HIFADHI KITULO NA UPEKEE WAKE;

31Mar 2023
Na Mwandishi Wetu
MBEYA
Nipashe
HIFADHI KITULO NA UPEKEE WAKE;
  • • Vivutio maua, ndege wanaosafiri kutoka Ulaya • Ukingoni mwa milima alikopita Dk. Livingstone

NI kilomita 110 kutoka jijini Mbeya kuelekea Kusini Mashariki inakopatikana Hifadhi ya Taifa Kitulo, maarufu Bustani ya Mungu.

Aina ya maua na mandhari, kivutio cha watalii kuyafuata Kitulo, kutoka safari ya mbali ughaibuni

Mahali hapo panaunganisha vilele vya milima Kipengere, Uporoto na safu za milima ya Livingstone alikopita Dk. David Livingstone, ikiundwa na mipaka ya wilaya za Makete (Njombe), Rungwe na Mbeya Vijijini (Mbeya).

Kijiografia, pana baridi sana ikielezwa miezi Desemba na Aprili, pia Juni hadi Agosti, hufikia nyuzi joto sifuri na katika hali ya kawaida, huwa nyuzi joto saba. Utajiri wa mvua nao upo, Oktoba hadi Mei, ni wastani wa milimita 1,500 hadi 1,700.

Ukubwa wake ni kilomita za mraba 412.9 ndani ya mwinuko kati ya mita 2,100 hadi 3,000, ikiwa ni hifadhi ya kwanza barani Afrika mahsusi kwa ajili ya kutunza mimea, hasa jamii ya maua.

Mkuu wa Hifadhi Kitulo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Theodora Batiho, anatoa historia, awali palijulikana Elton Plateau, baada ya kugunduliwa na mtafiti Fredrick Elton, aliyepita hapo mwaka 1870.

Anasema, mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), lilichukua eneo hilo kulimia ngano na kufuga kondoo. Baadaye, paligeuzwa shamba la ng’ombe ambalo, mradi unadumu hadi sasa.

KULIVYOTANGAZWA HIFADHI

Mkuu huyo anasema, hatua za kupafanya Hifadhi ya Taifa zilianza mwaka 2002 na kufanikishwa 2005, akimtaja mhifadhi wake wa kwanza, William Mwakilema, ambaye sasa ni Mhifadhi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Ziara ya mwandishi hivi karibuni, alishuhudia uzuri wa hifadhi yenye aina 45 za maua, huku baadhi yake yanapatikana hifadhini Kitulo peke yake duniani, yakiwa na tabia ya kuchanua kila mwezi Novemba hadi Aprili kila mwaka.

NDEGE WAHAMIAJI

Theodora anasema kuna ndege aina ya Great White Stork (abdmin stork) wenye uwezo wa kuruka kutoka eneo la Ulaya Mashariki na wengine kutoka Afrika Kusini, wakisafiri umbali kilomita 7,000 kwa siku 322. Wana kawaida ya kutaga na kuangua mayai mengi, kabla ya kuanza safari ndefu.

Ofisa Uhifadhi Daraja la Kwanza - Utalii, Susan Tesha, anafafanua sababu ni mazingira yake salama na rafiki kwao kuzaliana, huku chakula ni kingi, pia hifadhini Kitulo, kunapatikana ndege wengine kama vile Blue Swallow wanaotumia hifadhi kama makazi yao ya misimu.

Anataja kuwapo aina za nyani Kipunji, waliogunduliwa mwaka 2003, pundamilia walioletwa kutoka Hifadhi ya Taifa Mikumi na swala kutoka Ruaha.

Hao anawataja kuendana na vipepeo wanaosaidia kuchavusha maua, vinyonga, mijusi na vyura, wote wakiongeza utajiri wa kibailojia hifadhini Kitulo, wakiishi kwenye uwanda tambarare, mabonde,vilima na maporomoko ya maji na mabwawa, yanachangia maji yake kwenye Mto Ruaha Mkuu, tegemeo kwa Hifadhi ya Taifa Ruaha, mabwawa ya kuzalisha umeme ya Mtera mkoani Dodoma na Kidatu, Morogoro.

Susan anasema, ni ukanda wa mvuto, upepo mzuri unapopambwa na sauti za ndege unaofariji masikio yao, akiwa katika mahali anapashudia   vizuri bondeni, Mlima ya Rungwe, Ziwa Nyasa na milima Livingstone, pia maporomoko yanayozalisha maji Mwakilema na Mwakipembo.

KUNAVYOFIKIKA

Anasema, Kitulo kunafikika kirahisi mtu akitokea Mbeya Mjini umbali wa kilomita 110, vilevile umbali wa kilomita 70 kutoka Igawa wilaya ya Mbarali au mjini Makete, huku akishauri muda mzuri kuzuru mandhari ya maua yanayochanua, ni kuanzia Desemba hadi Aprili, huku utalii wa kupanda milima ni kuanzia Juni hadi Agosti, penye baridi kali.

Mwandishi wa makala, aliyekutana na mtalii kutoka Hispania, Marc Antillachraia, anaeleza kilichomvutia Kitulo ni mimea, maua, viumbe na maporomoko ya maji, ikiwa sehemu ya maeneo alikonuia kuzuru barani Afrika, akiahidi kuwa balozi mzuri wa hifadhi hiyo, atakaporudi kwao.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mafiga, kijiji jirani cha Missiwa, wilayani Makete, Laynada Mwasanga, anasema hivi karibuni walipeleka wanafunzi hifadhini Kitulo, kuona uzuri wa maua, mimea na wanyama. Shule iko jirani, ila wanafunzi walikuwa hawajawahi kutembelea.

Ni hatua kama hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kinyika wilayani Makete, Faida Ngulo, naye karibuni alipeleka wanafunzi hifadhini kujifunza na kuburudika na vilivyomo.

MATATIZO YAKE

Kamishna Theodora anasema, hadi sasa wanakabiliwa na shida kadhaa, ikijumuisha kiwapo miundombinu duni ya vumbi kufika hifadhini Kitulo na wakati wa mvua hali inakuwa ngumu zaidi.

Vilevile kuna utata wa wakulima kuvamia maeneo ya Hifadhi Kitulo akinyoosha wengine kuingia kuchimba viazi mahali hapo. Hapo anasema “tunaomba barabara hizi ziboreshwe kwa kuwekewa lami zitatusaidia kuongeza idadi ya watalii.”

Anadokeza kwamba, serikali iko katika hatua ya kujenga barabara kiwango cha lami kutoka Makete Mjini, kupita hifadhini Kitulo hadi Mbeya, akisema itawafungulia watalii wengi zaidi.

Lingine analitaja ni mwitikio mdogo wa wawekezaji wa hoteli ndani na kando ya hifadhi, kuwezesha watalii kupata pa malazi.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi Kanda ya Kusini, Steria Ndaga, anakiri kufahamu tatizo hilo, pia ujenzi wa barabara ya lami, Makete hadi Mbeya.

Anataja matatizo mengine ya hifadhi kanda yake; Ruaha, Katavi ambako kunaongoza kwa uvamizi, kuliko Kitulo. Ndaga anasema wamekuwa wakiyakabili kwa hatua za kisheria zilizoko, hata imesaidia kupunguza uvamizi huo.

MIKAKATI WAENDAKO

Kamishna Msaidizi Theodora, anataja kuna mikakati ya miaka mitano kukuza utalii hifadhini ni Kitulo, ni kujenga nyumba za kulala wageni na kuitangaza Hifadhi ya Kitulo kupitia maonyesho.

Mingine ni kuelimisha wanafunzi shule za msingi na sekondari jirani kuhusu uhifadhi, ikiwa njia ya kuwapandikizia uzalendo wanaoishi kando ya hifadhi. Hadi sasa tayari baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi Mafiga na Matamba, pia sekondari za Matamba na Kinyika, wilayani Makete wameshatembea hifadhi kuona vivutio.

Anasema, wanaendelea kuhamasisha wanaoishi kando ya hifadhi kutembelea na hadi sasa kuna mafanikio, kundi la wanawake 40 walizuru Desemba 2022 mwaka jana.

Mkakati mwingine ni kuanzishwa utaratibu, wageni kubebwa na punda na farasi hifadhini, utalii wa kutumia baiskeli, pia kuanzishwa mashindano ya mbio za masafa marefu yaani ‘Kitulo Marathon’.

Vilevile anataja matarajio ya utalii wa maombi, waumini wa madhehebu mbalimbali wakifika na kufanya maombi katika maeneo tulivu ya hifadhi, ikiwamo milima midogo na mikubwa iliyopo.

Maharusi nao sasa kupewa fursa kutembelea hifadhi hiyo, kwa ajili ya kupiga picha na kumpumzika wakati wa ‘fungate’ wakitangaza vivutio kwa kutumia mabango.