Miaka miwili iliyopita Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wakati huo akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, aliwahi kutangaza eneo la Ihumwa kuwa ndiko yatakapojengwa makao makuu ya serikali na kuahidi kuwa mkoani Dodoma, limetengwa eneo la kuwazika viongozi wakuu wa kitaifa, lakini hadi sasa haijaidhinishwa bajeti ya kufyeka na kuandaa eneo la kujenga ofisi hizo.
Pengine ni kutokana na historia yake kuwa mkoa huo ni jangwa na unakabiliwa na uhaba wa maji, jambo linalosababisha wizara na taasisi za umma kusita kuhamishia shughuli zake Dodoma mji ulio kilometa 450, magharibi ya Dar es Salaam.
Jitihada nyingi zimefanyika katika kuufikishia maji kwenye mji huo, ambao taasisi pekee iliyohamia na kuendesha shughuli zake ni Bunge. Mwaka 1998, unaandika historia ya kuboresha sekta hiyo kwa kuanzisha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (Duwasa), iliyoanza kwa lengo la kuendeleza, kusambaza, kufuatilia na kuboresha huduma hiyo.
Duwasa iliyokuwa ikitegemea ruzuku ya serikali kuendesha shughuli zake kwenye uwekezaji, kutafuta na kuendeleza vyanzo vya maji, miundombinu, mishahara ya watumishi, kushughulikia maji taka na umeme, ilifika wakati ikaanza kujiendesha yenyewe.
Julai mwaka 2003, ilianza kujitegemea kwa asilimia 100 hasa katika gharama za uendeshaji, matengenezo na sehemu ya uwekezaji.
UPATIKANAJI MAJI
Leo hali ya upatikanaji maji huko Dodoma ina sura nyingine kama ambavyo Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, David Pallangyo, anavyoieleza Nipashe, akianza na mambo yalivyokuwa hapo awali.
Anasema huduma ya majisafi ilikuwa chini ya Mhandisi wa Maji wa Mkoa, ambaye alikuwa akisambaza huduma hiyo kwa wateja na kwamba ilianza kuzorota jambo lililoifanya kuhamishiwa katika Idara ya Maji Ofisi ya Mkurugenzi wa Maendeleo wa Mkoa, lakini gharama za uendeshaji na matengenezo zikibebwa na serikali kuu.
“Huduma ya maji ilitolewa bila ya mikakati na msisitizo wa kuilipia jambo lililoigharimu idara kwa kuwa ilikuwa inawekeza, kuendesha na kusambaza maji bila wateja kulipia gharama za uendeshaji, hivyo ikaamuliwa kuanzisha Duwasa kwa lengo la kusimamia utoaji wa huduma za majisafi na uondoaji wa majitaka,” anaongeza Pallangyo.
Kuzorota kwa huduma hiyo kulisababisha kuwapo mgao wa mara kwa mara wa maji na mwaka 2002 hali ilikuwa mbaya jambo lililosababisha baadhi ya maeneo kupata maji mara moja kwa wiki na kuibua malalamiko ya wateja.
“Kipindi kile kulikuwa na kilimo cha umwagiliaji kilichofanyika jirani au kando ya njia ya bomba kuu la kusafirishia maji kutoka Mzakwe kwenda mjini, hivyo asilimia 80 ya maji yaliishia kwenye kilimo cha zabibu, bustani na migomba hivyo kuongeza matumizi makubwa ya maji,” anaongeza Pallangyo.
Kadhalika anasema awali uwezo wa uzalishaji maji kutoka chanzo cha Mzakwe ulikuwa mita za ujazo 24,000 kwa siku ukihudumia wateja 4,800 lakini pia, mfumo wa majitaka ulikuwa chini ya Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) hadi 2002 ulipokabidhiwa kwa Duwasa, hivyo nao ukiendesha shughuli zake kwa utaratibu uliokuwa unasimamiwa na mamlaka hiyo.
Akizungumzia mapato baada ya Duwasa kulazimika kujiendesha, anasema yalikuwa Shilingi milioni 14 kwa mwaka kutoka kwa wateja 800, waliokuwa wakilipia maji kwa uaminifu.
Hali hiyo, ilitishia zaidi upatikanaji wa maji na kuwahofisha wawekezaji ndiyo maana, mkoa huo ulianzisha Duwasa na kuweka mikakati ya kuzuia matumizi ya majisafi kwa kilimo.
Dodoma ilikamilisha mpango wa kufunga mita kwa watumiaji wa maji ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa kulipia kulingana na matumizi, kazi iliyokamilika mwaka 2003, hatua iliyosaidia kuboresha huduma na kupunguza migao na kuwapatia wateja huduma ya uhakika.
MAJI SAFI
Kwa upande wake Hamzah Bwanguzo, Mhandisi wa Uzalishaji Maji, Duwasa, anasema mwaka 2002-2003 ulifanywa utafiti kuhusu mahitaji ya maji kwa mji wa Dodoma.
Utafiti huo ulibainisha kiasi cha maji yaliyohitajika ambayo ni mita za ujazo 46,000 kinachojumuisha mahitaji ya Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) ambayo ni mita za ujazo 4,000 kwa siku.
Bwanguzo anaeleza kuwa licha ya mahitaji kuwa makubwa lakini chanzo pekee cha maji hayo ni visima 24, ambavyo vitano kwa ajili vya kuchunguza mwenendo wa maji ardhini vilivyo katika bonde la Makutupora, na kwamba, kwasasa uwezo wa visima hivyo ni kusafirisha mita za ujazo 61,500 ikilinganishwa na mita za ujazo 24,000 za mwanzo.
UTUNZAJI WA CHANZO
Bwanguzo, anaeleza kwamba mwaka 2000 serikali ilifanya tathmini ya kulipa fidia wananchi waliokuwa wakiishi bonde la Makutupora kazi ilighramu Shilingi milioni 590 zilizofidia kaya 2,048, mwaka 2002.Kadhalika mwaka 2007 ilihamisha vijiji vya Mzakwe, Gawaye, Mchemwa na Mamba kutoka kwenye bonde hilo.
Anasema usambazaji wa maji unategemea mabomba makuu mawili yanayosafirisha maji kutoka Mzakwe, hadi mjini yenye uwezo wa kubeba zaidi ya mita za ujazo 60,000 kwa siku.
“Mfumo wa kusambazia majisafi una urefu wa kilometa 397, ambao unajumuisha matangi mawili yenye ukubwa wa mita za ujazo 36,000 kila moja na mengine manane yenye mita za uajzo 20,030, ambayo huhifadhi na kusambaza maji.
Alisema hadi sasa Duwasa inahudumia wateja 32,000 wa majisafi kwa mgawanyo wa wateja wa majumbani kwa asilimia 94, taasisi kwa asilimia 2.7,wafanyabiashara asilimia 2.7 na wateja wa magari asilimia 0.6.
UBORESHAJI HUDUMA
Mwenyekiti wa Bodi ya Duwasa, Balozi Job Lusinde,ambaye, anasema kuanzia Januari, 2013 hadi Aprili 2015, mamlaka hiyo imeboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi na kwamba mradi huo umegharimu Dola milioni 49.623 (karibu sawa na Shilingi bilioni 23 kwa wakati huo) ambazo zilikuwa mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Korea kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF).
Anaongeza kwamba mradi huo umeongeza uzalishaji na usafirishaji wa maji kutoka kwenye chanzo cha Mzakwe kwa wastani wa mita za ujazo kutoka 32,000 kwa siku hadi kufikia 61,500.
CHANGAMOTO
Licha ya mafanikio hayo Lusinde anasema Duwasa inatatizwa na ofisi za serikali kushindwa kulipia ankara za maji kwa wakati hivyo kukwamisha jitihada za mamlaka hiyo kujitanua na kuendeleza kazi zake.“Mpaka kufikia Desemba, mwaka jana Duwasa inadai Shilingi milioni 800 kutoka taasisi za serikali pekee, hali hiyo inafanya mamlaka ishindwe kufikia malengo inayojiwekea,” anasema Lusinde.
Aidha mfumo wa kusambazia maji hautoshi kwani hadi Februari, mwaka huu una urefu wa kilometa 396 ikilinganishwa na mahitaji ya zaidi ya kilometa 478.
“Gharama za umeme kwa ajili ya mitambo ya kuzalisha na kusukuma maji ni kubwa kwani mpaka sasa zimefika milioni 340 kwa mwezi,” anaongeza Lusinde.
NINI KIFANYIKE
Kwa kutumia fedha za ndani, Duwasa imetenga bilioni 1.1 katika bajeti ya mwaka 2015/2016 ili kufikisha huduma ya maji kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa. “Ndiyo maana tunaona serikali inapaswa kuangalia uwezekano wa kuisaidia Duwasa iweze kupata umeme wa uhakika ili kutoa huduma hiyo kwa viwango na mahitaji ya wateja kwa ufanisi zaidi. Tena tunahitaji taasisi kuwajibika kulipa Ankara bila kusukumwa kwa vile maji ni moja ya mahitaji muhimu kwa wanadamu, wanyama na mimea. Lakini pia uwekezaji wake ni wa gharama kubwa,” anaongeza Lusinde.










