Klabu 5 zinazoweza kubadilisha makocha

04Apr 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Klabu 5 zinazoweza kubadilisha makocha

MSIMU wa 2021-22 umetoa uzoefu tofauti kwa klabu bora katika Ligi Kuu tano kubwa za Ulaya. Licha ya matarajio, shamrashamra, uwekezaji na malengo kuelekea msimu mpya, baadhi ya mambo yaliishia kukatisha tamaa.

Bado imesalia miezi kadhaa kabla ya msimu kukamilika. Hata hivyo, baadhi ya klabu maarufu tayari zimeonyesha nia ya kutaka kuboreshwa zaidi.

Baadhi bado zinatatizika kupata ushiriki wao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, huku nyingine zikiwa hazina cha kupigania.

Tunapokaribia kipindi cha mwisho cha msimu, ni kawaida kwamba klabu zinafikiria kufanya maamuzi muhimu kabla ya msimu ujao. Wale ambao wamefurahishwa na kiwango bora wakati wa msimu watakuwa wakifikiria njia za kuimarisha zaidi timu zao.

Wale waliokatishwa tamaa, watakuwa na nia ya kufanya mabadiliko makubwa upande wao. Hiyo bila shaka itasababisha makocha kadhaa kupoteza kazi zao na wengine kuzichukua.

Hapa tunaziangalia klabu tano zinazoweza kufanya mabadiliko ya makocha wakati wa msimu wa majira ya joto yanayokuja, twende sasa...

#5. Ajax

Kocha wa Ajax, Erik ten Hag hajawa na msimu mbaya. Hata hivyo, si mbaya kusema kwamba, Mholanzi huyo na timu yake wangefanya vema zaidi. Kwa sasa wanaongoza mbio za kuwania taji la Ligi Kuu Uholanzi, Eredivisie, wakiwa na pointi 66, lakini ni uongozi finyu tu kwani PSV wanafuatia kwa karibu wakiwa na pointi 64.

Timu hiyo ya Uholanzi pia imetolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya 16-bora baada ya kufungwa na Benfica kwa jumla ya mabao 3-2. Kwa mujibu wa gazeti la The Metro, huu unaweza kuwa msimu wa mwisho kwa Ten Hag katika uwanja wa Johan Cruyff Arena.

Mtaalamu huyo analengwa zaidi na klabu kubwa nyingi Ulaya Ulaya, huku Manchester United ikishika kiti cha mbele. Inabakia kuonekana ni wapi atakuwapo msimu ujao.

#4. Juventus

Massimiliano Allegri aliteuliwa tena kuwa kocha wa Juventus msimu uliopita wa majira ya joto kwa lengo la kuirejesha klabu hiyo kwenye mstari ulionyoka. Walimaliza nafasi ya nne msimu uliopita, na kushindwa kutwaa taji la Serie A baada ya mfululizo wa miaka tisa.

Hata hivyo, kwa kuzingatia mafanikio ya timu tangu wakati huo, haitakuwa mbali kusema kocha huyo hajafanya lolote kufikia matarajio yaliyotarajiwa.

'Bianconeri' hao waliondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Villareal. Mbio zao kwenye Serie A pia hazijawa bora zaidi. 'Kibibi Kizee' hicho cha Turin tayari kimetoka kwenye mbio za ubingwa na kwa sasa kinapigania kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimamo. Mambo yakiendelea hivi, kuna uwezekano mkubwa kubadilishwa kocha mwishoni mwa msimu huu.

#3. Real Madrid

Miamba hii ya Hispania iliingia msimu huu ikiwa na kiwango bora kabisa kwenye LaLiga na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Carlo Ancelotti alipata sifa nyingi baada ya timu yake kuilaza Paris Saint-Germain katika hatua ya 16-bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema mwezi uliopita.

Hata hivyo, 'Los Blancos' hao, walidhalilishwa kwa mabao 4-0 na Barcelona kwenye El Clasico mwezi uliopita katika Uwanja wa Santiago Bernabeu. Kwa hiyo, mazingira yanayomzunguka Ancelotti yamebadilika haraka. Kwa hali ilivyo, kuna hisia za kufadhaika taratibu zinakuja kwenye klabu hiyo.

Ancelotti atahitaji kufanya kila awezalo ili kuhakikisha Real Madrid wanachukua ubingwa msimu huu. Vinginevyo, kazi yake itakuwa chini ya tishio kubwa kabla ya msimu ujao.

#2. Manchester United

Manchester United wanaonekana kuzidi kuingia kwenye mgogoro. Hata kurejea kwa Cristiano Ronaldo hakujatosha kuziba nyufa pale Old Trafford msimu huu. 'Mashetani Wekundu' hao wameshindwa kutamba uwanjani.

Kwa hali ilivyo, United itamaliza msimu wake wa tano bila ya kupata medali yoyote. Tayari wametoka katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England na pia wameondolewa katika mashindano yote ya mataji msimu huu.

Ralf Rangnick alichukuliwa kuwa kocha wa muda Novemba 2021 baada ya kufukuzwa kwa Ole Gunnar Solskjaer. Kwa mujibu wa mkataba wake, raia huyo wa Ujerumani anatazamiwa kuchukua nafasi ya ushauri hapo Old Trafford baada ya msimu huu. Hata hivyo, kwa mujibu wa gazeti la The Sun, klabu hiyo ilikuwa inafikiria kumpa nafasi ya kudumu ya ukocha msimu ujao.

Lakini nafasi yake ya kuteuliwa kama kocha wa kudumu mwishoni mwa msimu huu ni ndogo sana baada ya matokeo yasiyoridhisha. Kuna uwezekano mkubwa atatoa nafasi kwa kocha mwingine kuchukua utawala kipindi cha majira ya joto.

#1. Paris Saint-Germain

Kuiona PSG wakiwa kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu Ufaransa, Ligue 1, inaonekana si kitu ila ni udanganyifu tu. Ukweli ni kwamba 'Waparis' hao wanastahimili mambo magumu chini ya kocha Mauricio Pochettino. Kwa kweli, haitakuwa rahisi kusema huu ni moja ya misimu yao ya kukatisha tamaa kuwahi kutokea kulingana na mashabiki na wadadisi.

Paris Saint-Germain italazimika kulipa takriban Euro milioni 20 kama fidia ikiwa wataachana na Pochettino na wafanyakazi wake kufutwa kazi.

Miamba hao wa Ufaransa walitarajiwa kutoa tamko barani Ulaya baada ya dirisha la usajili la majira ya joto walilokuwa nalo. Walisajili wachezaji kama Lionel Messi, Gianluigi Donnarumma, Achraf Hakimi na Sergio Ramos msimu uliopita wa majira ya joto. Lakini waliishia kudhalilishwa tena na Real Madrid katika hatua ya 16-bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Pia walitupwa nje kwenye Kombe la Ufaransa baada ya kushindwa na Nice Februari mwaka huu. PSG wanajulikana kwa kuwa na subira ndogo sana linapokuja suala la kuwaondoa makocha. Kila kitu kinaonyesha kutakuwa na mabadiliko ya kocha pale Parc des Princes katika msimu wa majira ya joto.