Democrat ina wagombea wawili, mwanamama Hillary Clinton, ambaye ni mke wa zamani wa rais wa 42 wa taifa hilo kubwa duniani, Bill Clinton, na Seneta wa sasa wa Vermont, Bernie Sanders.
Kwa upande wake chama cha Republican, wamebakia wagombea urais wanne miongoni kati ya 14 waliokuwapo.
Hii ni baada ya wengine kuachia ngazi kutokana na ‘upepo’ kuwaendea vibaya katika kampeni zao, na kwenye kura za awali za uteuzi zilizofanyika majimbo ya mwanzo.
Mgombea wa mwisho kujitoa alikuwa ni daktari bingwa wa upasuaji ubongo, Ben Carson ambaye ndiye alikuwa mgombea pekee Mmarekani, mwenye asili ya Afrika.
Wagombea waliobaki kwenye mbio hizo za kusaka kura za uteuzi zinazoendelea katika majimbo mbalimbali, ni pamoja na kinara Donald Trump, anayepambana kwa karibu na Ted Cruz, Marco Rubio na Gavana wa jimbo la Ohio, John Kasich.
Hata hivyo, katika mbio hizo, macho ya watu wengi ndani na nje ya Marekani, yamevutika kumfuatilia mgombea kinara wa Republican, ambaye ni Trump.
Wagombea walianza mbio hizo kwa kutangaza nia na baadaye wakaingia katika kura za uteuzi.
Mgombea huyu ambaye kimsingi siyo kada ndani ya Republican, na anayeonekana na ‘wenye chama’ ama wahafidhina kama mtu wa nje, ameshangaza wengi.
Ameshangaza wengi kuanzia kwa wahafidhina, wagombea wenzake ndani ya Republican na wagombea wa chama cha Democrat.
Lakini pia amewashangaza wananchi waliokuwa wakihudhuria mikutano yake ya kampeni, waliokuwa wakimfuatilia kwenye vyombo vya habari, magazeti, redio, televisheni na kwenye mitandao ya kijamii.
Kuna sababu nyingi zilizofanya awashangaze wengi, lakini baadhi ni pamoja na lugha na misimamo ambayo amekuwa akiitumia na kuionyesha kuanzia kipindi cha kampeni zake, mpaka nyakati hizi za kura za uteuzi zinazoendelea katika majimbo mbalimbali nchini humo.
Trump amekuwa na lugha kali, isiyo na staha na yenye ubaguzi wa moja kwa moja, kwa watu, kutokana na rangi na imani za kidini.
Amekuwa na lugha isiyo na staha kuanzia kwa wananchi wa taifa hilo analotaka kuliongoza.
Na hii ilijidhihirisha hasa pale alipomponda mmoja wa mgombea mwezake wa urais ambaye alikuwa mwanamke.
Huyu ni mwanamama Carly Fiorina, aliyejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho Februari 10, 2016, baada ya kuona ‘kina cha maji’ kinakuwa kirefu.
Katika moja ya mahojiano aliyoyafanya mwaka jana na jarida la Rolling Stone, Trump alimponda Fiorina kuwa na sura mbaya, isiyostahili kwa rais wa Marekani.
“Hebu angalia sura hiyo, hivi kuna mtu anayeweza kuipigia kura? hivi unaweza kufikiri kwamba sura hiyo inaweza kuwa ya rais ajaye?! Alisema na kuongeza;
“Ninachomaanisha, ni mwanamke na sipaswi kusema mambo mabaya, lakini jamani, hivi tuko makini kweli?”alisema.
Lakini katika mlengo huo huo wa namna kinara huyo alivyo na lugha za kuchukiza, ni jinsi alivyowageukia jirani zake Wamexico na kuwang’ong’a.
Trump alinukuliwa akiwaponda wananchi wa taifa hilo kwa kuleta shida ndani ya Marekani.
Aidha, akasema, iwapo atachaguliwa, atahakikisha anajenga ukuta mkubwa kwenye mpaka wa nchi hizo, ili kuwazuia wananchi wa Mexico wasiingie Marekani.
“Mexico inapoleta watu wake Marekani, haileti watu wazuri, bali wale wenye matatizo mengi, na wanakuja na matatizo hayo kutuletea sisi… Wanaleta dawa za kulevya, wanaleta uhalifu, ni wabakaji, nadhani siyo watu wema,” alisema.
Kikubwa ni pale alipotaka kuzuiwa kwa waslamu wote, kuingia ndani ya taifa hilo.
Alitoa wito huo, baada ya mauaji yaliyotokea San Bernardino, California, yaliyodaiwa kufanywa na mtu aliyetuhumiwa kuwa na mapenzi na kundi la Kigaidi la Islamic State (IS).
Msimamo wake huo umelaaniwa na watu wengi ndani na nje ya Marekani, wakiwamo wagombea wenzake.
Hizo ndizo baadhi ya lugha na misimamo ya Trump, iliyowashangaza na inayoendelea kuwashangaza wengi ndani na nje ya Marekani.
Lakini kitu cha ajabu na kinachoendelea kuwashangaza zaidi wengi ni kuwa, pamoja na lugha na misimamo hiyo ya kibaguzi ya wazi na isiyo na kificho aliyoionyesha kinara huyo, bado ndiye anayeongoza kwa kupigiwa kura na wanachama hadi sasa katika majimbo yaliyofanya kura za uteuzi.
Kati ya viti vya uwakilishi 1,237, vinavyotakiwa kwa mgombea ili aweze kuteuliwa na Republican, tayari Trump ana viti 460, akifuatiwa na Cruz, viti 369, Rubio 163, na Kasich 63.
Hali hiyo inashangaza kwa sababu tungetarajia kuwa kutokana na maneno yake makali na wakati mwingine yasiyo na staha, na misimamo yake mikali na wakati mwingine isiyo na maana, basi wapiga kura wangemtosa, walau katika majimbo yaliyopiga kura.
Na hoja hii inatiwa nguvu na ukweli kuwa, hata baadhi ya wagombea wenzake ndani ya Republican, wameshaanza kuona athari za lugha na misimamo hiyo mibaya kwa chama chao.
Hata hivyo, pengine ni bora tukapongeza wasiwasi wa wazi alioonyesha Rubio juzi dhidi ya maneno na misimamo ya kushangaza ya kinara huyo.
“Maneno mara nyingi yana athari zake,” alisema.
Na hii ni baada ya waandamanaji kuvamia na kuvunja mkutano wa kampeni wa Trump, jijini la Chicago, na kusababisha uahirishwe, kwa sababu za kiusalama.
“Nadhani tunapaswa kuangalia lugha inayotoka kwa Trump, kwani mtu anayewahimiza watu kwenye umati kumpiga mtu yeyote anayempinga, itasababisha nchi yetu kugawanyika,” anasema.
Jumamosi iliyopita, Trump aliwahimiza wafuasi wake kuwapiga waandamanaji waliokuwa wakimpinga, na akaahidi kulipa ada ya kisheria iwapo watapelekwa mahakamani.
Pengine ni wakati wa wanachama wa Republican kuamua sasa na si wakati mwingine, iwapo wanataka kuendelea kuwashangaza watu kwa kumpatia ushindi na hatimaye uteuzi bingwa huyo wa ubaguzi ama la.
Kama alivyosema Rubio, vinginevyo dunia ijiandae kukutana na kushuhudia dikteta mwingine wa tatu kuonekana.










