 

Mashujaa FC - Zanzibar

Hii ni timu ambayo itaanza kucheza Ligi Kuu msimu huu baada ya kupanda kwa mara ya kwanza, ikiwa na maskani yake mjini Kigoma.

Hata hivyo, imesafiri kutoka huko kwenda visiwani, mjini Zanzibar kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu.

"Tunapenda kuwataarifu kwamba, maandalizi ya msimu ujao kwa klabu yetu yatafanyikia visiwani Zanzibar," ilisema taarifa ya klabu hiyo, huku ikitajwa kuwa kocha mpya, Mohamed Abdallaah 'Bares' ndiye aliyependekeza kikosi hicho kwenda kuweka kambi huko.

 

Dodoma Jiji - Iringa

Klabu ya Dodoma Jiji, yenyewe imetoka makao makuu ya nchi na kwenda kujichimbia mkoani Iringa kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Kassim Liogope, anasema wameweka kambi mkoani Iringa ambapo pamoja na mambo mengine, hali ya hewa ya huko ni ya baridi hivyo inaruhusu wachezaji kufanya mazoezi kwa muda mrefu.

"Hali ya hewa nzuri, uwanja mzuri, yaani yale mahitaji yote ya 'pre season' tuliyokuwa tunayahitaji yamepatikana hapa na ndiyo maana tumechagua kuja Iringa, kulikuwa na sehemu kama tatu tulizipendekeza, lakini mwisho wa siku hapa ndipo tumepachagua kwa sababu kumekidhi vigezo ambavyo sisi kama benchi la ufundi tulikuwa tumependekeza vipatikane," anasema kocha huyo.