Hivi ndivyo unavyoifanya nyumba kuwa nyumbani

11Jun 2016
Vivian Machange
Dar es Salaam
Nipashe
Hivi ndivyo unavyoifanya nyumba kuwa nyumbani

MSEMO kuwa nyumbani kwako ndipo ulipo moyo wako ni barabara na una ukweli usiopingika.
Nyumba ni mkusanyiko wa maisha, kumbukumbu na upendo.

Kama unatafuta njia za kuifanya nyumba yako iwe nyumbani, kuna vitu rahisi na vidogo unavyoweza kufanya.

Na hii haihusishi kununua vitu vingi vya gharama kubwa.Fuatilia njia hizi ili uanze leo kuboresha makazi:

Pamba kwa picha

Kitaalam inaelezwa kuwa picha inaongea maneno elfu moja.Kuongeza kumbukumbu ya picha kwenye shelfu, juu ya meza na kuta za nyumba yako kutaifanya iwe nyumbani.Hii inaipa nyumba muonekano mpya na hisia kuwa mtu fulani anaishi hapo, badala ya kuonekana kama nyumba tu.

Pia ni njia nzuri za kuondoa hizo picha kutoka kwenye simu yako au kamera ili kuzipa lengo halisi la kuonekana.

Weka eneo la kukaa

Nyumba inageuka nyumbani pale kunapokuwa na eneo na viti vizuri vya kukaa kwa wenyeji na wageni. Kuwa na sehemu ya kutosha kwa ajili ya kukaa kutaleta mvuto wa mahali pa kuishi.

Chumba cha kulala kinoge

Jambo jingine ni hili fanya chumba cha kulala kiwe kama mahali patakatifu.

Kumbuka usingizi mzuri wa usiku ni kipaumbele kwa watu wa kila umri.

Hakikisha unapata usingizi mwororo kwa kuwa na kitanda na godoro linalofaa kwa kadri iwezekanavyo. Hii ni pamoja na malazi na mwanga wa chumba.

Usafi

Kila nyumba ina upekee wake na mahitaji tofauti kuendana na wakaaji wake.

Nyumba safi ni ile ambayo hakuna vyombo vinavyoachwa vichafu iwe ni kwenye sinki, karo, beseni, ndoo, popote pale pa kuoshea vyombo kuendana na maisha unayoishi na nguo chafu hazijazagaa kila mahali sakafuni.

Ni kujitahidi kupambana na uchafu palepale unapotokea ikiwa ni pamoja na kusafisha sakafu na kushughulikia madoa hasa palepale yanapotokea.

Nyumba safi ni nadhifu nje na ndani na kuna kanuni mlizojiwekea hapo nyumbani ili kuiwezesha kuendelea kuwa safi.

Mapambo ya msimu

Ni muhimu kwenda na wakati kwa kuiweka nyumba katika hali ya kisasa kwa mfano wakati wa sikukuu kuweka mapambo yanayoendana na msimu huo ambapo pia kunaifanya nyumba igeuke kuwa nyumbani na kuwapa hisia wanaoisherehekea sikuuku hiyo.

Usisahau misosi

Ni lazima jiko litumike kuwe na mahanjumati hasa.Hapa ina maana kuwa ndani ya nyumba kupikwe. Kuna baadhi ya nyumba ambazo hakupikwi, ni watu wa kula barabarani tu.

Ili nyumba yoyote ile igeuke kuwa nyumbani ni muhimu sana kuwe na chakula kila wakati. Jiko linapotumika kuandaa vyakula na harufu yake nzuri inaifanya nyumba kuwa na uhai wa kuitwa nyumbani.

Zaidi tembelea www.vivimachange.blogspot.com